5/30/16

Maalim Seif: Dk Shein ataondoka bila vurugu


WAKATI Polisi wakiendelea kuwapiga mabomu ya machozi wanachama wa CUF, wanaokusanyika katika ziara za ndani za Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kiongozi huyo

Amesema Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ataondoka madarakani kwa presha ya wananchi.

Maalim Seif alitoa tamko hilo jana alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji kwenye Ofisi za CUF Bumbwini, Wilaya ya Kaskazini B, akiwa katika ziara ya siku tano katika mkoa wa Kaskazini Unguja.

Pamoja na msafara wake kuzuiwa kwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwa muda wa saa moja baada ya kufunga njia kwa kuweka kizuizi, alifanikiwa kufika katika Bumbwini na kufanya mkutano wa ndani na viongozi na watendaji wakuu wa wilaya wa chama hicho.

Alisema serikali ya Dk. Shein haitomaliza muda wake kutokana na presha ya wananchi ya kutomtambua yeye na viongozi wake pamoja na vikwazo vya wahisani vinavyoendelea kuchukuliwa kutokana na kufutwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.

“Tutaendelea kudai haki yetu kwa njia ya amani ndani na nje ya nchi mpaka Dk. Shein aondoke madarakani kwa presha ya wananchi bila ya kusukumwa au kupigwa kofi,” alisema huku akishangiliwa na watendaji na viongozi wa chama hicho.

Alisema kimsingi uchaguzi mkuu wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu, haukuwa halali kwa sababu ulifanyika kinyume cha Katiba na sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984.

Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu wa Zanzibar, alisema pamoja na misukosuko wanayoendelea kupata kutoka kwa Jeshi la Polisi, hawatarudi nyuma kudai haki yao waliyopewa na wananchi kupitia uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.

Aidha, alisema matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana yalifutwa kibabe, lakini uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki kulingana na ripoti za waangalizi wa ndani na nje, wakiwamo Umoja wa Ulaya (EU), Jumuiya ya Madola, Marekani na Uingereza.

Katika hatua nyingine, alisema wakati umefika kwa Jeshi la Polisi kutafakari vitendo wanavyofanya kama vina maslahi kwa nchi na wananchi wake au limeamua kuifanyia kazi CCM baada ya kukataliwa na wananchi.

Maalim Seif alisema kuna viongozi wanatumia vibaya vyombo vya dola Zanzibar, hasa Jeshi la Polisi kunyanyasa viongozi wa CUF na wanachama wake tangu kuvurugwa kwa maridhiano, hivyo kusababisha chuki za kisiasa kurudi Zanzibar.

Alisema wananchi wa Zanzibar wameichoka CCM na haiwezi kuendelea kubakia madarakani kwa sababu imeshindwa kujenga uchumi imara na kusababisha hali ngumu ya maisha kwa wananchi.

Akizungumzia historia ya maisha yake ya kisiasa, Maalim Seif alisema suala la kunyanyaswa na polisi si jipya kwa sababu amewahi kukamatwa na kuwekwa mahabusu pamoja na kuishi kizuizini kwa miezi 18 baada ya kufunguliwa kesi ya kukutwa na nyaraka za serikali mwaka 1989 kabla ya kuachiwa huru na Mahakama ya Rufani Tanzania.

Awali, saa nne asubuhi jana, msafara wa Maalim Seif ulipata msukosuko baada ya kufika Kona ya Bumbwini Michungwa Miwili na kukuta polisi wamefunga njia kwa kuweka kizuizi huku askari wa FFU wakiwa na mabomu ya machozi na silaha za moto.

Askari Polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Aziza Ramadhan Toufiq, walisema hawataki kufanyika mikutano hiyo.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts