4/27/16

Wakazi wa Mkoani Njombe Wanufaika na Huduma za Madaktari Bingwa


Jumla ya wagonjwa 267 wa mkoani Njombe wamenufaika na huduma za matibabu za madaktari bingwa kutoka hospitali mbalimbali za hapa nchini.

Takwimu hizo zimetolewa leo mkoani Njombe na Afisa Mawasiliano Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Luhende Singu wakati akitoa taarifa za maendeleo ya zoezi la utoaji wa huduma za afya kwa wananchi chini ya ufadhili wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Amesema kuwa kati ya wagonjwa hao, 13 wamepatiwa huduma ya upasuaji kutoka kwa madaktari bingwa pia huduma hizo zinaendelea kutolewa  katika Hospitali ya Kibena mkoani humo.
"Tunawashukuru sana wananchi wa Mkoa wa Njombe kwa kuitikia wito wetu, leo ni siku ya tatu lakini tumeshawapatia matibabu jumla ya wananchi 267 kati ya hao wagonjwa 13 wamepatiwa huduma ya upasuaji, tunawasihi waendelee kuja kwakua bado tuna siku mbili za kuendelea kuwapatia huduma za afya"alisema Singu.

Amefafanua kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa waliopatiwa matibabu mkoani hapo ni wanawake ambao wengi wao wanasumbuliwa na magonjwa ya moyo pamoja na mfumo wa mkojo.
Lengo wa mpango huu wa kutumia madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali za Rufaa za Kanda ni kuhakikisha kuwa  huduma za matibabu kutoka kwa madaktari bingwa zinawafikia wanachama wa Mfuko huo na Watanzania kwa ujumla popote walipo.

Mpaka  sasa Mfuko wa Taifa wa  Bima ya Afya  umepeleka huduma ya madaktari bingwa katika Mikoa 14 ikiwa na lengo la kuhakikisha huduma bora za matibabu zinatolewa kwa usawa.

Singu ametoa wito kwa wananchi wa mkoani Njombe kuendelea kujitokeza kwa wingi kujipatia matibabu kwa kuwa huduma hizo zinatolewa kwa gharama nafuu
Weka Maoni Yako Hapa
Share:

Advertisment

Habari Mpya

Follow us on Facebook

Popular Posts

Blog Archive

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger Design by Yuvinusm