Mwigulu Nchemba Awajia Juu Maofisa Ushirika | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

4/27/16

Mwigulu Nchemba Awajia Juu Maofisa Ushirika

 

WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Lameck Nchemba amesema baadhi ya maofisa ushirika wamekuwa ni tatizo kwa kutumia vibaya mamlaka yao kushiriki kuhujumu na kudhoofisha Vyama vya Ushirika.

Waziri Mwigulu alisema hayo Mjini Moshi katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Gelazius Kamanzi kwenye ufunguzi wa Mafunzo ya Maofisa Ushirika kutoka Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.

“Ofisa Ushirika kuchukua mkopo wa fedha au pembejeo kutoka kwenye chama cha ushirika wakati sio mwanachama ni mfano mbaya kwa viongozi na wanachama wa ushirika,” alisema na kuongeza: “Vile vile, zipo tuhuma kwamba baadhi yenu mnaomba rushwa ili muweze kutekeleza wajibu wenu.Tatizo hilo la rushwa lipo pia kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika na wakati mwingine hufanyika kwa kushirikiana na baadhi yenu.”

Mafunzo hayo yameandaliwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa maofisa ushirika, yatafanyika kikanda nchi nzima kwa lengo la kuwajengea uwezo wa usimamizi na udhibiti wa vyama vya ushirika, uhamasishaji wa maendeleo ya ushirika na uandaaji na uwasilishaji wa takwimu za vyama vya ushirika na umuhimu wake.

Matatizo mengine yaliyoelezwa na Waziri Mwigulu na kuagiza yakomeshwe ni pamoja na vyama kutowalipa wanachama wao fedha zao zote za mauzo ya mazao, wanachama kuongezewa madeni wasiyokopa kama ya pembejeo.

google+

linkedin