12/9/16

BREAKING NEWS: YANGA YATAKIWA KUILIPA SIMBA FIDIA YA SH MILIONI 50 KWA KUMSAINI KESSY KINYUME NA UTARATIBU

Baada ya kupitia mawasilisho ya pande zote kwa njia ya mahojiano, na vielelezo Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji imebaini mambo yafuatayo ambayo yanapaswa kuchukuliwa hatua za haraka:
1. Mchezaji Hassan Hamis Ramadhan au Hassan Kessy alikuwa na Mkataba na Klabu ya Simba uliokuwa unaishia tarehe 15/06/2016.
2. Young Africans SC walikiri mbele ya Kamati kupeleka jina la Mchezaji Hassan Ramadhani Kessy huko Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) tarehe 10/06/2016 huku mchezaji huyo akiwa ndani ya mkataba na klabu ya Simba.
3. TFF kupitia Sekretarieti yake ilikuwa na nafasi ya kuweza kuielekeza Young Africans SC hatua stahiki za kuchukua ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Klabu ya Simba kama taratibu zinavyoelekeza. Kama hatua hii ingechukuliwa kwa wakati mwafaka mgogoro huu usingekuwa na sura ya sasa na pengine usingekuwepo.
4. Simba SC walileta machapisho yanayotokana na Mtandao/blog wa mtu waliomtaja kuwa ni Bin Zubeiry ukimwonyesha Mchezaji yuko na viongozi wa Young Africans.
5. Young Africans SC ilionesha Mkataba iliosainiwa na Hassan Hamis Kessy tarehe 20/6/2016 na hivyo hakukuwa na sababu ya msingi ya kufanya mambo yaliyoainishwa kwenye kipengele cha 2 na cha 4 kabla ya kumalizika kwa mkataba kati mchezaji Haasan Kessy na Klabu ya Simba.
6. Bila kuathiri hadhi ya Uanachama wengine wa TFF, Klabu ya Simba ni brand kubwa kama ilivyo Klabu ya Young Africans, umakini mkubwa unapaswa kutumika katika kushughulikia brand hizi ili kuepuka madhara yasiyokuwa ya lazima.
HATUA
Kitendo cha Klabu ya Young Africans kupeleka jina la mchezaji wa klabu nyingine CAF huku mchezaji huyo akiwa ndani ya mkataba na mwanachama mwingine wa TFF ni kosa kubwa kwa mujibu wa kanuni za ligi kifungu 69[5] ambalo linapaswa kupewa adhabu itakayopelekea wanachama wote kuheshimu nafasi ya TFF kwenye suala la usajili na sio kuanza kwenda CAF au kwingineko ili kulinda integrity ya soka la Tanzania.
Klabu ya Young Africans inatozwa faini ya Sh 3,000,000 (Sh milioni tatu) kwa mujibu wa kanuni na fidia kwa klabu ya Simba ya Sh 50,000,000 (Shilingi milioni hamsini).
Ofisa wa TTF aliyehusika ama kwa kushirikiana na Uongozi wa Klabu ya Young Africans au kwa kutochukua hatua stahiki kwa wakati apelekwe kwenye mamlaka yake ya nidhamu, yaani, Katibu Mkuu wa TFF ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Share:

AZAM KUVIPIMA VIFAA VYAKE VIPYA KWA MTIBWA SUGAR JUMAMOSI HII CHAMAZI

Katika kujiandaa vilivyo kuelekea mechi za raundi ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Klabu ya Azam FC, inatarajia kukipima kikosi chake kwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Jumamosi ijayo Desemba 10 saa 1.00 usiku.
Azam FC iliyoanza maandalizi ya mzunguko huo wa pili Jumatatu iliyopita, itautumia mchezo huo kuwapima wachezaji wake kabla ya kuanza mikikimikiki ya ligi, ambapo inatarajia kufungua pazia kwa kucheza na African Lyon Desemba 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Baadhi ya wachezaji wapya itakaowatumia katika mchezo huo ni washambuliaji Yahaya Mohammed (Aduana Stars) na Samuel Afful (Sekondi Hasaacas), ambao wametua nchini alfajiri ya leo Jumatano wakitokea nchini kwao Ghana sambamba na beki wa kati, Yakubu Mohammed (Aduana Stars) aliyekuja kufanya majaribio ya kujiunga na Azam FC.
Mabingwa hao wanawafanyia majaribio wachezaji wengine wawili kutoka Cameroon, beki wa kati Batetakang Flavius (Canon Yaoundé) na kiungo mkabaji Stephane Kingue (Coton Sport FC de Garoua), ambao nao wanatarajia kuwemo kwenye mtanange huo.
Hadi inamaliza raundi ya kwanza ya ligi, Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachochangamsha mwili na kuburudisha koo pamoja na Benki bora kabisa nchini kwa sasa ya NMB, imejikusanyia jumla ya pointi 25 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa nyuma pointi 10 dhidi ya Simba (35).
Mbali na kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi, Azam FC pia inayatumia mazoezi hayo kujiandaa ipasavyo na michuano mingine ya Kombe la Mapinduzi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la Shiikisho Afrika (CC), ili iweze kufanya vizuri.
Share:

Vanessa Mdee Kuigiza Tamthilia ya MTV Base


BAADA ya kumaliza mwaka na wimbo wa ‘Cashmadame’, mkali wa muziki Afrika Mashariki, Vanessa Mdee, mwakani ataanza kuonekana kwenye tamthilia ya Shuga iliyochezwa nchini Afrika Kusini.
vanessa33
Msimu wa tano wa tamthilia hiyo unaanza Machi mwakani ambapo Vanessa Mdee kutoka Tanzania atashirikiana na wasanii wengine kutoka nchi mbalimbali katika kunogesha msimu huo wa tamthilia hiyo.
“Nafurahi mwaka huu naumaliza vizuri na wimbo wangu wa ‘Cashmadame’ lakini mwakani Mungu akipenda nitauanza tena vyema kwa kuwa nimechaguliwa na MTV Base nishiriki katika tamthilia ya Shuga kwa msimu wa tano, ni mafanikio makubwa kwangu na kwa taifa langu na hii ndiyo itakuwa tamthilia yangu ya kwanza kuwahi kuigiza,” alieleza Vanessa.
Tamthilia hiyo anayokwenda kushiriki Vanessa ina umaarufu mkubwa kutokana na watu wengi maarufu kuwahi kushiriki, akiwamo mshindi wa tuzo ya Oscar mwaka 2014, Lupita Nyong’o kupitia filamu ya‘Twelve Years a Slave’.
Mtanzania
Share:

Vijana zaidi ya 2,500 nchini watengewa mabilioni


Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni 15 kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana zaidi 2,500 ili kuwajengea uwezo waweze kushiriki kama nguvu kazi kwenye viwanda vinavyotarajiwa kujengwa nchini.
Baadhi ya vijana wa kitandani katika maadhimisho ya siku ya vijana duniani

Alitoa kauli hiyo jana usiku kwenye sherehe za utoaji wa tuzo ya muajiri bora wa mwaka 2016, zilizofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, tuzo ambazo zimeandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE).
Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kujielekeza katika kutoa mafunzo kwenye sekta za kipaumbele kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo kama kilimo biashara, mafuta, gesi, utalii, usafirishaji, ushonaji na bidhaa za ngozi.
Alisema jitihada zinaendelea kwenye maeneo mengine ili waajiri wawe na wigo mpana wa kuwapata wafanyakazi wenye stadi stahiki kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa wao kuwa nguvu kazi yenye ujuzi na umahiri mkubwa kwa lengo la kuongeza tija.
Share:

Rais Magufuli ataja mambo yanayoikwamisha Tanzania


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameitaja rushwa kama changamoto sugu ambayo bado inaendelea kulitafuna taifa la Tanzania katika miaka yake 55 ya Uhuru.
Rais John Magufuli
Rais Magufuli ameitaja changamoto hiyo leo akati akiwaongoza watanzania katika maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru wa Tanzania Bara ikiwa ni mara ya kwanza tangu aingie madarakani na kutaja changamoto nyingine kuwa ni tatizo la ajira pamoja na umasikini.
Akizungumza katika hotuba yake ya shukrani katika maadhimisho hayo ambayo yamefanyika katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam, Dkt. Magufuli, amesema kuwa serikali yake itaendelea kupambana na vitendo na rushwa na ufisadi, kwa ajili ya kuliletea taifa maendeleo.
Aidha Rais Dkt. Magufuli amesema kuwa serikali itahikisha kuwa inaondoa uonevu hasa kwa wananchi wanyonge ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili ili kila mtanzania aweze kufaidika na matunda ya nchi yake.
Maadhimisho hayo ambayo kwa mujibu wa Rais Magufuli ndio ya mwisho kufanyika Jijini Dar es Salaam na kuanzia mwakani yataadhimishwa Dodoma, yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wastaafu na serikali pamoja na mabalozi wa nchi mbalimbali zenye uwakilishi hapa nchini.
Share:

Serikali kupangua sheria zinazokwamisha uwekezaji

Serikali imesema inazitambua changamoto zinazowakabili waajiri nchini ikiwemo uwepo wa tozo mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka tofauti za Serikali kwa huduma ileile, na kusema itazifanyia mapitio sheria zinazoweka changamoto hizo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa tayari mchakato wa kuainisha sheria zote zinazoonekana kukwamisha uwekezaji pamoja na mazingira ya biashara nchini umeanza.
Ametoa kauli hiyo jana usiku kwenye sherehe za utoaji wa tuzo ya muajiri bora wa mwaka 2016, zilizofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam. Tuzo hizo zimeandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE).
“Lengo letu ni kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini ili yaweze kuvutia zaidi na mchakato huu unashughulikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango. Tunaomba mvumilie na mshirikiane nasi katika kuendelea kuziainisha sheria zinazokwaza biashara ili tuweze kuzijumuisha kwenye mapitio hayo,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwashauri waajiri wote nchini waendelee kufanyakazi zao kwa mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima mahala pa kazi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk. Aggrey Mlimuka alisema lengo la uaandaji wa tuzo hiyo ni kutambua wanachama wenye sera nzuri za usimamizi wa rasilimali watu katika taasisi na makampuni mbalimbali mwanachama hapa nchini.
Dk. Mlimuka alisema kuwa tuzo hio pia ilijikita zaidi katika kuangalia maeneo muhimu ya rasilimali watu, uongozi, utawala, usimamizi wa Rasilimali watu, kusaidia jamii pamoja na kuwajibika katika jamii, ubora na uzalishaji.
Share:

Video: Rais Dk Magufuli akitembea kama mwanajeshi baada ya kukagua gwaride

Leo Desemba 9 Tanzania Bara imeazimisha miaka 55 tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa wakoloni mwaka 1961. 
Maadhimisho hayo yamepambwa na shughuli mbalimbali za kijeshi lakini pia ngoma za asili kutoka kwa makundi mbalimbali.

Mbali na mambo hayo yaliyoonekana kuwavutia wengi, jambo lingine lililowafurahisha ni pale Rais Dk Magufuli alipoamua kutembea kiukakamavu kama mwanajeshi mara baada ya kumaliza kukagua gwaride katika maadhimisho haya ya 55 ya uhuru.

Hapa chini ni video ra Rais Dk Magufuli akitembea kiukakamavu baada ya kukagua gwaride katika sherehe za uhuru
Share:

Advertisment

Habari Mpya

Follow us on Facebook

Popular Posts

Blog Archive

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger Design by Yuvinusm