5/9/16

Dar Kuongeza madampo kukabiliana na uchafu Jijini
Na Lilian Lundo
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam limeazimia kuongeza idadi ya madampo na kurekebisha miundombinu ya dampo la Pugu ili kuhakikisha jiji linakuwa safi.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Isaya Mwita alisema Baraza hilo limeazimia kuongeza na kurekebisha miundombinu baada ya ziara walioifanya na kugundua mapungufu katika dampo la Pugu.
“Tumegundua kuna udhaifu mkubwa katika dampo la Pugu, magari yanayopeleka taka yananasa barabarani hivyo tukaona kuna sababu ya kutengeneza miundombinu, hivyo tumetenga milioni 700  kwenye bajeti hii ili kutengeneza barabara hiyo,”alisema Mhe. Mwita.
Aidha, alisema kwamba baraza limetenga kiasi cha shilingi milioni 200 katika bajeti ya 2016/17 ili kununua eneo Mkuranga kwa ajili ya dampo, huku wakiendelea na mchakato wa kuongeza madampo mengine Kigamboni na Kisarawe ili kuhakikisha taka zote zinazozalishwa ndani ya jiji la Dar es Salaam zinapelekwa kwenye madampo badala ya kuzagaa mitaani.
Kwa upande wake, Naibu Meya wa jiji la Dar es Salaam Mhe. Mussa Kafana alisema kuwa, suluhisho la kumaliza taizo la uchafu si kuwa na dampo tu bali ni kuwepo kwa vifaa maalumu vya kuhifadhi taka. Hivyo baraza likaamua kuwepo na vyombo vya kuhifadhia taka katika mitaa yote ya jiji la Dar es Salaam ili kudhibiti uzagaaji wa taka.
Usafi ni moja ya kipaumbele cha Rais wa Awamu ya Tano Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambapo kwa mara ya kwanza alitangaza siku ya Uhuru wa Tanzania (Tisa Desemba) iazimishwe kwa kufanya usafi nchi nzima ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu pamoja na kuiweka Tanzania katika hali ya usafi.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts