5/4/16

Kawawa: Madiwani msiuze vyanzo

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Vita Kawawa amewataka madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, kutokubali kuuza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi ya vyanzo vya maji.

Alitoa mwito huo kwenye kikao cha wadau wa maji kilichofanyika jana mjini Kahama, kilicholenga kuangalia changamoto zinazokabili Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama na Shinyanga (Kashwasa).

Katika kikao hicho kilichohusisha madiwani na watendaji wa Kashwasa, Vita alisema wapo baadhi ya watu ambao wanataka kununua maeneo ya vyanzo vya maji mjini Kahama.

Alitaja mfano wa eneo la bwawa lililopo Kata ya Nyihogo kuwa ni muhimu, kwani limekuwa likisaidia maeneo muhimu ya mji hususani hospitali, magereza na polisi inapotokea tatizo la maji kukatika.

“Nawaomba madiwani wangu wa Halmashauri ya Mji wa Kahama msikubali kupitisha maombi ya kuuza maeneo yenye vyanzo vya maji kama Bwawa la Nyihogo,” alisema.

Aidha, alisema Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Kahama (KUWASA) imeongeza wateja wake kutoka 80 mwaka 2002 hadi 12,401 mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Kawasa alisema fedha zimeshatolewa kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi, waliokuwa wakiidai Kuwasa, waliopisha ujenzi wa tangi la maji.

Alisema serikali imetoa Sh milioni 478 na ziko kwenye akaunti ya mamlaka hiyo, ikisubiri utaratibu wa kuzigawa.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts