4/26/16

KCMC katika kashfa, watumishi tisa walipwa mishahara mitatu


HOSPITALI ya Rufaa ya KCMC, imeingia katika orodha ya taasisi nyeti za umma zilizokumbwa na kashfa ya kuwa na watumishi hewa tisa, wakiwamo vigogo wa Wizara ya Afya wanaolipwa mishahara mitatu kwa mwezi.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, alisema kati ya watumishi hao, yupo kigogo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ambaye mamlaka ya kumsimamisha kazi au kumfukuza yako mikononi mwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
“Tulijipa kazi ya ziada ambayo hatukupaswa kuifanya sisi kama mkoa, lakini kwa sababu institution (taasisi) iko ndani ya mkoa wetu, tuliona ni vizuri tukafanya kazi ya ziada kubaini watumishi hewa, kwa kutumia mbinu tulizonazo na tumebaini watumishi hewa wapatao tisa,” alisema Sadick.
Bila ya kuwataja majina, Sadiki alisema mmoja wao ni mtu mzito ambaye analipwa mishahara na Wizara ya Afya, Hospitali ya KCMC, Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi cha KCMC.
Kati ya watumishi hao, yumo pia Daktari Bingwa wa viungo ambaye alistaafu utumishi wa umma, lakini anaendelea kulipwa mshahara. Aidha, yumo pia daktari aliyehamishwa kazi KCMC na kupelekwa katika hospitali Teule ya Serikali,
akarejeshwa na Machi, mwaka huu, alilipwa mshahara kupitia Wilaya ya Hai, Hospitali Teule aliyekuwamo awali na kulipwa tena na Wizara ya Afya.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa, yuko kigogo analipwa na Wizara ya Afya na Hospitali ya KCMC, lakini pia kuna Mhadhiri mwandamizi wa chuo hicho cha tiba cha KCMC, ameajiriwa na Wizara ya Afya, pia analipwa mshahara wa pili na chuo hicho.
“Huyu alikuwa KCM College (Chuo cha KCMC), lakini sasa hivi ana mkataba mwingine na Wizara na analipwa na serikali, na chuo. Halikadhalika mtu wa nne, analipwa na chuo, Wizara, na Hospitali ya KCMC.
Alisema wa tano, ameajiriwa na wizara na chuo, wa sita analipwa mshahara na KCM College na wizara, wa saba aliwahi kufanya kazi KCMC, akahamishwa na kupelekwa Hospitali Teule ya Serikali na mwezi uliopita akarejeshwa na akalipwa mshahara kupitia Wilaya ya Hai, KCMC na wizara.
Alisema mkoa umeanza na Hospitali ya Rufani ya KCMC kwa sababu ina wajibika Wizara ya Afya moja kwa moja, na kwamba mbinu walizozitumia kuhakiki na kuwabaini watumishi hao, zitaendelea kutumika kwenye taasisi moja hadi nyingine.
Kuhusu hatua zitachukuliwa dhidi ya vigogo hao, Sadiki alisema majina yao yamepelekwa kwa mwajiri wao, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, kwa ajili ya hatua zaidi.
Alifafanua kuwa kwa sababu watumishi hao wako nje ya mamlaka yao, na nje ya uwezo wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, wamemwandikia barua Katibu Mkuu wa wizara hiyo ili achukue hatua ya kuwaondoa katika orodha ya malipo, na kusababisha afanye uhakiki na kutoa uamuzi.
“Tumefanya hivyo, kwa sababu isije ikafika mahala, wakasema ninyi mlikuwapo huko na tuliwakabidhi mkoa, hata kama walikuwa chini ya wizara ilikuwa ni wajibu wenu kuifanyia kazi. Watumishi hewa ni hewa tu, na ikibainika katika mkoa wako wapo hutakwepa lawama, kama RC,” aliongeza.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts