5/17/16

Hotuba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa kufungua mafunzo ya uhakikk wa mikatabaya ununuzi wa umma.

HOTUBA YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI, NDUGU GEORGE M. MASAJU WAKATI WA KUFUNGUA MAFUNZO KUHUSU UHAKIKI WA MIKATABA YA UNUNUZI WA UMMA, DODOMA,
TAREHE 16 – 25 MEI, 2016
____________________________
Dkt. Medard Kalemani, Naibu Waziri,
Wizara ya Nishati na Madini,
Mkurugenzi wa Mikataba,
Mawakili wa Serikali Wafawidhi,
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,


Kwa namna ya pekee ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia uhai, uzima na afya na hatimaye kutuwezesha kufika hapa Dodoma salama kwa ajili ya kushiriki katika mafunzo haya muhimu kuhusu uhakiki wa mikataba ya ununuzi. Niwashukuru Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuona umuhimu wa mafunzo haya kwa kulipia gharama zote kuhusiana na mafunzo haya. Aidha, ninapongeza Divisheni ya Mikataba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa maandalizi mazuri ya mafunzo haya.


Nimefahamishwa kuwa mafunzo haya yatafanyika katika makundi matatu na kwa tarehe tofauti. Makundi hayo ni Mawakili wa Serikali Wafawidhi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mikoa ya Tanzania Bara ambao mafunzo yao yanafanyika leo tarehe 16 hadi 18 Mei, 2016; Mawakili wa Serikali ambao mafunzo yao yatafanyika tarehe 19 hadi 21 Mei, 2016 na Maafisa Ugavi na Maafisa Sheria kutoka Halmashauri za Iramba, Manyoni, Singida Vijijini, Singida Mjini, Bahi, Chamwino, Chemba, Dodoma Mjini, Dodoma Vijijini,Kilosa,Morogoro Vijijini, Morogoro Mjini, Mvomero, Igunga, Nzenga, Sikonge,Uyui na Tabora Mjini pamona na TANROADS na TANESCO ambao mafunzo yao yatafanyika tarehe 23 hadi 25 Mei, 2016. Ninawashauri mtumievizuri nafasi hii adimu kwa kujifunza na kubadilishana mawazo, kushirikishana uzoefu na utaalam wenu katika masuala mikataba.


Ndugu Washiriki;
Kama mnavyofahamu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni ya Kikatiba na imeanzishwa chini ya Ibara ya 59 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiye mshauri mkuu wa Serikali katika masuala ya kisheria. Majukumu haya yanaweza kutekelezwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwenyewe au kupitia wasaidizi wake ambao ni Naibu Mwanasheria Mkuu, Maafisa Sheria (Law Officers) na Wanasheria wa Serikali (State Attorneys). Dira (Vision) ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kuwa Ofisi bora ya Kisheria nchini wakati Dhima (Mission) kuu ya Ofisi hii ni kutoa huduma bora za kisheria kwa serikali na wananchi kwa ujumla kwa lengo la kuwezesha, kuimarisha na kuendeleza utawala wa Sheria, Haki za Binadamu, Uendeshaji wa Mashauri ya JInai na Madai pamoja na Uandishi wa Sheria ili kudumisha amani na ustawi wa uchumi wa nchi.


Majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yameainishwa katika Katiba na sheria mbalimbali, ikiwemo Ibara za 59, 59A and 59B za Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Sura ya 2 ya sheria za Nchi; Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (The Office of the Attorney General (Discharge of Duties) Act), Sura 268; Sheria ya Uendeshaji Mashtaka ya mwaka 2008 (The National Prosecutions Services Act2008); Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (The Basic Rights and Duties Enforcement Act), Sura ya 3; Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Kabidhi Wasii (The Administrator General (Powers and Functions Act), Sura ya 27; Sheria ya Ubia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafisi ya mwaka 2010 (The Public Private Partnership Act, 2010); Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 (The Public Procurement Act, 2011) na Sheria nyinginezo.
Ndugu Washiriki;
Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni zake imeweka bayana taratibu za kufuata hadi Mkataba kukamilika. Katika hatua hizo nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewekwa katika Kifungu cha 60 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni ya 59 ya Kanuni za Ununuzi wa Ummaza Mwaka 2013. Hapo awali Kanuni ya 59 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013 ilikuwa inaelekeza kwamba Mikataba yote ya ununuzi wa umma ambayo thamani yake inafikia shilingi milioni hamsini au zaidi ifanyiwe uhakiki na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya kusainiwa. Kanuni hizo zimerekebishwa kupitia Marekebisho ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2016 (The Public Procurement (Amendments) Regulations,) Government Notice Na. 121/2016 zilizochapishwa tarehe 22 Aprili, 2016 na sasa mikataba ya ununuzi ambayo inatakiwa kuhakikiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Kanuni 59(1) ya Kanuni hizo ni ile yenye thamani ya kuanzia shilingi bilioni moja au zaidi na mikataba ya ununuzi inayohusu ushindani wa zabuni ya kimataifa.


Aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya 59(2) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma, mkataba wowote wa aina hiyo ambao haukufanyiwa uhakiki na Mwanasheria Mkuu utakuwa batili.


Aidha, Kanuni ya 59(5) inaelekeza kuwa Afisa masuhuli anapaswa kuhakikisha kuwa ushauri wa kisheria uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati akihakiki mkataba husika umezingatiwa ipasavyo na kuingizwa katika rasimu ya mkataba.


Mikataba chini ya thamani ya shilingi bilioni moja inafanyiwa upekuzi na Afisa Sheria wa Taasisi ya Manunuzi husika kama inavyoelezwa katika Kanuni ya 60(1). Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni ya 60(4) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma, Taasisi ya Manunuzi haizuiwi kuomba ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa jambo lolote linalohusu mkataba unaoweza kuhakikiwa na Afisa Sheria (Legal Officer) wa taasisi husika.


Kuongezeka kwa thamani ya mikataba ambayo inafanyiwa uhakiki na wanasheria wa Taasisi ya Manunuzi kunaonesha namna wanasheria hao wanavyotakiwa kuwa makini, kutumia uweledi na kuwa waadilifu katika kutekeleza wajibu huo ili Taasisi zisiingie katika mikataba ambayo haijazingatia sheria zilizopo na ambayo haina manufaa kwa taasisi husika. Kwa sababu hiyo sasa, Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013 kama zilivyorekebishwa kupitia The Public Procurement (Ammendments) Regulations, 2016 katika Kaununi ya 60(2)zinaelekeza kwamba Afisa Sheria wa Taasisi ya ununuzi anayehakiki mikataba ya ununuzi atawajibika kuzingatia masharti ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sheria nyinginezo zinazohusika na mikataba husika na Kanuni za Maadali na Mienendo ya Kitaaluma Maafisa Sheria katika Utumishi wa Umma.


Kutokana na kuongezeka kwa thamani ya mikataba inayohakikiwa na Wanasheria wa Taasisi ya Manunuzi ni wazi kwamba kuna umuhimu wa Maafisa Sheria haokujengewa uwezo kuhusu uhakiki wa mikataba kwani iwapo watashindwa kutekeleza wajibu huo ipasavyo watawajibishwa kwa watachukuliwa hatua za kinidhamu au kisheria ipasavyo.


Wanasheria wa Serikali wanaohakiki mikataba yote nao wanawajibika kuzingatia Sheria zinazohusiana na mikataba husika pamoja na Maadili ya Wanasheria wa Serikali na wanasheria wengine katika Utumishi wa Umma kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 27 cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, 2005 pamoja na Jedwali la sheria hiyo.


Utekelezaji wa majukumu ya Wanasheria wa Serikali na Maafisa Sheria unasimamiwa na Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, 2005 ambayo, pamoja na mambo mengine, inawataka Wanasheria wote katika Utumishi wa Umma kuzingatia Kanuni za Maadali na Mienendo ya Kitaaluma kwa Afisa wa Sheria (Law Officer), Wakili wa Serikali (State Attorney) na Afisa Sheria(Legal Officer) yaliyoko katika Jedwali la Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, 2005. Maadili hayo ni pamoja na; uwezo wa kumudu majukumu (competency), uadilifu (intergrity), uaminifu (honesty), utunzaji wa siri (confidentiality), ubora wa huduma (quality of service), haki na usimamizi wa haki (justice and administration of justice) na uvaaji wa mavazi yaheshima (appropriate presentation and attire).


Ndugu Washiriki;
Kwa kuwa Divisheni ya Mikataba iko katika Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pekee, mikataba hiyo imekuwa ikipelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya kuhakikiwa. Hatua hii imekuwa ikisababisha wadau wetu na hasa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa, Jiji na wengine walioko mikoani kusafiri na kupeleka mikataba Dar es Salaam kwa ajili ya uhakiki. Mbali na kuongeza gharama kwa halmashauri na wadau wenine,utaratibu huo unaweza kuchelewesha mradi kuanza mapema.


Kutokana na changamoto hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliona umuhimu wa kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali wa Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali zilizoko Mikoani ili hatimaye baadhi ya Mikataba kutoka kwa wadau walioko wilayani na mikoani iwe inapelekwa katika Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali zilizoko mikoani. Ninapenda kuwashukuru tenaShirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kukubali kugharimia gharama za mafunzo haya. Tunatambua kuwa taasisi hizi ni wadau muhimu katika jambo hili kwani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa ikipokea mikataba ya miradi mingi kutoka kwao.


Ndugu Washiriki;
Ninatambua kuwa katika siku mtakazokuwa hapa mtaweza kufundishwa masuala yanayotakiwa kuangaliwa au kuzingatiwa wakati wa kufanya uhakiki. Kamusi ya Kiingereza inatafisri kuwa vetting ni “to examine carefully and critically for faults or errors”. Tafsiri rahisi ni ‘kuchunguza kwa makini makosa au upungufu’. Upekuzi au Uhakiki wa mikataba huongozwa na Sheria na Kanuni katika kubainisha masuala ya jumla ambayo hutumika katika mikataba yote ya ununuzi na yale ambayo ni mahususi kwa ajili ya mikataba mbalimbali kama vile Works, Goods, Services au Consultancy. Kazi ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ni katika kuhakiki mikataba ni kuchunguza kwa makini kama taratibu za manunuzi zilifuatwa; kuangalia ibara mbalimbali za mkataba kama zimewekwa sahihi ili kuondoa uwezekano wa athari hasi kwa Serikali; na kujiridhisha kama mikataba husika inakidhi au kuzingatia maslahi ya Umma au Taifa. Hivyo, ninapenda kuwakumbusha kuwa kwa mujibu wa vifungu vya 47 na 63 vya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2013, ununuzi wote wa umma na uuzaji unaofanywa kwa njia ya zabuni unatakiwa kuendeshwa kwa mujibu wa misingi iliyoainishwa katika Sheria hiyo na pia ununuzi nauuzaji wa kwa njia ya zabuni unatakiwa kuendeshwa kwa namna ambayo itaongeza ushindani na kuleta nafuu, ufanisi, uwazi na thamani ya fedha.Kwa msingi huo, hakikisheni kwamba Taasisi husika ya Manunuzi imezingatia misingi hiyo kwa kila mkataba mnaoufanyia uhakiki. Lakini siyo Mikataba yote ya manunuzi inapaswa kushindanishwa hadharani. Msomeni na kukielewa vizuri Kifungu cha 63 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma, 2011 katika muktadha wa vifungu vingine vya sheria hiyo.


Ninawakumbusha pia kuwa makini na kutoa ushauri kwa uadilifu na uweledi wahali ya juu wakati wa kutekeleza jukumu hilo mkizingatia kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 23 cha Sheria ya Utekelezaji Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ushauri unaotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndio msimamo wa Serikali hadi utakapoondolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwenyewe au Mahakama.


Ndugu washiriki;
Ili Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itekeleze wajibu huo wa kuhakiki mikataba kwa ufanisi ipasavyo, Wizara, Taasisi na Idara za Serikali zinazoleta Mikataba katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali zinakumbushwa kuzingatia ipasavyo masharti ya kifungu cha 22 cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, 2005,Kanuni ya 13(1) ya Kanuni za Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, 2006 inayoelekeza namna ya kupata ushauri katika Ofisi hiyo kwa kuainisha maelezo muhimu kuhusu mkataba husika.Haitoshi kuandika barua na kuiomba Ofisi kuhakiki mkataba husika pasipo kutoa maaelezo muhimu au taarifa zinazojitosheleza kuhusiana na mkataba huo au jambo linalohitaji kutolewa ushauri wa kisheria ili Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serkali itoe ushauri wake ikiwa well informed.


Masharti yanayoitaka Taasisi inayoomba ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa taarifa inayotosheleza pamoja na ushauri wa taasisi kuhusu suala husika yamewekwa pia katika Kanuni ya 60(5) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma ambayo inaelekeza ifuatavyo;
“Where the legal advice of the Attorney General is requested in relation to the formal contract refered to under sub- regulation (4), the procuring entity shall state clearly the matters and issues involved, together with a legal opinion from within the procuring entity”.


Utekelezaji wa masharti haya ni muhimu kwani kama nilivyoeleza awali unaiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa ushauri ikiwa well informed. Pia, utaratibu huo unaisaidia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa ushauri unaoombwa mapema badala ya kuiomba tena Taasisi husika kuwasilisha taarifa inayokosekana au inayotakiwa. Ikumbukwe kwamba masharti hayo kuhusu kutoa taarifa inayotosheleza wakati wa kuomba ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali yameainishwa pia katika Kanuni ya 96 yaKununi za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003 na Kanuni B.11 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009.


Vile vile, napenda kutumia nafasi hii kuzikumbusha Wizara, Idara naTaasisi za Serikali kuzingatia ipasavyo masharti ya kifungu cha 20(1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, 2005 pale zinapohitaji huduma za kisheria kutoka nje ya Ofisi ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kifungu hicho kinaelekeza kuwa Mkataba wa utoaji huduma ya kisheria kwa Wizara au Taasisi ya Serikali uingiwe baada ya kupata kibali kwa maandishi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Ninanukuu:
“20.-(1) The engagement of consultants by any Ministry, Government Department or Agency for rendering legal services shall be made after obtaining written approval of the Attorney General in respect of issues that requires consultancy.”
Ndugu Washiriki;
Mwisho, ninapenda kuwakumbusha kwamba ninyi ni watumishi wa umma na mnaongozwa na Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2003 kama walivyo watumishi wengine wa umma. Kwa msingi huo, ninyi ni sehemu ya Serikali na nafasi yenu katika Serikali ni kubwa. Kwa Mawakili wa Serikali, umuhimu wenu unatokana na nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenye Serikali kama ilivyowekwa wazi na Katiba. Uwepo wa Mwanasheria Mkuu ni muhimu kwa kuwa yeye ndiye mshauri mkuu wa Serikali juu ya mambo ya kisheria na ninyi ndio mnaomsaidia kutekeleza jukumu hilo kwenye maeneo yenu ya kazi. Haishangazi kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiye anayekuwa Afisa wa kwanza wa Serikali kuteuliwa na Rais mara tu Rais anapokuwa anaunda Serikali mara baada ya kuwa ameapishwa kuwa Rais. Hii ni kwa sababu shughuli zote za Umma zinaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi. Ndiyo maana Mwalimu J.K. Nyerere aliwahi kusema kwamba, “Serikali ni Sheria. Hakuna kitu kinaitwa Serikali bila Sheria na Sheria zikishatungwa lazima zifuatwe”.


Hivyo, ninyi ni sehemu ya uamuzi wowote unaotokana na utendaji wa Serikali kwa ujumla. Kwa mujibu wa Ibara ya 6 na 151 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali maana yake ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar au Halmashauri ya Wilaya au ya Mji, na pia mtu yeyote anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya Serikali au Halmashauri. Hali hiyo inawalazimu kutetea na kutekeleza maamuzi sahihi ya Serikali katika utekelezaji wa majukumu yenu ikiwemo uhakiki wa mikataba. Kutokana na umuhimu wenu, mnao wajibu wa kuwa kioo cha tabia njema miongoni mwa watumishi wa umma kama jamii nzima inavyowatarajia.


Ndugu Washiriki;
Kazi niliyoombwa kufanya ni kufungua Mkutano huo. Nimeona vyema kuwakumbusha haya ili yaangaliwe na kuzingatiwa ipasavyo wakati wa utekelezaji wa majukumu yetu. Baada ya kusema hayo sasa natamka rasmi kuwa mafunzo haya kuhusu uhakiki mikataba ya ununuzi yamefunguliwa rasmi.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts