Kikwete Ataja Utajiri Wake | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

4/30/16

Kikwete Ataja Utajiri Wake


RAIS mstaafu Jakaya Kikwete ametaja mali alizochuma alipokuwa madarakani kwa miaka 10, kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma hivi karibuni kama sheria inavyomtaka, lakini tamko hilo ni siri kwa mujibu wa sheria, imeelezwa.

Kamishna wa Tume ya Maadili, Jaji mstaafu Salome Kaganda ameiambia Nipashe katika mahojiano maalumu katikati ya wiki kuwa Kikwete ameshawasilisha tamko la mali zake tangu aondoke madarakani Novemba 5, mwaka jana.
Jaji Kaganda alisema Kikwete aliwasilisha fomu inayoonyesha mali alizozipata wakati akiwa madarakani kati ya 2005-2015, na alizozipata kabla hajangia madarakani kwa Sekretarieti yake.
Nipashe ilizungumza na Jaji Kaganda kujua kama Kikwete alishatoa tamko kama Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 na kanuni zake zinavyoelekeza, lakini pia kufahamu idadi ya mali anazomiliki Rais huyo mstaafu na thamani yake.
Kaganda alisema ni kweli Kikwete aliorodhesha mali zake zote kwa tume lakini Jaji huyo alikataa katakata kumwonyesha mwandishi wa habari hizi tamko hilo.
Jaji Kaganda alisema sheria inazuia kumwonyesha mtu mwingine tamko la mali la mtu mwingine hadi kuwe na sababu ya maana ya anayehitaji, na pia kuwe na ulazima wa kufanya hivyo.
"Mwananchi anaweza kupata taarifa za mali za viongozi kwa kufuata utaratibu uliopo, lakini baada ya kupata taarifa hizo, haruhusiwi kuzitangaza au kuzichapisha kwenye vyombo vya habari,” alisema Jaji Kaganda.
Kwa mujibu wa kifungu kifunga 9(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, “Kila kiongozi wa umma atatakiwa katika kipindi cha miezi mitatu au katika kipindi cha siku thelathini baada ya kupata wadhifa, mwisho wa mwaka au mwisho wa kutumikia wadhifa wake kumpelekea Kamishna tamko la maandishi katika hati rasmi linaloorodhesha mali au rasilimali zake.”
Aidha, kifungu namba 9 (6) kinataka “Wakati wa kutoa tamko la rasilimali zake kwa mujibu wa fungu hili, kiongozi wa umma atatakiwa: (a) kutaja thamani ya mali aliyotamka na chanzo au namna alivyopata mali hiyo."
Kifungu namba 11 (2) cha sheria hiyo kinaeleza kuwa rasilimali zinazotakiwa kutajwa ni pamoja na (a) nyumba, mali ya starehe na mashamba yanayotumiwa au yanayotarajiwa kutumiwa na viongozi wa umma au familia zao.
Kifungu 2 (b) kinataka kutajwa kwa kazi za sanaa, mambo ya kale na vitu alivyonunua kidogokidogo; (c) magari na aina nyingine binafsi za usafiri kwa matumizi binafsi; (d) fedha taslimu na amana zilizowekwa benki au taasisi nyingine za fedha.
Kifungu 2 (e) kinataka taarifa za hawala za hazina na uwekezaji mwingine katika dhamana zenye thamani maalumu, zinazotolewa au kudhaminiwa na serikali au wakala wa serikali.
SH. MILIONI 25
Wakati viongozi wengi wa umma wakitaja mali zao kwa Tume ya Maadili tu ama kushindwa kutaja mali hizo huko kwa mujibu wa sheria, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ana historia ya peke yake.
Pinda alitaja mali anazomiliki ambazo miongoni mwake ni nyumba mbili pamoja na akaunti katika benki, zilizokuwa na fedha zisizozidi Sh. milioni 25 Januari 15, 2010.
Pinda alisema alikuwa akimiliki nyumba moja mjini Dodoma na nyingine Mpanda, mkoani Rukwa eneo la Makanyagio.
Aidha alisema alikuwa na kibanda shambani kwake Pugu, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
“Mimi kila mwaka nataja mali zangu kwa Tume (Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma)," alisema Pinda wakati huo akiwa madarakani. "Sijaulizwa, sijagombana na Tume.
"Ukiniuliza ni masikini kiasi gani, nitakwambia nina property (nyumba) Dodoma, nimejenga kwa utaratibu wa serikali wa kuomba mkopo, ninayo nyingine kwetu Mpanda pale Makanyagio.
“Dar es Salaam sina nyumba, pale Pugu nina nyumba kidogo, inahitaji kazi ya ziada.
"Kijijini nilikuwa nafikia kwa babu, babu ana kanyumba kake ka ovyo ovyo… kile ambacho mlikiona, ana vyumba viwili nilikuwa nalala pale, lakini baada ya Uwaziri Mkuu, jamaa wakaniambia aah… haiwezekani pale.
"Nilijua nitaweza kulala pale na hawa jamaa (wasaidizi wake) watalala mjini humo, nikaambiwa hapafai.”
Pinda ambaye wakati huo alikuwa pia Mbunge wa Mpanda Mashariki, alisema hana gari lolote zaidi ya alilopewa kwa kuwa Mbunge, na kwamba katika akaunti zake zote, wakati huo alikuwa na Sh. milioni 22 hadi 25 tu.

google+

linkedin