4/26/16

Posho kamati za afya zafyekwa
Serikali imefuta posho zilizokuwa zikitolewa kwa kamati za afya za vijiji kila wanapokutana kwenye vikao vya robo mwaka na sasa fedha hizo zitaelekezwa kwenye ununuzi wa dawa.


Hayo yalibainishwa jana na Mratibu wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Yonna Ndaiga alipotembelea zahanati za Tarafa ya Chilonwa.


Alisema kuanzia sasa wajumbe wa kamati za afya za vijiji watakuwa wakifanya kazi za kujitolea, zile posho za Sh5,000 walizokuwa wakilipwa wakati wa vikao hazitatolewa.


Ndaiga alisema kazi za kamati ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa gharama nafuu.


Pia, kila mwanakamati anatakiwa kuwa mwanachama wa CHF ili awe mwakilishi mzuri anapowahamasisha wananchi wajiunge na mfuko huo.


“Utaratibu wa dawa uko mikononi mwa wanakamati, kila kituo kina fedha lazima zitumike kununua dawa,” alisema Ndaiga.


Aliwataka wanakamati hao kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kujiunga kwa wingi na CHF ili waweze kupata huduma za matibabu.


Alisema vituo vingi hivi sasa vina dawa za kutosha tofauti na awali, wananchi walikuwa wakizikosa licha ya kuwa na kadi ya mfuko huo.


Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi aliwataka wananchi kubadilika kwa kujiunga na CHF ili kupunguza gharama za matibabu.


Meneja wa CHF Wilaya ya Chamwino, Abdallah Misenge alisema wamejipanga kutoa elimu kwenye kata zote za wilaya hiyo.


Aliwataka waganga wa vituo vya afya na zahanati kutuma madai kwa wakati ili fedha za dawa zilipwe.

Chanzo: Mwananchi
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts