4/29/16

Magufuli Apongezwa Kufunga Akaunti za Serikali

 

CHAMA cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Iringa, kimesema uamuzi wa serikali ya Rais Dk. John Magufuli wa kufunga akaunti za mashirika na taasisi zake katika mabenki ya biashara na kuhamishia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), utasaidia kuikuza sekta binafsi nchini.Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Iringa, Lucas Mwakabungu aliyasema hayo jana kwenye warsha ya mafunzo ya Dawati la Majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi, iliyofanyika kwa siku mbili mjini hapa.

“Uamuzi huo wa rais wetu utasaidia sana kushusha riba za mabenki yetu ya biashara kwa sababu sekta binafsi ndiyo itakayokuwa mteja mkubwa wa mabenki hayo,” alisema Mwakabungu.

Pamoja na kuipongeza serikali kwa kazi kubwa inayofanya ya kuboresha mazingira yanayokuza sekta binafsi, Mwakabungu alisema bado mazingira ya biashara yameendelea kuwa katika changamoto nyingi.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na kodi nyingi, masoko ya bidhaa na huduma kutokuwa ya uhakika, miundombinu mibovu ya barabara na ukosefu wa umeme vijijini, matumizi ya pembejeo bandia na sheria ya vipimo na mizani kutosimamiwa ipasavyo.

Nyingine zinahusu wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya chini ya gharama za uzalishaji kwa sababu ya ukosefu wa bei elekezi, ukubwa wa ushuru wa mazao na ulipaji wa leseni za biashara ambao ni kikwazo kikubwa katika urasimishaji wa biashara.

Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts