4/27/16

Simba yamuachia Banda J'pili

SIMBA imemfungia beki wake anayecheza pia nafasi za kiungo, Abdi Banda, kwa mwezi mmoja ambao ameshautumikia kuanzia Aprili mosi kutokana na makosa manne ya utovu wa nidhamu na atakuwa huru kuanzia Jumapili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa klabu hiyo jana, Banda pia atatakiwa kuomba radhi kwa maandishi kufuatia makosa yake yakiwamo ya "kutuma ujumbe kupitia mitandao ya kijamii kumshambulia mwalimu kwa lugha zisizo za kiungwana."

Makosa mengine ni pamoja na kukataa kujiandaa kuingia kucheza, kukataa kuvaa vazi la mdhamini wakati wa safari na kuandika ujumbe kwa viongozi akielezea kukataa kuendelea na timu.

Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Simba, Amos Gahumeni, Banda katika utetezi wa makosa yake alisema alimshauri kocha ambakishe uwanjani mchezaji ambaye (Banda) aliamini kwamba angeendelea kucheza vizuri zaidi yake kama angeingia na kwamba kuhusu kutovaa sare ya mdhamini safarini, alijua kwamba angebaki Tanga hivyo akaacha kuvaa sare hizo.

Kamati ya Nidhamu iliyokaa na kutoa adhabu hiyo iliridhika kwamba kulikuwa na makosa ya msingi ambayo ni ukiukaji mkubwa wa taratibu za kazi.

Banda alimgomea kocha Mganda, Jackson Mayanja, kuingia katika dakika ya tano wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union, kuchukua nafasi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, akidai ni mapema mno kumtoa beki mwenzake kwa sababu ya makosa machache aliyofanya.

Baada ya mchezo huo ambao Simba ilishinda mabao 2-0, uongozi wa Simba alimtaka Banda kumuomba msamaha kocha Mayanja, lakini akagoma na tangu hapo hakuripoti mazoezini.

Baadaye Banda akatakiwa kuandika barua ya kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua kwa utovu wa nidhamu aliofanya, naye akafanya hivyo, ingawa Simba SC wamechukua muda mrefu kutoa uamuzi.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts