5/27/16

Homa ya ini : Ugonjwa hatari uliopuuzwa na jamii nyingi-Ufahamu Hapa

 
Watu wengi hawana elimu kuhusu ugonjwa wa homa ya ini ambao unaonekana kuwa hatari kuliko magonjwa yanayoogopeka kama vile Ukimwi.
Hali hii inaashiria kuwa homa ya ini ni ugonjwa uliosahaulika lakini ni wa hatari kwa jamii hivyo inapaswa kuchukua hatua.
Mratibu wa shughuli za Maabara Hospitali ya Halmashauri ya mji Tarime Joshua Makoa anasema kuwa wilayani, ugonjwa huo umeonekana kuwapata watu wengi ukilinganishwa na magonjwa mengine kama Virusi Vya Ukimwi (VVU) na kaswende.
Makoa anaeleza kuwa kwa mwaka 2014 watu 578 walijitokeza kupima damu kwa hiari ambapo 83 walibainika kuwa na ugonjwa huo.
Jambo la ajabu, anasema kati ya hao, hakuna hata mmoja aliyekutwa na maambukizi ya VVU ama kaswende.
“Idadi ni kubwa sana inaonyesha ni kiasi gani ugonjwa huo unawakumba watu wengi ukilinganisha na magonjwa mengine,” anasema Makoa.
Homa ya Ini ni nini?
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa homa ya ini ama kama inavyojulikana kitaalamu hepatitis B, ni ugonjwa unaotokana na virusi. Hivi uvimbe katika ini ambao baadaye huwa ni chanzo cha saratani ya ini. Saratani hii haina tiba mwafaka.
Inakadiriwa watu milioni 350 duniani wameathirika na ugonjwa huo ambapo wagonjwa 620,000 hupoteza maisha kila mwaka.
Kinachosababisha ugonjwa
Mratibu huyo wa maabara anasema kuwa ugonjwa wa homa ya ini husababishwa na virusi waitwao hepatitis B (HBV) ambao hukaa katika ini, damu na baadhi ya majimaji mwilini. Hugunduliwa kwa uchunguzi wa damu.
Makoa anasema kuwa ugonjwa huo huambukizwa kwa njia mbalimbali kama vile kujamiiana bila kinga, mapenzi ya kunyonyana ndimi, wakati wa kujifungua mama mwenye ugonjwa huo anaweza kumuambukiza mwanaye, kuchangia damu, vitu vya ncha kali kama sindano, wembe na hata kuchangia miswaki.
Dalili
Makoa anaonya kuwa mtu hapaswi kusubiri hadi aone dalili. Ni vyema akapima na kugundua tatizo mapema.
Anasema dalili zikionekana inaashiria tayari mgonjwa yupo kwenye hali mbaya ya kuathirika.
“Watu wajenge mazoea ya kupima damu mara kwa mara ili wawe na uhakika hawana maambukizi,” anasema.
Dalili za wazi anasema ni uchovu, kichefuchefu, mwili kuwa dhaifu, homa kali, kupoteza hamu ya kula, tumbo kuvimba na kuzidi mwili wake.
Dalili nyingine ni kutuna kwa misuli, kupungua uzito, maumivu makali ya tumbo upande wa ini, homa ya njano, macho na ngozi kuwa vya njano na mkojo kuwa na rangi nyeusi. Makoa anataja kinga ya ungonjwa huo kuwa ni kupata chanjo, kutumia kinga wakati wa kujamiana, kuacha kuchangia vitu vya ncha kali kama sindano, wembe na vinginevyo.
Makoa anasema kuwa ugonjwa huo hauna tiba ila anasisitiza kuwa mgonjwa akiwahi hospitali atapatiwa dawa za kupambana na virusi ili kupunguza nguvu za kushambulia ini.
Wananchi wailalamikia Serikali
Baadhi ya wananchi wanaitupia lawama Serikali kwa kile wanachoeleza ndiyo inachangia watu kupoteza maisha kwa kushindwa kuielimisha jamii hasa maeneo yanayoonekana yana maambukizi makubwa.
Mwita Marwa mkazi wa Nyamongo anasema: “Nyamongo tuna kituo cha afya ambacho hakiruhusiwi kupima damu mpaka hospitali ya wilaya hali hiyo ni hatari kwa kuwa watu wanalazimika kupeleka wagonjwa zahanati binafsi, huko ndiyo wanaotoa huduma ya kuongezewa damu, ambayo inawezekana si salama,” anasema.
Bhoke Marwa mkazi wa Muriba anaitaka Serikali iviwezeshe vituo vya afya kuwa na uwezo wa kuongezea watu damu salama. Alisema hiyo itasaidia kwa sababu watu wengi huona ni bora wakatibiwe hospitali za watu binafsi ambako wakati mwingine hakuna uhakika wa damu salama.
Diwani wa Kata ya Nyansicha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati za huduma za jamii Elimu, Afya na Maji, Samwel Muhono anakiri kwamba ipo haja ya vituo vya afya kuboreshwa badala ya kutegemea hospitali ya wilaya pekee.
Muhono anaongeza kuwa vituo vya afya vikiboreshwa vinaweza kuwa na benki ya damu na hii itasaidia wengi hasa kinamama wanapoenda kujifungua.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga anasema pamoja na maboresho ya vituo vya afya, hospitali ya wilaya nayo inapaswa kuongezewa uwezo.
Anasema kuwa bado huduma zinazotolewa na hospitali ya wilaya haziridhishi.
Anasema kuna haja sasa Halmashauri ya Mji wa Tarime na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kushirikiana kuhakikisha hospitali inaboreshwa na kutoa huduma stahiki ili wananchi wawe na imani.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts