Magari ya Serikali kulipa Daraja la Nyerere Isipokuwa ya Magereza, Polisi na JWTZ | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

5/11/16

Magari ya Serikali kulipa Daraja la Nyerere Isipokuwa ya Magereza, Polisi na JWTZ

 
Serikali imetangaza viwango vya tozo kwa watumiaji wa Daraja la Nyerere (Kigamboni) na utekelezaji wa tozo hizo utaanza Jumamosi, huku kiwango cha juu zaidi kikiwa ni Sh75,000 kwa malori makubwa yanayobeba magari ya ujenzi.
Katika tozo hizo ambazo hazitawahusu waenda kwa miguu, baiskeli zitatakiwa kulipa Sh300 baadaye itakapotangazwa, lakini kwa sasa watapita bure.
Akitangaza viwango hivyo vya tozo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia sekta ya ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga alisema viwango hivyo walihusisha wadau mbalimbali na kufikia uamuzi huo.
Baadhi ya viwango vya tozo kwa vyombo vitakavyopita katika daraja hilo ni pikipiki zitakazotozwa Sh600, mkokoteni Sh1,500, pikipiki ya magurudumu matatu (bajaj) Sh1,500, gari dogo (saloon) Sh1,500, pick-up ya tani mbili Sh2,000 na shangingi Sh2,000.
“Magari yote ya Serikali yatatakiwa kulipia daraja hili. Ninashauri taasisi za Serikali kutenga fedha kwa ajili hiyo. Magari yote yenye namba za jeshi (JWTZ, Polisi na Magereza) yatapita bure,” alisema.
Nyamhanga alibainisha kuwa mabasi madogo ya kuchukua mpaka abiria 15 yatalipia Sh3,000, mabasi yanayobeba abiria 15 hadi 29 yatalipia Sh5,000, mabasi yanayobeba zaidi ya abiria 29 italipiwa Sh7,000, gari bila tela lake, Sh7,000 na trekta na tela lake Sh10,000.
Magari yenye uzito wa zaidi ya tani mbili mpaka saba yatalipia Sh7,000, uzito wa zaidi ya tani saba mpaka 15 (Sh10,000), uzito wa zaidi ya tani 15 mpaka 20 (Sh15,000), uzito wa zaidi ya tani 20 mpaka 30 (Sh20,000) na lori la semi-trailer Sh25,000.
Alisema, lori na tela lake litalipiwa Sh30,000, magari ya ujenzi Sh40,000 na magari makubwa yanayobeba magari ya ujenzi Sh75,000.
“Magari yote yenye uzito mpaka tani 56 yatapita katika daraja hilo. Kwa yale yenye uzito zaidi huo yatapita kwa kibali maalumu kutoka kwa Wakala wa Barabara (Tanroads),” alisema katibu mkuu huyo.
Nyamhanga aliongeza kuwa, Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) litatoza malipo hayo kwa muda wa miaka 30, ili kufidia gharama za ujenzi wa daraja hilo. Alisema muda unaweza kupungua endapo fedha zinazotakiwa (zaidi ya Sh250 bilioni) zitapatikana mapema.
Mkurugenzi wa Uwekezaji, Yacoub Kidula alisema daraja hilo limejengwa kwa fedha za wanachama wa NSSF, kwa hiyo fedha hizo zinatakiwa zirudi kwa wenyewe.
“Malipo hayo ni kila chombo kinapopita kwenye daraja hilo. Tukianza kutumia mfumo wa kielektroniki tutatoa unafuu kwa watumiaji wa kadi maalumu ambao watakuwa wamelipia kwa miezi sita au mwaka,” alisema Kidula.
Wakati huohuo, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alitembelea daraja hilo na kutoa wito kwa viongozi wa Serikali ya mkoa wa Dar es Salaam kubuni mbinu za kumaliza msongamano wa magari katika jiji hili. Kikwete alipendekeza kujengwa kwa treni ya kisasa ambayo inachukua watu wengi kwa wakati mmoja.
Alisema usafiri huo utasaidia kupunguza magari barabara na kufanya watumiaji wa magari kuwa wachache.
“Nilipokwenda India nilifanya mazungumzo na waziri mkuu wao kuhusu mradi wa ujenzi wa treni ya kisasa akaonyesha nia. Ni jambo la kufuatilia. Tatizo viongozi wetu watakwenda, watarudi, watajadili bila kufanya uamuzi,” alisema Kikwete.
Kiongozi huyo wa Serikali ya awamu ya nne, aliwataka viongozi kuwekeza kwenye ujenzi wa miji maeneo mengine. Alisema wakati wa utawala wake walianzisha miradi ya Kigamboni, Luguruni na Mabwepande. “Eneo la Mabwepande, nalo mnatakiwa kulisimamia vizuri, mkichelewa itakuwa kama maeneo mengine ya uswahili, ” alisema Kikwete.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema daraja hilo litasaidia kupunguza foleni kwa wakazi wa jiji hilo. Alisema bado anatambua kwamba zinahitajika jitihada za kumaliza tatizo la Dar es Salaam ili iwe historia.

google+

linkedin