4/26/16

CAG akosoa mashirika ya UDA, ATCL

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imekosoa uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kuuza hisa kwa Kampuni ya Simon Group na kusema mauzo yaliyofanyika ni batili.
Katika ripoti hiyo ya ukaguzi wa hesabu za mwaka 2014/15 iliyowasilishwa jana bungeni, imeweka wazi kuwa Bodi haikuwa na mamlaka ya kuuza hisa za UDA na ameshauri kwamba hisa hizo zinapaswa kurudishwa serikalini.
Akifafanua, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali , Profesa Mussa Assad alisema UDA ilikuwa na uwezo wa kuwa na jumla ya hisa za mtaji milioni 15 kwa thamani ya Sh 100 kwa kila hisa.
Hisa 47.5 sawa na asilimia 7.1 ziliwekwa sokoni na asilimia 51 ziliuzwa Benki ya DCB na asilimia 49 ziliuzwa kwa Serikali Kuu. Imeelezwa kuwa, hisa asilimia 52.2 zilizobakia hazikugawiwa, badala yake Bodi ya Wakurugenzi iliziuza kwa kampuni hiyo ya Simon Group bila kufuata mapendekezo ya Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC).
Katika ukaguzi wa CAG, amebaini kwamba hisa zilizobakia hazikugawiwa bali ziliuzwa kwa kampuni hiyo kwa Sh bilioni 1.14 huku kampuni ikilipa asilimia 24.9 pekee ya bei ya makubaliano ambayo ni Sh milioni 298.
Imebainishwa kwamba, kiasi kilichobaki hakuna ushahidi kama kililipwa au la. CAG amemshauri Msajili wa Hazina kufuatilia suala hilo kubaini kama fedha zilizobaki zililipwa. Amesisitiza kuwa UDA inapaswa kurudi chini ya usimamizi wa serikali hadi hapo mgogoro utakapotatuliwa.
“Kuna mgogoro kwenye suala la Uda, kwanza hisa zilizouzwa kwa kampuni ya Simon Group hazikupata idhini ya serikali na sasa tunaandaa mapendekezo ya kuuza asilimia 49 ya hisa za UDA na tutayafikisha mbele ya Bazara la Mawaziri”, alisema Profesa Assad.
Wakati huo huo akizungumzia ukaguzi wa uendeshaji wa ATCL, CAG, alisema shirika hilo linaendeshwa kwa hasara na kwamba linahitaji mageuzi makubwa ya kuwa na menejimenti imara itakayokuwa na mpango madhubuti wa kulifufua.
Alisema mpango wa kununua ndege ili kulifufua shirika hilo unapaswa kuangaliwa upya kwa sababu mpango huo ni kununua ndege kwa mkopo hivyo kama hakutakuwa na mpango madhubuti uwezekano wa kushindwa kufufuliwa kwa shirika hilo unaweza ukatokea.
Taasisi nyingine za serikali ambazo ripoti ya CAG imeibua kasoro mbalimbali na kutoa mapendekezo juu ya utatuzi ni Mamlaka ya Bandari (TPA) aliyosema wamebaini kuwa mita za kupima mafuta katika bandari hiyo hazitumiki hivyo udhibiti wa mapato ya serikali unakuwa mgumu na kushauri mita hizo zitumike kupima mafuta, kama alivyoshauri kwenye ripoti nyingine za miaka ya nyuma.
“Hili nalo ni tatizo sugu, nilishauri kwenye ripoti za nyuma kwamba mita zilizofungwa bandarini kwa ajili ya kupima mafuta zitumike kwa kazi hiyo, ila hadi tunaandika ripoti hii hakuna mita iliyokuwa ikitumika, sasa serikali inashindwa kudhibiti mapato yake,” alisema Profesa Asaad.
Kuhusu uchakavu wa karakana ya kutengenezea meli, CAG alisema TPA, ina karakana ambayo imejengwa mwaka 1950 lakini haifanyiwi matengenezo ili kuongeza ufanisi na badala yake matengenezo ya matishari za meli yamekuwa yakifanywa nchini Kenya, ambapo ni gharama kubwa.
“Nilibaini kuwa matengenezo ya matishari kwa muda mrefu sasa yamekuwa yakifanywa katika bandari ya Mombasa ambapo kiasi cha Sh bilioni 1.33 kilitumika kulipa matengenezo hayo na hii pia inafanya meli kubwa kushindwa kutia nanga bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa wanaogopa kukosa karakana ya matengenezo ya vifaa vya meli zao”, alisema Profesa Asaad.
CAG aigusa TICTS
Dosari nyingine ambayo CAG ameibaini ni kwamba TPA, haina uwezo wa kufahamu na kusimamia taarifa za kontena zinazopokelewa na TICTS kwa kuwa mamlaka hiyo haina haki ya kuingia katika mfumo wa kompyuta wa TANSIC, ambao unatumiwa na Mamlaka ya Mapato nchini TRA, kuhifadhi taarifa hizo.
Alisema TPA, inategemea taarifa kutoka TICTS ambazo zinaweza kuwa sio sahihi na kushauri mamlaka hizo TPA na TRA kuwa na mfumo wa ushirikiano wa kupata taarifa sahihi ili kuwa na kumbukumbu sahihi ya mizigo yote inayoingia kupitia bandari hiyo.
Akizungumzia kasoro za Mkataba wa TICTS na TPA, CAG, alisema umiliki wa asilimia 51 ya hisa wa Kampuni ya TICTS ulihamishwa kwenda kwa kampuni ya Hutchison International Port Holding Desemba 30, mwaka 2005 kinyume na matakwa ya mkataba.
Alisema kulingana na mkataba wa awali, endapo kiwango cha ufanyaji kazi kwa mwaka kitashuka chini ya kiwango cha asilimia 25, mkataba unaweza kutenguliwa. Imeelezwa kwamba kwa miaka mitano mfululizo tangu kuingiwa kwa mkataba huo mwaka 2000, TPA haikufanya tathmini ya ufanisi kinyume na makubaliano ya mkataba na mwaka 2007 TPA ilifanya ufanisi wa TICTS na kugundua kampuni hiyo ilifanya kazi chini ya kiwango.
Pamoja na kugundua hilo, alisema, bado TPA haikuvunja mkataba bali walihamishia mkataba huo kwa kampuni hiyo ya Hutchison. Pia CAG, katika ripoti hiyo alibaini kuwa kwa mwaka 2014/15 kati ya meli 1,253 zilizotia nanga nchini meli 145 hazikuonekana katika mfumo wa mapato ya mamlaka hiyo na menejimenti ilifanikiwa kupata nyaraka za meli 60 tu hivyo meli nyingine 85 hakuna nyaraka zilizoonekana.
“Sasa kitu kama meli na ukubwa wake hazikuonekana kwenye mfumo wa bandari ni jambo la kushangaza”, alisema CAG. TFDA na bidhaa za bil.4.6/- Kwa upande wa ukaguzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), CAG amebaini kwa mwaka huo wa ukaguzi bidhaa za Sh bilioni 4.6 ziliingizwa nchini na mamlaka hiyo bila kufanyiwa ukaguzi na sababu zilizotolewa ni kwamba mamlaka hiyo ina upungufu wa wafanyakazi.
Bohari Kuu ya Dawa
Kwa upande wa Bohari Kuu ya Dawa nchini, ripoti ya CAG, imebaini kuwa dawa za thamani ya Sh bilioni mbili ambazo hazikuwa kwenye kumbukumbu zilionekana ziko njiani kutoka MSD kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili tangu Mei mwaka 2012. Pia ripoti ya CAG ilibaini kuwepo kwa bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 18 zilizokuwa kwenye maghala ya bohari hiyo kwa muda mrefu hivyo kuisha muda wa matumizi yake.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts