4/30/16

Mahakama Kuu yaingilia kati kesi ya Kitilya, Shose


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeingilia kati kesi inayowahusu Kamishna Mkuu wa zamani wa TRA, Harry Kitilya na wenzake, Miss Tanzania (1996), Shose Sinare, na Sioi Solomon baada ya kuita jalada la kesi hiyo. Kutokana na jalada la kesi hiyo kuitwa Mahakama Kuu jana asubuhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyokuwa inasikiliza kesi hiyo ilishindwa kutoa uamuzi kama ina mamlaka ya kuendelea na mwenendo wa kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.


Upande wa mashtaka katika kesi hiyo uliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama hiyo kuwafutia shtaka la utakatishaji fedha lililokuwa likiwakabili washtakiwa hao.


Kitilya na washtakiwa wenzake wawili, Sinare na Sioi waliokuwa maofisa wa Benki ya Stanbic (T) walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manane likiwamo la kutakatisha fedha Dola za Marekani 6 milioni.


Lakini Jumatano iliyopita Mahakama ya Kisutu iliwafutia shitaka hilo baada ya upande wa utetezi kuomba liondolewe kwa maelezo kuwa halijakidhi vigezo vya kisheria kuwa shtaka la utakatishaji fedha kwani hakuna maelezo ya wazi jinsi walivyotenda kosa hilo.


Hakimu Emilius Mchauru anayesikiliza kesi hiyo alikubaliana na hoja zilizotolewa na Wakili Alex Mgongolwa na katika uamuzi wake alisema maelezo ya shtaka hilo yanachanganya na hivyo akaamua kulitupilia mbali shtaka hilo.


Baada ya kufutiwa shtaka hilo na hivyo kubakiwa na mashtaka ya jinai ya kawaida, mawakili wanaowatetea wakiongozwa na Majura Magafu waliwaombea dhamana wateja wao.


Lakini wakati Mahakama ikijiandaa kutoa uamuzi wa maombi hayo, baada ya kuahirisha kwa muda, upande wa mashtaka uliibuka na hoja kuwa umewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa kuwafutia shtaka hilo.


Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekoma alisema kutokana na taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa ambayo tayari imeshawasilishwa mahakamani, mahakama hiyo ya Kisutu haiwezi kuendelea na lolote kuhusiana na kesi hiyo, kwani tayari shauri hilo liko ngazi ya rufaa.


Hoja hiyo ya Jamhuri ilipingwa na mawakili wa utetezi wakidai kuwapo taarifa ya kusudio hakuwezi kuizuia mahakama hiyo kutoa uamuzi ambao ilikuwa tayari imeshauandaa kwa kuwa hakuna kifungu chochote cha sheria kinachoizuia.Baada ya mvutano mkali, mahakama iliahirisha na kupanga kutoa uamuzi wake jana. Hata hivyo, jana Hakimu Mchauru alishindwa kutoa uamuzi wowote badala yake akasema jalada la kesi hiyo limepelekwa Mahakama Kuu. Hakimu Mchauru alipanga kesi hiyo kuendelea Mei 12, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts