4/27/16

Bomoabomoa Yatua Moshi

 
Ubomoaji wa majengo yaliyojengwa kinyume na sheria za mipango miji katika Manispaa ya Moshi unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Ubomoaji huo unakusudiwa kuambatana na uvunjaji wa vibanda zaidi ya 20 vya Chama cha Mapinduzi (CCM) vilivyopo katika Kata ya Mawenzi.
Meya wa manispaa hiyo, Raymond Mboya amewaambia waandishi wa habari kuwa wanatarajia kusimamia ipasavyo sheria hiyo ili kuhakikisha majengo yaliyojengwa kinyume na sheria yanavunjwa.
Mboya amesema sheria ni lazima ifuatwe haijalishi ni chama gani kimejenga kinyume.
“Leo tunapata ugumu wa kuwa jiji kutokana na sisi wenyewe kushindwa kusimamia sheria za mipango miji, hatuwatendei haki wakazi wa Manispaa ya Moshi ni lazima ifike wakati watu tujue kuna mamlaka ambayo imekabidhiwa kusimamia mji,”amesema Mboya.
Akizungumzia uharibifu wa miundombinu ya barabara kutokana na mvua zilizonyesha, amesema baadhi ya watu wamekuwa wakisema barabara zilijengwa chini ya kiwango, jambo ambalo siyo la kweli.
“Mfano barabara ya Nakumatt na Tanesco zinatakiwa zipite gari za uzito wa tani 10, lakini gari zinazopita pale ni zaidi ya uzito huo, jambo hilo limefanya barabara hizo kuharibika mapema lakini siyo kwamba zimejengwa chini ya kiwango,”amesema.
“Zamani gari zilikuwa zinabeba mizigo juu tofauti na siku hizi mizigo inakaa ndani ya buti, huwezi kujua gari imebeba mzigo mzito kiasi gani na barabara inaharibika, hivyo huwezi kuona athari zake leo au kesho. Sasa wakati wa mvua kama hizi tunaona athari zake kwa kuchimbika kwa barabara,”alisema.
Katibu wa CCM wa manispaa hiyo, Loth Ole Nessele amesema hana taarifa kuhusiana na vibanda hivyo mpaka atakapofika eneo linalokusudiwa kubomolewa vibanda vyao.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts