4/30/16

Wakulima Skimu ya Iganjo washauriwa kuanzisha Saccos


Wakulima Skimu ya Iganjo washauriwa kuanzisha Saccos
Serikali imewataka wakulima waliojiunga katika ushirika wa Umwagiliaji maji kutoka katika kata za Iganjo, uyole, Idude, Salaga na Igawilo zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuanzisha Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo ili kuifanya skimu yao kuwa endelevu.
Ushauri huo ulitolewa na Afisa Kilimo Mkuu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bwana Leo Mavika wakati alipoitembelea skimu hiyo ya umwagiliaji ambayo ipo nje kidogo ya jiji la Mbeya.
Alisema ili Skimu ya umwagiliaji ya Iganjo iwe endelevu, wakulima hao hawana budi kuondokana na mtindo wa sasa wa kuhifadhi fedha kidogo benki na kutokuwa na malengo ya muda mrefu ya mradi huo.
Aliongeza kuwa uendelevu wa skimu hiyo unategemea sana namna wana ushirika hao watakavyoweka mipango yao ya pamoja katika kukusanya ushuru wa fedha kutoka kwa wana ushirika wapatao 1006 ambao wanafaidika na huduma ya kilimo cha umwagiliaji.
Sambamba na kuanzisha Saccos bwana Mavika aliwataka wakulima hao kuhakikisha kuwa wanalijadili suala la soko la mazao yao ili kuepuka kupunjwa na walanguzi mbalimbali wanaofika katika mashamba yanayozunguka skimu hiyo ili kujipatia mazao kutoka kwa wakulima kwa bei rahisi.
"Ni lazima mkulima ujue bei ya soko kuepuka kuuza mazao yako kwa bei ya hasara na mwisho wake kushindwa kufaidika na jasho lako," alisema.
Aliwaasa wakulima hao kutoridhika na bei zinazotamkwa na walanguzi wa bidhaa hizo bali wanapaswa kufanya utafiti wa bei za mazao yao katika masoko yaliyopo ndani na nje ya mkoa wa Mbeya.
Akielezea jinsi ulivyoibuliwa mradi huo, Fundi Sanifu Umwagiliaji kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya bwana Hamis Manyaji alisema kuwa mradi huo uliibuliwa moja kwa moja na wananchi wa kutoka kata za Iganjo, uyole, Idude, Salaga na Igawilo kupitia Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs).
Alisema kuwa mradi huo uliibuliwa rasmi mwaka 2006 ambapo katika awamu ya kwanza serikali ilitoa shilingi milioni 21 na wananchi wakachangia shilingi milioni sita katika kujenga banio na mfereji mkuu wa kusambaza maji katika skimu hiyo.
Bwana Manyaji alisema serikali iliendelea kuwapatia fedha wakulima hao katika awamu ya pili mwaka 2007/08 kiasi cha shilingi milioni 40 ambapo wananchi walichangia nguvu zao na kufikia shilingi milioni 11. Fedha hizo zilitumika kujenga mifereji yenye urefu wa mita 2000 kuzunguuka mashamba ya skimu hiyo.
Katika awamu ya tatu walipewa shilingi milioni 28 na wakulima walichangia shilingi milioni sita, ambazo walizitumia kuongeza mifereji wenye urefu wa mita 650. Katika awamu ya nne mwaka 2010/11 serikali iliwapa shilingi milioni 11.8 ambazo walizitumia kuongeza mfereji wenye urefu wa mita 530 na kalavati na awamu ya tano serikali iliwapatia shilingi milioni 30 na wakulima kuchangia shilingi milioni 11 ambazo zilitumika kujenga mfereji wenye urefu wa mita 1500 na kalavati mbili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika wa Umwagiliaji maji Iganjo bwana John Soda alisema kuwa yeye na wakulima wenzake wanaishukuru serikali kwa kuwajengea miundombinu ya skimu hiyo kwani inawawezesha kulima mazao ya chakula na biashara mwaka mzima.
Alisema kutokana na uwepo wa skimu hiyo wakulima wana uhakika wa kupata mazao mara tatu zaidi tofauti na kilimo cha kutegemea mvua. Alisema kutokana na kuwepo kwa skimu hiyo, wamejiwekea utaratibu wa kupanda mazao ya chakula hususani mahindi ambapo wanapata hadi gunia 25 kwa heka moja ya mahindi huku kwa mazao ya biashara kama vile viazi mviringo wanapata kati ya gunia 75 hadi 80 kwa heka moja.
Mmoja wa wakulima waliokutwa katika skimu hiyo bwana Serafini Jackson alisema kuwa skimu hiyo imebadilisha maisha yake kwani imemuwezesha kumudu kuihudumia familia yake ya watu watano.
Pia alisema kuwa skimu hiyo imemtoa katika utegemezi wa kufanya kazi za vibarua katika mashamba ya watu na badala yake naye ameweza kushiriki kikamilifu katika kilimo na sasa anamiliki mashamba yake.
Skimu ya umwagiliaji ya Iganjo ina ukubwa wa hekta 110 ambapo wakulima katika skimu hiyo pia hujishughulisha na kilimo cha mazao mengine ya biashara kama vile karoti, maharage na mboga mboga kama vile mchicha, figiri, kabichi, chainizi.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts