Contact us: yuvinusm45@gmail.com | email: yuvinusm45@gmail.com

We're Coming Soon

Tutarudi Baada ya Matengenezo

Tupo kwenye matengenezo ya Mtandao Wetu Tutarudi Mchakato Ukishakamilika, Tunaomba Radhi kwa Usumbufu Utakaojitokeza!

We are working very hard on the new version of our site. It will bring a lot of new features. Stay tuned!


days

hours

minutes

seconds

Subscribe to our newsletter

Sign up now to our newsletter and you'll be one of the first to know when the site is ready:

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger
Design by Yuvinusm

5/12/16

Bunge Laanika Majipu Matano Sekta ya Afya


WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ikiahidi kutoa huduma bora za afya kwa wananchi, Bunge limeanika changamoto tano zinazokwamisha maendeleo ya sekta hiyo.
waziri wa afya ummy mwalimu
Mwaka jana, wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, Rais John Magufuli aliahidi kuimarisha huduma za afya nchini ili kila Mtanzania apate huduma bora na za uhakika.
Rais Magufuli aliahidi serikali yake itahakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati na kila kata inakuwa na kituo cha afya.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ziliainisha matatizo mbalimbali yanayoikabili sekta ya afya mara tu baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17 bungeni mjini hapa jana.
Changamoto zilizotajwa na wabunge ni pamoja na ucheleweshaji na kutolewa kidogo fedha za bajeti, uhaba na mishahara duni ya watumishi, ongezeko la vifo vya akina mama wanaojifungua, tatizo la utapia mlo na uhaba wa dawa kutokana na Bohari ya Dawa (MSD) kupewa fedha kidogo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba alisema kamati yake ilifanya uchambuzi wa matumizi ya bajeti ya 2015/16 ya wizara hiyo na kugundua kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu, fedha iliyotolewa na Hazina kwa ajili ya bajeti ya wizara hiyo haikufikia asilimia 50 ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge.
"Kamati inasikitishwa na kitendo cha serikali kutopeleka fedha zilizoidhinishwa na Bunge hili tukufu kwa wizara hii pamoja na umuhimu wake katika bajeti ya mwaka 2015/16," alisema Serukamba.
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (CCM), alisema kamati yake inaona juhudi na mpango wa serikali kujali afya za wananchi wa Tanzania zitabaki kuwa ndoto, hivyo kuendelea kuwa na taifa lisilokuwa na wananchi walio na afya bora.
Serukamba alisema Tanzania sasa ina kata 38,000, hivyo kunapaswa kuwa na vituo vya afya 38,000, lakini kamati yake imebaini vituo vya afya vilivyopo nchini kwa sasa ni 716 tu ambayo ni sawa na asilimia 18.8 ya mahitaji ya vituo vya afya kisera.
Kati ya vituo hivyo, Serukamba alisema serikali inamiliki 484, mashirika ya dini yana 141, vituo vya afya binafsi 79 na vya taasisi binafsi 12.
Alibainisha kuwa kati ya Sh. bilioni 440.642 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wizara hiyo mwaka huu, Sh. bilioni 18.196 ndio zilipelekwa, sawa na asilimia nne ya fedha zilizoidhinishwa.
"Kamati inaona serikali kutokupeleka fedha kwa wakati kunaikwamisha wizara katika kutekeleza majukumu yake ambayo ni pamoja na ununuzi wa dawa, vifaa tiba na kuwalipa watumishi katika kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kiofisi," alisema.
AJIRA, MISHAHARA AFYA
Mbunge huyo alisema nchi inakabiliwa na uhaba wa wataalam wa afya, lakini serikali imetoa kibali cha kuajiri wataalam 10,000 kati ya 30,000 waliohitimu mafunzo, sawa na theluthi moja ya wataalam waliopo ambao hawajaajiriwa.
Serukamba pia alisema madaktari wamekuwa wakisita kwenda kufanya kazi mikoani kutokana na kuwepo tofauti ya mishahara kulingana na hospitali wanazopangiwa kufanya kazi.
"Kwa mfano, madaktari wenye Shahada ya Kwanza waliomaliza masomo pamoja, wale watakaokwenda kufanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), KCMC, Bugando au Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, mishahara yao inatofautiana na madaktari wanaokwenda kufanya kazi katika hospitali ya mkoa wa Rukwa, Katavi, Ruvuma, Mara na maeneo mengine.
Hali hii inafanya madaktari wengi kukataa kwenda kufanya kazi katika hospitali za mikoa kwa sababu ya tofauti za mishahara," alisema.
KAMBI YA UPINZANI
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika wizara hiyo, Dk. Godwin Mollel, alikosoa kile alichodai Serikali ya Awamu ya Tano haijaipa kipaumbele sekta ya afya kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya wizara hiyo kwa Sh. bilioni 18 katika mwaka ujao wa fedha kulinganisha na mwaka 2015/16.
"Wakati bajeti ya taifa imepanda kwa Sh. trilioni 6.5 kutoka Sh. trilioni 22.4 katika mwaka wa fedha 2015/16, bajeti ya Wizara ya Afya imepungua. Hii ina maana kwamba huduma za afya zitakuwa mbaya na hafifu kuliko katika mwaka wa fedha unaoisha," alisema Dk. Mollel.
Alisema Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iongoze bajeti ya wizara hiyo ili angalau sekta ya afya ibakie kuwa asilimia 11 ya bajeti ya taifa kama ilivyo katika mwaka huu wa fedha.
Dk. Mollel aliitaka serikali kujipanga kuhakikisha inatenga fedha zake yenyewe kwa ajili ya sekta ya afya badala ya kuwategemea wafadhili ambao mchango wao wa kibajeti umepungua kwa asilimia 47 kutoka Sh. bilioni 374.6 mwaka 2015/16 hadi Sh. bilioni 198.4 mwaka 2016/17.
WANAWAKE 42 HUFARIKI KILA SIKU WAKIJIFUNGUA
Dk. Mollel alisema hali ya vifo vinavyotokana na uzazi nchini inatisha. Akinukuu ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya mwaka huu, Mbunge huyo alisema kina mama 1,255 hufariki kwa mwezi, sawa na 42 kila siku na wawili kila saa.
"Kama ukiwakusanya kina mama wanaofariki kutokana na uzazi kila siku, ni sawa na basi la abiria aina ya ‘Coaster’," alifafanua Dk. Mollel.
Alisema Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri serikali kuhakikisha kunakuwa na mpango madhubuti kunusuru afya ya mama na mtoto.
KILA DK 12 UTAPIAMLO HUUA MTOTO
Dk. Mollel pia alisema tatizo la ukosefu wa chakula na lishe duni nchini bado linaathiri familia nyingi hasa watoto chini ya miaka mitano.
Akinukuu utafiti wa Taasisi ya Afya Ifakara, Dk. Mollel alisema mtoto mmoja hufariki dunia kila dakika 12 kutokana na utapiamlo.
Alisema utafiti huo unabainisha kuwa zaidi ya watoto milioni 2.5 nchini wamedumaa na takribani 430,000 ni miongoni mwa walio katika hatari ya kufariki kila mwaka ikiwa hatua za haraka zisipochukuliwa.
Dk. Mollel pia alisema takwimu za Shirika la Utafiti la Twaweza zinaonyesha Tanzania sasa ni nchi ya 10 duniani kwa ukubwa wa changamoto, akilinganisha na nchi za Ethiopia (7) na Sudan Kusini (15) ambazo zimekuwa zikikumbwa na tatizo la njaa mara kwa mara.
MILIONI 44 HAWATAPATA DAWA
Mbunge huyo wa Siha (Chadema) alisema pia kiasi cha Sh. bilioni 65.1 kilichotengwa kwa ajili ya MSD kununua dawa katika mwaka ujao wa fedha, kitatosha kwa mwezi mmoja na nusu tu.
Alisema kuwa kwa kukadiria Tanzania ina watu milioni 49.8 wanahitaji matibabu, kiasi kilichotengwa kinatosha kutibu watu milioni 5.6 kwa mwaka. "Je, watu wengine milioni 44 wanaobaki, watatibiwa na nini na wapi?" alihoji Dk. Mollel.
Alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri serikali iongeze bajeti ya dawa kutoka asilimia 11 (Sh. bilioni 65.1) hadi asilimia 50 (Sh. bilioni 295.9). Ili dawa na vifaa visambazwe, Dk. Mollel alisema MSD inahitaji kupewa Sh. bilioni 114 iliyoomba kwa ajili ya kulipia mizigo bandarini na usambazaji wa dawa na vifaa tiba, lakini katika bajeti ya mwaka ujao imetengewa Sh. bilioni 35 tu.
"MSD inaidai serikali Sh. bilioni 131. Serikali imetenga Sh. bilioni 108 kulipa deni hilo, hivyo kubakiza deni la Sh. bilioni 23.
Kiasi hiki kilichotengwa kinakidhi mahitaji ya MSD kwa miezi minne tu. Je, serikali inataka dawa na vifaa tiba viozee kwenye bohari na bandarini kwa miezi mingine?" alihoji Dk. Mollel.