5/28/16

JOSE VAN GAAL: ROHO YA BABAYE SASA ITAPUMZIKA KWA AMANI


Ni sawasawa na baba anayekaribia kukata roho katikakati ya msitu mnene lakini moyo wake unamuuma na anamuomba Mungu asimchukue kwanza mpaka pale atakapomshuhudia kwa macho yake huyo atakayekuja kumchukua mwanae wa pekee na kumlea kwa niaba yake. Akifa kabla ya kushuhudia tukio hilo basi roho yake haitapumzika kwa amani na endapo Mungu akimjibu maombi yake hayo basi hufa kwa amani kwani anajua kuwa mwanae yupo kwenye mikono salama. Utanielewa tu…!!!
Baba na mwana
Gary Neville, mkongwe wa zamani wa Manchester United alishawahi kusikika akisema kuwa Jose Mourinho ni mafanikio makubwa ya Louis Van Gaal katika mpira wa miguu. Licha ya ukweli kwamba Van Gaal ameshawahi kutwaa mataji makubwa na ya heshima duniani, lakini Jose Mourinho ni taji lake kubwa ambalo miaka nenda rudi ataendelea kujivunia.
Miaka 19 iliyopita, Jose Mario dos Santos Mourinho Felix alikuwa kocha msaidizi wa Barcelona ya Louis Van Gaal licha ya kumtangulia msimu mmoja katika kikosi hicho kilichokuwa na wachezaji mahiri kama vile Luis Enrique, Luis Figo, Rivaldo na wengine wengi kwani Mourinho alitua rasmi Barcelona mwaka 1996 akiwa kama msaidizi wa Bobby Robson ambaye walitoka wote FC Porto.
baba na mwana5
Mourinho alitokea kupendwa na kuaminiwa sana na Van Gaal kama ilivyokuwa kipindi alipokuwa chini ya Bobby Robson. Licha ya kuwa kocha msaidizi, lakini Van Gaal alimchukulia Mourinho kama kocha mkuu mwenzake kwani alikuwa akimpa nafasi ya kukifundisha kikosi cha kwanza kwa kutumia mbinu zake mwenyewe na kubwa zaidi ni pale ambapo Van Gaal aliamua kuwa kocha msaidizi wa Mourinho katika mechi za kombe la Copa Catalunya ambalo Mourinho alilichukua mwaka 2000 akiwa kama kocha Mkuu na van Gaal akiwa kama kocha msaidizi. Hata katika ya kawaida baba hawezi kumuamini mwanae kiasi hicho hususani katika kibarua ambacho anajua akikipoteza tu, basi imekula kwake. Lakini Van Gaal alimuamini Mourinho zaidi ya mwanae.
International Friendly - FC Barcelona
Na kama hiyo haitoshi, Mwaka 2000, Benfica ilikuwa ikitafuta kocha baada ya kumtimua Jupp Heynckes na Mourinho alionekana kuitaka kazi hiyo na alipomuomba Van Gaal ushauri kuhusu kurudi Benfica kuwa kocha msaidizi, Van Gaal alimwambia “Hapana, usiende, waambie Benfica kama wanakutaka uwe Kocha Mkuu basi utaenda lakini kama wanataka uwe msaidizi basi utabaki hapa”,
Maneno hayo ya Van Gaal yanaonesha dhahiri kuwa alikuwa anamuandaa Mourinho kuja kuwa kocha Mkuu na sio msaidizi tena. Hivyo, Van Gaal alikuwa akimuandalia Mourinho maisha yake ya baadaye kama ambavyo kina baba hufanya kwa watoto wao na wala hakutaka kumtumia tu kwa manufaa yake yeye. Mourinho alitagazwa rasmi kuwa kocha wa Benfica mwaka huo licha ya kujiuzulu mechi tisa baadaye kufuatia kutoelewa na Rais mpya wa klabu hiyo. Bila shaka sasa utakuwa umeelewa ni kwa jinsi gani Mourinho na Van Gaal ni mtu na baba yake kwenye soka.
baba na mwana6
Sasa turudi kwenye mada yetu….
Masaa kadhaa yaliyopita, Jose Mourinho ameteuliwa kuwa kocha mpya wa Manchester United zikiwa ni siku chache tu tangu kutimuliwa kwa baba yake, Louis Van Gaal kwenye timu hiyo licha ya kuifunga Crystal Palace kwenye fainali ya kombe la FA wikiendi iliyopita.
jose
Hii inatokana na ukweli kwamba hali ya Van Gaal haikuwa nzuri klabuni hapo kufuatia kushindwa kutimiza ndoto za mashabiki wa Manchester United ambao walikuwa na matarajio makubwa kutoka kwake huku mbaya zaidi ni pale ambapo United haijafuzu kucheza mashindano ya UEFA baada ya kumaliza nafasi ya tano msimu huu wakiwa chini ya Van Gaal.
Uongozi wa United unaamini kuwa Mourinho ndiye mtu sahihi wa kuwarudisha kwenye ramani ya soka duniani tangu walipoondokewa na mzee wao, Sir Alex Ferguson mwaka 2013. Tangu hapo Manchester walishindwa kufurukuta kwani Fergie aliwaacha na kombe la ligi, na mpaka sasa hawajalibeba tena si chini ya David Moyes wala Van Gaal. Lakini kwa kumpa kibarua Mourinho ambaye ametwaa makombe 22 tangu mwaka 2003 ni ishara kwamba United wanataka kurudisha heshima yao barani Ulaya.
Naungana na Manchester United kuamini kuwa Mourinho atarejesha heshima iliyopotea Old Trafford ambayo hata baba yake, Louis Van Gaal ameshindwa kuirejesha kwani ukweli utabaki palepale kuwa Mourinho mwenye umri wa miaka 53 ni miongoni mwa makocha bora duniani kwa sasa licha ya kutimuliwa na Chelsea mwezi Desemba mwaka jana.
Licha ya ukweli kwamba Luois Van Gaal hajafurahia kutimuliwa kwake, lakini kwa upande mwingine kama alikuwa na mapenzi ya dhati na United, basi roho yake itakuwa imepumzika kwa amani kwasababu nyumba aliyoiacha imepata mrithi sahihi, mrithi ambaye anamuamini kuwa ataendeleza kazi aliyoianza yeye. Na kama kuna mtu anamuamini Jose Mourinho basi atakuwa si mwingine ila ni Van Gaal na nafikiri unaielewa furaha anayoipata mzazi baada ya kujua kuwa amepata mrithi sahihi wa kuitunza familia hata pale yeye atakaposhindwa kufanya hivyo.
baba na mwana3
Van Gaal alikuwa na mipango mingi na mizuri kwa United na bado alikuwa anaamini kuwa yeye ni mtu sahihi wa kuiletea mafanikio klabu hiyo. Sasa ametimuliwa na nafikiri roho yake ilibaki Old Trafford ili kushuhudia ni nani atakayerithi mikoba yake katika kuindeleza kazi nzuri aliyokuwa ameianza. Lakini baada ya kutangazwa kwa Mourinho, bila shaka roho yake itakuwa imefarijika kupita kiasi kuona kuwa aliyerithi mikoba yake ni mwanae aliyemlea na kumkuza yeye mwenyewe.
Hakuna raha kwa mzazi kama kuona mji wake umerithiwa na mtu sahihi anayemuamini na kumpenda kwa dhati. Mourinho na Van Gaal ni mfano halisi wa baba na mwana katika soka. Japokuwa kifo kinauma lakini machungu hupungua pale ambapo unajua kabisa kuwa uliyemuacha atakuwakilisha vyema maana kinachowalizaga wazazi wengi muda mfupi kabla ya kukata roho ni msongo wa mawazo juu ya nani atakayelea familia zao watakazoziacha.
baba na mwana4
Van Gaal sasa atapumzika kwa amani maana anayemrithi ndiye aliyemuandaa kwa miaka minne, miaka 19 iliyopita ili kuja kufanya kazi hii.
Tusubiri tuone kama Mourinho atakuwa ni mrithi sahihi wa Van Gaal Old Trafford.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts