5/4/16

Bajeti ya Elimu Inatakiwa Kuzingatia Gharama Halisi
BAJETI ni nyenzo muhimu katika kutekeleza na kufikia matokeo chanya ya mpango wowote unaohusu maendeleo ya taifa, taasisi na mtu mmoja mmoja.

Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mipango mbalimbali itakayowezesha utoaji wa huduma muhimu kwa raia wake ili kuchochea maendeleo na kukuza uchumi kwa ujumla. Sekta ya elimu ni miongoni mwa maeneo ambayo Serikali hii imeahidi kuitilia mkazo na kutoa kipaumbele katika kipindi hiki cha miaka mitano ya uongozi wa Rais John Magufuli. Kupitia sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, iliyozinduliwa Februari mwaka jana na kuanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali imeazimia kutekeleza mambo mbalimbali.

Miongoni mwa mambo hayo ni utoaji elimu msingi bila ada, kuongeza ubora wa elimu kwa kuimarisha ukaguzi shuleni, kuboresha miundombinu na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa stahili vya kujifunza na kufundishia pamoja na kuongeza ubora wa walimu kwa kutoa mafunzo, motisha na kuimarisha udhibiti wa taaluma ya ualimu. Hata hivyo, kufanikiwa kwa mipango hii, kunahitaji siyo tu upangaji makini wa bajeti ya sekta ya elimu, lakini pia upatikanaji wa bajeti hiyo pamoja na usimamizi madhubuti wa utekelezaji wake.

Mkurugenzi Mtendaji Hakielimu, John Kalage anatoa uchambuzi na ushauri juu ya mwelekeo wa bajeti ya sekta ya elimu 2016/17. Kalage anasema kama mtetezi na mdau muhimu wa upatikanaji wa elimu bora nchini, HakiElimu inapendekeza kwa Serikali maeneo ambayo yanahitaji kutiliwa mkazo katika upangaji wa bajeti ya sekta ya elimu katika mwaka wa fedha 2016/17.

“Tunaikumbusha na kuishauri Serikali kuhusu maeneo ya vipaumbele ambavyo ikiwa yatafanyiwa kazi ipasavyo, mipango na malengo ya Serikali kutoa elimu bora iliyo nafuu yatafanikiwa,” anasema. Anaelezea moja ya maeneo hayo kuwa ni bajeti ya utekelezaji wa elimu bila ada. Anasema kupitia sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, iliyofuatiwa na tamko la utekelezaji katika waraka namba 5 wa mwaka 2015, Serikali imeagiza kufutwa kwa ada za masomo katika shule za sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na michango ya aina yoyote kwa shule za msingi.

Anasema tafsiri ya agizo hilo ni kuwa shule za umma sasa hazitategemea michango na makusanyo ya ada kama vyanzo vya mapato ambayo yalikuwa yakisaidia shule kujiendesha. Kalage anasema kwa tamko hilo Serikali inalazimika sasa kugharamia mahitaji yote ya shule za msingi na sekondari ili kuwezesha ujifunzaji na ufundishaji. Mkurugenzi huyo anasema kabla ya agizo hilo la elimu bila ada na kusitishwa kwa michango ya wazazi uchangiaji wa elimu katika shule za umma ulifanywa kwa ushirikiano baina ya Serikali pamoja na wazazi.

Hata hivyo, upatikanaji wa fedha shuleni ulikuwa wa shida kwa kuwa Serikali iliweza kupeleka wastani wa Sh 4,000 hadi 5,000 tu kama ruzuku kwa shule za msingi badala y a Sh 10,000 zilizotakiwa kwa kila mtoto kwa mwaka. Aidha Serikali iliweza kutoa wastani wa Sh 12,000 hadi Sh 15,000 kwa kila mtoto kwa mwaka kama ruzuku kwa shule za sekondari badala ya Sh 25,000 zilizostahili.

Inadaiwa kuwa Serikali pia ilishindwa kupeleka fedha za maendeleo katika shule hasa zile zilizohusu ujenzi wa miundombinu na ukarabati wa madarasa, vyoo, maabara nk. Gharama hizi kwa kiwango kikubwa zilifidiwa na michango ya wazazi na ushiriki wajamii. Kalage anasema ili Serikali iweze kugharamia utoaji wa elimu pasipo wazazi kuchangia ni lazima kuongeza bajeti ya elimu inapopanga bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17.

Anasema kwa kuwa gharama za ujenzi wa madarasa ni kubwa, Serikali inaweza kuzigawa katika vipindi vya miaka mitatu ili itenge Sh bilioni 384 kila mwaka. Kama itaamua kufanya hivyo gharama ya miundombinu kwa mwaka wa fedha 2016/17 itakuwa Sh bilioni 671. “Ili kugharamia utoaji wa elimu bure Serikali inapaswa kufidia pesa za ada iliyokuwa ikitolewa na wazazi kwa shule za sekondari na fedha ya gharama za chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi kuanzia darasa la awali mpaka la saba,” anasema Kalage.

Pia inapaswa kulipia gharama za uboreshaji na ujenzi wa miundombinu inayohitajika kwa mwaka. Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na hakielimu kwa kuzingatia takwimu za idadi ya wanafunzi, shule na mahitaji, kila mwaka Serikali itapaswa kutenga kiasi cha fedha kisichopungua Sh bilioni 1,034.5 nje ya mahitaji mengine ya kisekta ili kugharamia elimu bila malipo,” anasema.

Ameishauri Serikali kuwa ni muhimu kuhakikisha kiwango hicho kinajumuishwa katika bajeti ya sekta ya elimu ya mwaka wa fedha 2016/2017 ili kutekeleza kwa ufanisi azma yake ya utoaji wa elimu bure. Eneo lingine ni upangaji wa bajeti ya sekta ya elimu. Mkurugenzi huyo wa hakielimu anasema upangaji huo umekuwa ni changamoto za muda mrefu, kwani mara zote umeshindwa kuzingatia uwiano unaokubalika kati ya matumizi ya kawaida na yale ya maendeleo.

Anasema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita wastani wa bajeti ya maendeleo ya sekta ya elimu umekuwa kati ya asilimia 11 mpaka 16 tu wakati ile ya matumizi ya kawaida imekuwa kati ya asilimia 80 mpaka 90. “Kiwango kilichotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika sekta ya elimu ni kidogo sana kulinganisha na changamoto za kimaendeleo kama ujenzi wa miundombinu ya madarasa, nyumba za walimu, mabweni, vyoo na maabara,” anasema Kalage.

Anasema mathalani mwaka wa fedha 2015/16 bajeti ya sekta nzima ya elimu ilikuwa Sh bilioni 3,887. Hata hivyo bajeti ya maendeleo sekta ya elimu ilikuwa Sh bilioni 604 tu ya sekta nzima, huku bajeti ya matumizi ya kawaida ikiwa ni Sh bilioni 3,282 ya bajeti ya sekta nzima ya elimu. Anasema jambo la kushangaza zaidi katika upangaji huo ni kuwa sehemu kubwa ya fedha inayodaiwa kuwa ni ya maendeleo katika sekta ya elimu huelekezwa katika kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Kwa mfano katika bajeti hiyo ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2015/16 Sh bilioni 604, nusu ya fedha hiyo Sh bilioni 306 ilikuwa kwa ajili ya mikopo ya elimu yajuu. Hivyo bajeti halisi ya shughuli za maendeleo ya sekta ya elimu ilikuwa Sh bilioni 298 tu. Anaeleza athari ya kupanga fedha za mikopo katika bajeti ya maendeleo ni pamoja na kuhadaa uhalisia wa bajeti yenyewe, kwani bajeti ya maendeleo inaweza kuonekana kama kubwa na inayotosha wakati katika hali halisi ni fedha kidogo sana isiyokidhi mahitaji.

“Tunaishauri Serikali kuchukua tahadhari juu ya aina hii ya upangaji wa bajeti, kwani ukweli ni kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ni kidogo sana kuliko zile za matumizi ya kawaida. Hii husababisha miradi mingi ya maendeleo katika sekta ya elimu kutotekelezwa,” anasema. Anasema Hakielimu inaitaka Serikali kufuata maelekezo ya upangaji bajeti yaliyotolewa ndani ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano yanayoitaka bajeti ya kawaida na ya maendeleo kuwa na uwiano wa asilimia 60 kwa 40.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts