4/30/16

Serikali Yakubali Hoja ya Zito


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali itaifanyia kazi hoja iliyotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ya kutaka ufanyike uchunguzi dhidi ya Benki ya Standard ICBC ya Uingereza juu ya mkopo wa dola za Marekani milioni 600 (Sh trilioni 1.2), wenye harufu ya ufisadi.

Juzi Zitto alitaka Bunge liunde kamati teule kuichunguza benki hiyo kutokana na hati fungani hiyo ya dola za Marekani milioni 600.
Zitto alitaka kamati hiyo iundwe ili nchi iache kutegemea taarifa za Taasisi ya Uingereza ya Kuchunguza Rushwa Kubwa (SFO), ambazo ndizo zilizotumiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), baadhi ya watu mahakamani.
Kamishna Mkuu Mamlaka ya Mapato wa zamani, Harry Kitilya na waliokuwa wafanyakazi wa Benki ya Stanbic, Sioi Sumari na Shoshe Sinare wamefikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuhusiana na sakata hilo.
Mbunge huyo wa Kigoma Mjini alisema taasisi hiyo ya Uingereza ilifanya uchunguzi kwa masilahi ya nchi yake, ndiyo maana haijaichunguza benki hiyo ya Uingereza.
Na Tanzania ikiichunguza na kubaini kwamba mchakato wa kutoa mkopo huo uligubikwa na rushwa, alisema Zitto, nchi itafutiwa deni la Sh. trilioni 2 ambazo inatakiwa kulipa ikiwa ni mkopo halisi na riba.
Jana Waziri Mkuu alisema “Hoja alizotoa (Zitto) ni nzuri na zina mashiko, kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, tumechukua ushauri wake tutaufanyia kazi.
"Pindi utaratibu ukikamilika tutataarifu umma.”
Akichangia hotuba ya Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora juzi, Zitto alisema Machi mwaka 2013 Serikali ilikopa dola za Marekani milioni 600 (Sh trilioni 1.2) kwa msaada wa Benki ya Standard ya Uingereza ambayo sasa inaitwa Standard Bank ICIC Plc.
Alisema mkopo huo umeanza kulipwa mwezi uliopita na kwamba ulipaji huo utaendelea mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo tisa inayolingana.
“Ifikapo mwaka 2020, Tanzania italipa deni pamoja na riba dola milioni 897 ( Sh trilioni mbili)… Vile vile kuna taarifa kwamba hata fedha ambazo zilipatikana kutokana na mkopo huu hazikufika kule kunakotakiwa,” alisema Zitto.
Alisema amewasilisha maswali Wizara ya Fedha kutaka kujua miradi ambayo fedha hizi zilikwenda, ingawa kwa orodha ya miradi aliyonayo na kutokana na habari za hivi karibuni za Serikali kudaiwa na wakandarasi, mradi wa Kinyerezi na Kiwira, inaonyesha sehemu ya fedha zilizopatikana katika mkopo huu hazikupelekwa huko.
“Uchunguzi wa kina unatakiwa kwenye eneo hili ili kupata ukweli na kuzuia mambo kama haya kutokea siku za usoni.
“Nitatumia kanuni ya 120 (2) kutaka Bunge lako tukufu kuunda Kamati Teule kuichunguza Benki ya Standard ICBC ya Uingereza na kampuni yake dada ya Stanbic Tanzania kuhusiana na Mkopo wa Hatifungani wa Dola milioni 600, matumizi ya mkopo huo na ufunguzi wa Akaunti ya Escrow ya Bomba la Gesi la Mtwara – Dar es Salaam,” alisema Zitto.
Alisema kesi iliyopo mahakamani sasa inahusu dola milioni sita lakini wanaosemekana kula rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa.
Alisema kutokana na unyeti wa suala hilo, kundi la Watanzania zaidi ya 2,000 kutoka kona zote za dunia wamesaini barua kutaka Benki ya Standard ya Uingereza ichunguzwe kwenye suala hilo la Hati Fungani.
"Leo hii Takukuru inasaidiwa katika kesi hii na wataalamu kutoka Uingereza katika kesi inayohusu Benki ya Uingereza!
"Watanzania walioandika petition kutaka Benki ya Standard kuchunguzwa wanataka ukweli wote kujulikana – Standard Bank walihusika kwa kiwango gani katika kutoa rushwa ili kupata biashara?"
Takukuru inapaswa kufanyia kazi jambo hili kwa kuwafungulia mashtaka Standard Bank, alisema Zitto, ambayo ni ya kutoa rushwa ili kupata biashara nchini.
Alisema hii siyo mara ya kwanza SFO kuchunguza Tanzania kwani ilishafanya tena katika kesi ya rada na Shirika la BAE la Uingereza.
“Safari hii Tanzania isikubali kubeba tu makubaliano ambayo SFO inafanya na makampuni ya kimataifa," alisema Zitto.
"Ni lazima tufanye uchunguzi wetu na tufungue kesi dhidi ya makampuni haya.
"Haiwezekani wawe ni Watanzania tu wanaoshtakiwa kwa rushwa na kuwaacha wanaotoa rushwa hizo wakiendelea na biashara zao kama kawaida.”
Kuhusu sula la Akaunti ya Tegeta Escrow, alisema Mwaka 2014 Takukuru waliijulisha Kamati ya Bunge ya PAC kwamba ilichunguza na kumaliza uchunguzi wa suala hilo lakini hata siku moja hawajasema ni lini watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
“Naomba tupate kauli ya Serikali kuhusu jambo hili, Serikali inaogopa nini? Serikali inamwogopa nani? Kwanini kesi ya ufisadi wa IPTL inakaliwa kimya? Kwa maslahi ya nani?,”
 -NIPASHE
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts