5/12/16

BoT Yafafanua Uvumi Kuhusu Sarafu ya 500/-

BENKI Kuu Tanzania (BoT), imekanusha uvumi uliokuwa ukiendelea kuhusu mzunguko wa sarafu ya Sh. 500 kuwa mdogo na kusababisha wananchi kuhisi benki hiyo imeizuia kutokana na madai kutoka kwa baadhi watu kwamba hununuliwa na kuyeyushwa ili kutengenezea vito vya thamani.

Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa BoT, Marcian Kobello, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Nipashe kuhusiana na uvumi huo.
Kabello alisema uvumi huo si wa kweli kwa kuwa Bot imetengeneza sarafu za kutosha na mpaka sasa ina kiasi cha kutosha katika hifadhi yake.
“Kwanza jamii itambue kuwa suala la kuzuia sarafu hiyo haliwezekani maana mpaka Benki Kuu inaamua kuitengeneza, ilikuwa ni kwa malengo thabiti na siyo kukurupuka kama baadhi ya watu walivyofikiria,” alisema Kobello.
Alisema kwa sasa BoT imefungua dirisha la chenji makao makuu na katika matawi yake yote yaliyopo Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Zanzibar na sarafu hiyo inatolewa kwa mwananchi yeyote atakayeomba.
Aidha, alisema sarafu hiyo hupatikana katika benki zote za biashara kwa wateja wanaochukua fedha.
Akizungumzia kuhusu suala la kuiyeyusha na kutengeneza vito vya thamani, Kobello alisema sarafu hiyo imetengenezwa kwa madini ya chuma asilimia 94 na nickle asilimia sita, hivyo hakuna madini ya fedha katika sarafu hiyo na kuwataka wale wote wanaojihusisha na jambo hilo kama wapo, kuacha mara moja maana ni kinyume cha sheria.
BoT ilizindua sarafu ya Sh. 500 Oktoba, 2014 kutokana na noti ya Sh. 500 kuwa na mzunguko mkubwa na hivyo kuchakaa haraka, hali iliyoifanya benki hiyo kulazimika kuchapisha noti hiyo mara kwa mara.
 -NIPASHE
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts