4/23/16

Yanga: Tutafanya Maajabu CAF

KOCHA WA YANGA

BAADA ya kuangukia katika michuano ya Kombe la Shirikisho ilikopangwa kukutana na Sagrada Esperanca ya Angola katika hatua ya mtoano, Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm ameahidi kuipaisha Yanga Kimataifa.

Amesema anaamini timu yake ina nafasi kubwa ya kutinga hatua ya makundi, hivyo atafanya kila linalowezekana kuhakikisha dhamira yake ya kuitoa Yanga kimasomaso inatimia, huku akitamba kuwa na kikosi bora na imara, ingawa kilikosa bahati mbele ya Al Ahly ya Misri, katikati ya wiki hii.

Usiku wa Jumatano iliyopita, Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 3-2 na Al Ahly kwenye mchezo wa raundi ya pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1, kwenye mchezo wa marudiano kwenye Uwanja wa Borg El Arab, jijini Alexandria, Misri.

 Pluijm alisema matumaini hayo yanatokana na ari na ubora iliyokuwa nao kikosi chake ambacho kilipambana kufa kupona katika mchezo na Al Ahly, licha ya kutolewa kwenye michuano hiyo.

“Siwezi kuwadharau wapinzani wetu Esperanca, lakini naamini hawatakuwa bora kama ilivyokuwa kwa Al Ahly na kama hivyo, ndivyo basi kuna uwezekano mkubwa wa Yanga kucheza hatua ya makundi kwa sababu tupo kwenye kiwango bora hivi sasa,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi, lakini mwenye uzoefu mkubwa na soka ya Afrika.

Esperanca inayomilikiwa na Shirika la Taifa la Madini la Angola, ina nyota kadhaa akiwemo `babu’ mwenye umri wa miaka 37, lakini mwenye makali ya upachikaji mabao, Arsenio Sebastiao Cabungula maarufu kama Love ambaye mwaka 2006 alikuwa miongoni mwa nyota wa Angola waliocheza Kombe la Dunia nchini Ujerumani.

Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts