5/29/16

Hospitali Yalaza Wagonjwa na Maiti Chumba Kimoja


JE, umewahi kulala chumba kimoja na maiti walau kwa siku mbili katika maisha yako? Ni hisia gani hukujia pindi ukiwazia kukutana na jambo hilo?
Kama bado hujafikiria hilo, basi ni hali hiyo ndiyo inayowakuta hivi sasa wagonjwa wanaolazwa katika Kituo cha Afya cha Bulugwa kilichopo katika Halmashauri ya Ushetu, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ambao wanakabiliwa na hali ngumu ya kulala na maiti katika chumba kimoja na kuwasababishia mauzauza kila uchao.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa hali hiyo ya kulala wagonjwa na wafu katika chumba kimoja, imedumu kwa miaka takribani tisa tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, hali inayodhihirisha kuwa serikali ya sasa ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli italazimika kufanya kazi ya ziada ili kutimiza ahadi zake za kuboresha huduma za afya ilizozitoa wakati wa kampeni za kueleka uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.

Aidha, imebainika kuwa baadhi ya wagonjwa wanaolazwa katika kituo hicho hujikuta katika wakati mgumu zaidi nyakati za usiku kwakuwa hofu ya kifo huwajaa kutokana na woga wa kulala na maiti na pia mauzauza yatokanayo na ndoto za kuogofya.

“Kwakweli hali ni ngumu, kulala na maiti siyo kazi ndogo kwa sababu kila giza linapoingia mambo huwa magumu zaidi.

Ndoto za mauzauza ya kifo zinazotokana na woga wa kulala pamoja na maiti huwa hazikwepeki,” alisema mmoja wa wagonjwa waliokutwa kwenye chumba kimojawapo kinachotumika kama wodi na pia mahala pa kuhifadhia maiti kwenye kituo hicho cha afya.

“Ukilala na maiti chumba kimoja unatamani asubuhi ifike na usiku huwa ni mrefu sana … ni vyema serikali ikaangalia namna ya kumaliza tatizo hili,” mgonjwa mwingine alisema

Nipashe imebaini kuwa chanzo cha kuwapo kwa hali hiyo, ni kutowahi kujengwa kwa mochwari tangu kituo hicho kianzishwe baada ya zahanati iliyokuwapo awali kupandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya kinachohudumia wagonjwa wengi zaidi.

Katika uchunguzi huo uliohusisha pia ziara iliyomfikisha mwandishi kwenye kituo hicho, Nipashe imebaini kuwa kinachofanyika pindi mgonjwa anapofariki dunia, ni kuletwa kwa pazia zito la kijani na kuzungushwa kwenye kitanda cha mwili wa marehemu kabla ya kusubiri ndugu zake waje wauchukue mwili huo.

“Hali hii inatisha. Fikiria unashuhudia mgonjwa mwenzio aliyekuwa kitanda cha jirani akirusha miguu kabla ya kufa, halafu wakati ukijitahidi kusahau hali hiyo, unajikuta ukiwa katika mtihani mwingine mzito wa kuendelea kulala na marehemu kwa siku moja na hata zaidi kutegemeana na wepesi wa ndugu kuchukua maiti ya mpendwa wao,” alisema mmoja wa wagonjwa aliyekutwa amelazwa katika chumba ambacho pia huhifadhiwa maiti.

“Hali hii inasababisha ndoto nyingi za vitisho. Wakubwa waje watusaidie tafadhali,” mgonjwa mwingine awa kike aliyekataa kuandikwa jina lake gazetini aliiambia Nipashe juzi.

Mgonjwa aitwaye Vumilia Simon, ambaye pia alikutwa amelazwa hospitalini hapo, alisema kuwa Mei 24 mwaka huu, wagonjwa wawili walifariki akiwamo mtoto ambaye mwili wake ulichukuliwa siku hiyo, lakini mwili wa mtu mzima ulibaki wodini kwa siku nzima.

“Binafsi nilijawa na huzuni na pia kuingiwa na hofu kubwa… nilijisikia vibaya sana kulala chumba kimoja na maiti na kuna wakati zilinijia hisia za kutaka kutoroka. Ni vizuri hali hii ikasitishwa kwa kujenga chumba cha kulala wagonjwa,” alisema Simon.

Mgonjwa mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Justina William, alisema yeye na wagonjwa wengine kadhaa waliolazwa hapo hushindwa kupata usingizi kutokana na woga wa kulala chumba kimoja na maiti na hivyo, ni vizuri serikali ikaongeza nguvu katika kumaliza tatizo hilo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Bulugwa, Paulina Ndutu, alisema wagonjwa wanaolazwa katika kituo hicho wamekuwa wakihangaika na kupatwa na hofu kubwa kutokana na tatizo hilo lililodumu kwa miaka tisa na sasa wanasubiri utekelezaji wa ahadi kadhaa za viongozi wa halmashauri kuhusiana na namna ya kumaliza tatizo hilo.

MADAKTARI, WAUGUZI WANENA
Akizungumza na Nipashe juzi, Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk. Peter Dalali, alikiri kuwapo kwa tatizo la ukosefu wa chumba cha kulaza maiti tangu kianzishwe mwaka 2007 na kwamba, hadi sasa, wanachojua ni kwamba kuna jitihada mbalimbali zinaendelea kufanywa na uongozi wa halmashauri yao ya Ushetu ili kuondokana na hali hiyo.

Alisema kuwa wao hawafurahishwi na hali hiyo ya kuacha maiti kwenye wodi wanazolaza wagonjwa lakini hawana namna ya kufanya, wakisubiri kujengwa kwa chumba rasmi cha maiti.

Alisema kituo chao kinahudumia wastani wa wagonjwa wa nje 50 kwa siku na pia hulaza wengine wa idadi kati ya 13 na 15 kwa siku.

Dk. Dalali alisema kuna umuhimu mkubwa wa kupatiwa chumba cha maiti kwa sababu kituo chao hicho ni kikubwa na hutegemewa na wananchi wanaopelekwa hapo wakitokea katika zahanati za kata za Bugomba, Igwamanoni, Sabasabini, Mpunze, Butibu, Nyankende, Nyalwelwe na pia maeneo mengine ya jirani na kata hizo.

“Wagojwa wanaolazwa katika kituo cha Afya Bulugwa, walianza kulala na maiti katika chumba kimoja au wodi moja tangu 2007… sasa ni takriban miaka tisa tangu waanze kupata shida hii,” alisema Dk. Dalali.

“Madaktari hatuwezi kuacha kuwatibu na kuwalaza wagonjwa hata kama mwili wa marehemu upo ndani ya wodi, tunachofanya ni kuzungushia kwa shuka maalum kwa sababu hakuna chumba cha kuhifadhia maiti. Kwakweli hakuna namna nyingine kwakweli,” alisema.

Wakizungumza bila kutaja majina yao, baadhi ya wauguzi walisema hali huwa ngumu zaidi pale inapotokea ndugu wa marehemu wakachelewa kuchukua mwili wa mpendwa wao, na hasa wanapokufa watu zaidi ya wawili.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu, John Dutu, alikiri kuwapo kwa tatizo hilo lakini akiongeza kuwa suala hilo ni la kiutendaji na kisera, hivyo yeye hawezi kuwa na majibu ya kujitosheleza.

MKUU WA WILAYA
Akielezea hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Vita Kawawa, alikiri kutambua kuwapo kwa tatizo hilo kwa sababu alishatembelea kituo hicho na kujionea hali halisi.

"Baada ya kupata taarifa ya wagonjwa na maiti kulala pamoja, nilienda kuangalia hali halisi na kuagiza eneo maalum litengwe kwa ajili ya ujenzi wa ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti," alisema Kawawa.

Kawawa aliongeza kuwa ili kukamilisha ujenzi huo wa chumba cha maiti, ofisi yake itatoa mifuko 10 ya saruji na kuutaka uongozi wa halmashauri kuhakikisha wanatenga eneo na kufanikisha jengo hilo ili hatimaye kuwaondolea wananchi adha iliyopo sasa ya wagonjwa kulala na maiti.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts