5/18/16

Mabasi ya Dart yatoa ajira kibao

  Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam, (Dart) umewaita kwenye usaili waombaji zaidi ya 800, kwa nafasi za watakaopokea malalamiko ya wasafiri na wakata tiketi kwenye vituo vyao mbalimbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Ofisa Uhusiano wa Dart, William Gatambi alisema waombaji zaidi ya 800 wameitwa kwenye usaili katika vitengo mbalimbali, zikiwamo za kupokea malalamiko ya wasafiri na wakata tiketi.
Gatambi alisema watakaofanikiwa kupita kwenye usaili huo, wataungana na watendaji waliopo tayari kwenye mradi ili kuboresha huduma hiyo ya usafiri.
“Zimetolewa nafasi mbalimbali lengo ni kuboresha huduma ndiyo maana utaona kuna watu wenye sifa wameitwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kukusanya nauli na wapo pia watakaoshughulikia malalamiko ya wateja,” alisema.
Kuhusiana na changamoto ambazo zimeanza kulalamikiwa siku mbili baada ya kuanza kwa utaratibu wa kulipa nauli, Gatambi alisema hali hiyo inatokana na ugeni katika huduma hiyo, lakini kila kitu kitakwenda sawa watakapopatikana watoa huduma wenye sifa. “Tunaamini hizi ni changamoto za ugeni wa huduma, ila mambo yatakwenda sawa kadiri siku zinavyokwenda na hawa waajiriwa wapya watazidi kuleta maboresho,” alisema.
Tangu kuanza rasmi kwa mradi huo Jumatatu kumekuwapo na malalamiko kadhaa, ikiwamo mfumo wa ukatishaji tiketi na kukosekana kwa utaratibu maalumu wa kuwaongoza abiria kuingia kwenye mabasi, hivyo kusababisha msongamano.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts