5/4/16

Hotuba ya Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu kutoka Dodoma -Soma Hapa

AuS97vtl5MZP_Q3RKRzab0Oh_zhQsu0knv3LuwZ5rrcy
HOTUBA YA MHE. UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA UZINDUZI WA KITUO CHA MATIBABU KILICHOPO HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA DODOMA TAREHE 4/5/2016
Selemani Jafo, Naibu Waziri TAMISEMI,
 • Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
 • Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,
 • Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya,
 • Katibu Tawala wa Mkoa,
 • Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dkt. Margaret Mhando na Timu ya Wataalamu kutoka Makao Makuu ya Wizara,
 • Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma,
 • Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma,
 • Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima, ya Afya, Bw. Benard Konga,
 • Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
 • Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali, Balozi Job Lusinde,
 • Viongozi na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,
 • Viongozi kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,
 • Meneja wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Kanda ya Kati,
 • Mwakilishi wa Mradi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa Dodoma (HPSS),
 • Ndugu Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali,
 • Wageni Waalikwa,
 • Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha hapa kwa ajili ya tukio hili muhimu, katika historia ya utoaji wa huduma za matibabu nchini. Pili, niwashukuru sana waandaaji wa shughuli hii kwa kunialika kuwa mgeni rasmi na kwa maandalizi mazuri. Hongereni sana.
Kipekee, napenda kuushukuru Uongozi Mzima wa Mkoa wa Dodoma, chini ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Jordan Rugimbana kwa makaribisho mazuri. Kwa sisi ambao mara kwa mara tunakuwa hapa kikazi hasa katika kipindi hiki cha Bunge la Bajeti, tunaona kazi kubwa mnayofanya katika maeneo mbalimbali hasa katika huduma za jamii ikiwemo utoaji wa huduma za afya.
Mhe. Mkuu wa Mkoa na Wageni Waalikwa,  
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alipotukabidhi jukumu la kusimamia Wizara hii, kazi yetu ya mwanzo na ambayo tunaendelea kuifanya katika maeneo mbalimbali nchini, mijini na vijijini, ni kutembelea vituo vya matibabu na kuzungumza na watumishi na wananchi, kuhusu upatikanaji wa huduma za matibabu. Jambo moja tulilolibaini kwa haraka ni kuwa Halmashauri nyingi hasa za Manispaa hawana Hospitali za Wilaya. Ni ukweli usiopingika kuwa, baadhi ya Halmashauri hasa zile mpya, hawana hospitali, hali inayosababisha wagonjwa wengi kutibiwa katika Hospitali za Rufaa ngazi ya Mkoa na hivyo kuongeza idadi ya wagonjwa katika Hospitali hizo.
Kwa kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ya HAPA KAZI TU ni kuboresha huduma kwa kuzingatia uwazi, uadilifu na uwajibikaji wenye matokeo, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI itaendelea kuimarisha huduma katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Wilaya ili kuleta uwiano wenye tija wa upatikanaji wa huduma bora.
Mhe. Mkuu wa Mkoa na Wageni Waalikwa,  
Mkoa wa Dodoma, mbali ya kuwa ni makao makuu ya nchi yetu, ni Mkoa ambao unapata wageni na wasafiri wengi wanaofika kikazi au kimatembezi. Vilevile, ni Mkoa unaofikika kirahisi zaidi na umepakana na wilaya nyingi za mikoa ya jirani ambazo wakazi wao wanatibiwa katika Mkoa huu. Tunapozindua kituo hiki cha matibabu leo hii, ninafarijika sana kwa sababu ninayo imani kubwa kuwa, huduma za matibabu kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na wale wanaotibiwa kwa misamaha na utaratibu wa Papo kwa Papo zitakuwa zimeimarika kwa kiwango kikubwa.
Mhe. Mkuu wa Mkoa na Wageni Waalikwa,  
Napenda kwa dhati kuwapongeza sana NHIF na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) kwa jitihada kubwa zilizowezesha kupatikana kwa kituo hiki. Kwa namna ya pekee, tunatambua mchango wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na jitihada wanazofanya katika kuboresha huduma za matibabu kupitia miradi mbalimbali na uwekezaji wenye udhamini wa Serikali. Kama Mfuko huu ungekuwa unafanya majukumu ya kukusanya michango na kuwalipa watoa huduma bila kushirikiana na Serikali kuboresha huduma za matibabu, hali ya upatikanaji wa huduma ingekuwa duni sana na leo hii tusingekuwa tunajivunia hatua hii tuliyofikia ya Mataifa mengine kuja kujifunza kutoka kwetu.
Nimefahamishwa kwamba, katika mpango wa NHIF unaolenga kuboresha huduma za matibabu, upo mkakati wa kujenga vituo vya matibabu vya mfano katika Kanda kwa awamu. Ninawahimiza kazi hii ifanyike haraka, bila urasimu, na kwa kuzingatia falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya HAPA KAZI TU ya uwazi, uadilifu na uwajibikaji wenye tija na matokeo. Ni imani yangu kuwa Mfuko wa NHIF utaharakisha ujenzi wa kituo kama hiki huko Mkoani Kigoma na katika Mikoa mingineyo hasa ile yenye uhitaji mkubwa. Na hili ni jambo linalowezekana hasa iwapo NHIF mtafanya kazi hii kwa uadilifu na kutanguliza mbele maslahi ya nchi.
Mhe. Mkuu wa Mkoa na Wageni Waalikwa,  
Wakati tunazindua kituo hiki, sisi sote ni mashuhuda kuwa kituo hiki ni kizuri na mandhari yake inavutia. Katika mazingira kama haya, hata mgonjwa akifika hapa anaanza kupata nafuu kabla hata ya kuanza kupata huduma za matibabu. Rai yangu kwa Uongozi ni kukifanya Kituo hiki kiendelee kuwa safi na kung’ara siku zote. Vivyo hivyo, nitoe wito kwa Jamii na wananchi kwa ujumla kuilinda miundo mbinu ya kituo hiki isiharibiwe. Na katika jukumu hili, nahimiza kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake ili tukitunze kiweze kudumu.
Mbali ya usafi, ni vyema suala la ukusanyaji mapato na udhibiti wake lizingatiwe na kupewa umuhimu mkubwa. Aidha, ni vema kituo hiki kianze na ukusanyaji mapato kwa njia za kielektroniki ili kuboresha makusanyo na kuzuia mianya ya kuvujisha mapato hayo. Aidha ninaagiza kwamba fedha zinazotokana na Mifuko ya uchangiaji ya NHIF, CHF na Papo kwa Papo zitumike kuboresha huduma katika kituo hiki, na hasa ununuzi wa dawa za ziada kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Asilimia 50 ya fedha hizi zitumike kununua dawa. Tutahakikisha dawa muhimu zote zinapatikana kutoka Bohari Kuu ya Dawa kwa bei nafuu na kwa wakati.
 Mhe. Mkuu wa Mkoa na Wageni Waalikwa,  
Kama nilivyosema awali, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa watanzania wote kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji wenye matokeo. Uboreshaji huu ni katika maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo uwepo wa wataalamu wa kutosha na wenye kuzingatia miiko na maadili ya taaluma zao, vifaa tiba, miundombinu na upatikanaji wa huduma za dawa. Tunachokishuhudia leo hii hapa Dodoma ni miongoni mwa mafanikio ya jitihada hizo za Serikali.
Mhe. Mkuu wa Mkoa na Wageni Waalikwa,  
Serikali imekuwa ikitenga fedha katika bajeti ya Afya kila mwaka kwa ajili ya kuwalipa watumishi, kununulia dawa, vifaa tiba na kulipia gharama za uendeshaji. Vyote hivi vinakuja katika vituo vya matibabu ili kuvijengea uwezo. Vilevile, vituo vinavyotoa huduma za afya, hasa vile vya Serikali, wanapata fedha za kununulia dawa kutoka Serikali kuu zinazopelekwa moja kwa moja Bohari kuu ya Dawa (MSD). Aidha, mbali ya fedha hizo zipo pia fedha zinazopatikana kutoka katika mifuko ya uchangiaji. Napenda kusisitiza kwamba ni lazima fedha hizi zitumike vizuri na kwa matumizi yaliyokusudiwa. Endapo hili halitatokea, Serikali haitosita kuchukua hatua stahiki mara moja.
Kwa hapa Mkoani Dodoma, nimetaarifiwa kuwa kuanzia mwezi Julai, 2015 hadi mwezi Machi, 2016 vituo vya matibabu vya Mkoa wa Dodoma vimepokea jumla ya shilingi 2,695,578,747.00 kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa huduma za matibabu walizotoa kwa wanufaika 166,578. Aidha, wakati fedha hizo zikiwa katika baadhi ya akaunti za vituo, dawa katika baadhi ya vituo zimeendelea kukosekana hali inayoleta malalamiko na usumbufu kwa wateja wa Mfuko na wananchi kwa ujumla. Ninawaagiza NHIF, MSD, Mganga Mkuu wa Mkoa na Timu yako mkutane ili kubaini ni nini chanzo cha tatizo hilo, na hatua zipi zichukuliwe kulitatua kwa haraka.
Mhe. Mkuu wa Mkoa na Wageni Waalikwa,    
Mwezi April, 2016 tulizindua “Kampeni ya Mzee Kwanza” mjini Morogoro, ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Mhe. Dokta John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kutoa kipaumbele cha huduma na kuwashirikisha wazee kwenye mambo muhimu kwa vitendo. Katika azma hiyo, Mheshimiwa Rais ameunda Idara maalumu ya kuhudumia wazee na kuiweka chini ya Wizara yangu. Nami napenda kurudia yale niliyoyasema Morogoro, kwamba ninawahakikishia wazee wangu wa Tanzania nzima kuwa sitawaangusha.
Kwa kushirikiana na Idara na Taasisi mbalimbali zinazohudumia wazee kwa namna moja au nyingine, tumeanza kutekeleza mikakati ya kutoa kipaumbele kwa wazee katika huduma zote za kijamii. Napenda kusisitiza agizo langu kwa kila Taasisi  ama Asasi inayotoa huduma yoyote, kutenga dawati maalum la kuhudumia wazee wanaokuja kupata huduma.
Ningependa pia kuwafahamisha kwamba Serikali iko mbioni kupeleka muswaada Bungeni unaohusu uimarishaji wa Huduma kwa Wazee.
Mhe. Mkuu wa Mkoa, Wageni Waalikwa,
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, napenda nichukue fursa hii kuagiza mambo muhimu yafuatayo:-
 1. Watoa huduma hakikisheni mnatoa huduma bora za afya kwa wanachama wa Mfuko wa NHIF, CHF na wananchi kwa ujumla katika kituo hiki na vituo vyote nchini. Ninachotaka kukiona ni wenye Bima wanapewa kipaumbele.
 2. Watoa huduma, hakikisheni mnawasilisha madai yenu kwa usahihi na bila kughushi kwenye Mfuko na kwa wakati; na NHIF ihakikishe inawalipa watoa huduma madai yao kwa wakati.
 3. Uongozi wa kituo hiki, hakikisheni mnakitunza kituo na vifaa vyake ili viweze kudumu muda mrefu na kunufaisha wananchi wengi.
 4. Uongozi wa NHIF na MSD, hakikisheni kazi za kufunga samani na vifaa kutoka MSD zinakamilika ndani ya mwezi huu na nipate taarifa ya utekelezaji wa kazi hii.
 5. Wekeni pia dawati/sehemu maalumu kuhudumia wazee katika kituo hiki ili wapate huduma kwanza. 
Hitimisho:
Mwisho, naomba nimalizie hotuba yangu kwa kuwashukuru sana nyote, na sasa niko tayari kufanya ile kazi ya kukifungua rasmi kituo hiki cha Bima ya Afya, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
                    Asanteni kwa kunisikiliza.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts