4/24/16

Mbowe Apewa Somo la Bajeti na Tume ya Mipango

 

SIKU moja baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), kudai kuna uvunjifu wa sheria katika uhamishaji wa fedha zilizoidhinishwa na Bunge, Tume ya Mipango imetoa ufafanuzi na kusema hakuna sheria iliyovunjwa.Akizungumza mara baada ya kuzinduliwa kwa Kitabu cha Muongozo kuhusu wa Usimamizi Rasilimali za Umma, Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Mipango, Florence Mwanry alisema madai yaliyotolewa juzi na Mbowe bungeni si ya kweli.

“Wabunge ndio walipitisha wenyewe Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015, ambayo inafafanua kuhusu uhamishaji wa fedha kutoka kifungu kimoja kwenda kingine, hivyo uhamisho wa fedha uliofanywa uko sahihi na hakuna sheria iliyovunja, wakaisome vizuri,” alisema Mwanry.

Mbowe akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kususa Bunge, alitoa mfano wa bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa na Bunge kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2015/16, iliyokuwa ya Sh bilioni 883.8, ambapo kati ya fedha hizo, fedha za ndani zilikuwa ni Sh bilioni 191.6.

Alisema inashangaza kuwa hadi kufikia Machi 2016, Wizara ilikuwa imeshapokea kutoka Hazina Sh bilioni 607.4, ambazo ni fedha za ndani, tofauti na ilivyopangwa kuwa fedha za ndani ni Sh bilioni 191.6. Mbowe alidai kuwa hiyo inaonesha kuwa kuna ongezeko la fedha zilizotolewa na Hazina hadi kufikia Machi 2016, ikilinganishwa na fedha zilizoidhinishwa na Bunge.

Akitoa ufafanuzi, Mwanry ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Mipango, alisema Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015, inamruhusu Ofisa Masuhuli kuhamisha fedha kutoka kifungu kimoja kwenda kingine, ili mradi asivuke asilimia saba ya bajeti nzima.

Kadhalika, kwa upande wa Waziri, alisema sheria hiyo inampa uwezo wa kufanya uhamisho wa fedha kutoka kifungu kimoja kwenda kingine ili mradi asizidi asilimia 10 ya bajeti na katika uhamisho uliofanywa na wizara tajwa, mambo hayo yamezingatiwa.

Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts