Mamlaka ya Osha yawaburuza waajiri 150 mahakamani | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

4/26/16

Mamlaka ya Osha yawaburuza waajiri 150 mahakamani
Mamlaka ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi (Osha) imewafikisha mahakamani waajiri 150 wakiwamo wa viwanda na migodi kwa kutokuwa na kamati za afya na usalama kazini na watoa huduma ya kwanza katika maeneo yao ya kazi.


Kwa kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana, waajiri 250 walitozwa faini na wawili walifungiwa viwanda vyao kwa kukiuka Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 na hivyo kuhatarisha usalama wa wafanyakazi.


Akizungumza jana baada ya kufungua semina ya afya na usalama mahali pa kazi kwa wajasiriamali wa Manispaa ya Morogoro, Meneja mafunzo wa Osha Kanda ya Mashariki, Jerome Materu aliwapa mwezi mmoja wamiliki wa viwanda, migodi na kampuni kuhakikisha wanaunda kamati hiyo, vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.


Materu alisema kuundwa kwa kamati hizo ambazo zitapewa mafunzo maalumu na Osha, kutasaidia kupunguza ajali zinazowapata wafanyakazi ambao wengi hupata ulemavu wa kudumu na vifo kwa kutojikinga na vifaa ama kuchukua tahadhari.


Baadhi ya wajasiriamali waliopata mafunzo hayo walisema wameelewa namna ya kulinda afya na usalama wao wanapokuwa katika shughuli zao za kila siku na kuahidi kuifikisha elimu hiyo kwa wajasiriamali wengine.


Mmoja wa wajasiriamali hao, Husna Shabani alisema kabla ya mafunzo hakujua kama kazi yake ya kusaga unga wa sembe inamadhara kwa afya yake wakati wa kusaga unga na kufungasha kwenye mifuko.

chanzo: Mwananchi

google+

linkedin