5/29/16

Dar sasa kujengewa ‘fly- over’ tisa

SERIKALI iko mbioni kujenga barabara za juu (fly-over) saba mojawapo ikitarajiwa kujengwa Mwenge, ili kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.
Kuongeza barabara hizo kutalifanya jiji kuwa na fly-ova tisa, baada ya ujenzi wa nyingine mbili kufanyika katika makutano ya barabara ya Ubungo na Tazara.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alieleza jana na kuongeza kuwa ujenzi huo, utaanza mwishoni mwa mwaka huu na kwamba mazungumzo na Kampuni ya Mabe Bridge ya Uingereza yanaendelea.

Alisema mazungumzo ya kujenga barabara hizo yapo kwenye hatua nzuri na inatarajiwa kwamba mradi utajenga fly-ova nne za watembea kwa miguu na tatu za magari.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha wizara hiyo, Waziri alisema ujenzi wa barabara hizo, utatumia miezi mitatu hadi sita kukamilika na zitagharamiwa na fedha za ndani na kwamba ujenzi wake unatarajiwa kuanza Desemba mwaka huu.

“Wataalamu wanaendelea kubaini maeneo mengine yatakayojengwa fly- ova hizo, na kwa sasa eneo la Mwenge ndilo ambalo wamekubali kuweka barabara za juu”,alisema Profesa Mbarawa.

Barabara za juu zimeanza kujengwa jijini Dar es Salaam, eneo la Tazara na baada ya kukamilika kwa fly- ova hiyo nyingine itajengwa Ubungo.

Aidha, Waziri amekagua maendeleo ya utoaji huduma katika Daraja la Nyerere na kuagiza vitengenezwe vitambulisho vya msimu vitakavyowawezesha watumiaji wa daraja kulipa tozo kwa miezi sita au mwaka ili kupunguza msongamano wa kulipa kila siku.

“Hakikisheni mnatengeneza na kuuza kadi za kuvukia katika daraja sehemu mbalimbali ili kuwawezesha watumiaji kupata huduma hiyo kabla ya kufika darajani”, alisema Prof. Mbarawa.

Pia alimtaka Mtendaji Mkuu wa Daraja la Nyerere, Gerald Sondo, kuhakikisha tozo zinakusanywa inavyostahili na kupanga njia maalumu za kupita magari makubwa na madogo ili kuwezesha huduma ya kupita darajani kuwa ya haraka.

“Magari yote yanayopita katika daraja hili yakiwamo ya serikali ni lazima yalipe tozo inayostahili isipokuwa yale yenye vibali maalumu yakiwemo ya Jeshi la Wananchi, Zimamoto, Polisi, na yanayobeba wagonjwa ”, alisema.

Kwa upande wake Sondo alitaja tatizo la kubaini magari yenye vibali maalumu, malalamiko ya magari ya abiria (daladala), uelewa mdogo wa matumizi ya daraja na mazoea ya kupita bila ya kulipa tozo ni moja ya changamoto zinazowakabili.

Aprili 19, mwaka huu Daraja hilo lenye urefu wa mita 680 na barabara unganishi zenye kilomita 2.5 lilizinduliwa na Rais John Magufuli.

Ujenzi wa daraja hilo umefanywa na kampuni ya China Railway 15 Group ikishirikiana na ile ya China Bridge Engineering Group kwa gharama ya Shilingi bilioni 214.6.
Weka Maoni Yako Hapa
Share:

Advertisment

Habari Mpya

Follow us on Facebook

Popular Posts

Blog Archive

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger Design by Yuvinusm