5/14/16

Magufuli abaini madudu Uwanja wa Ndege Dar

 
Rais John Magufuli, jana alifanya ziara ya kushtukiza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kubaini mashine za ukaguzi hazifanyi kazi kwa muda mrefu huku maofisa wa uwanja huo wakimdanganya kuwa ni nzima.
Akionekana kukasirishwa na namna maofisa wa uwanja huo walivyotaka kuficha ukweli, Rais Magufuli, ambaye alikuwa akitokea jijini Kampala, Uganda kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Yoweri Museveni, alisema kutokana na ubovu huo wa mashine, watu wanaweza kupitisha dawa za kulevya, meno ya tembo, dhahabu na almasi bila kugundulika.
Rais aliiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja dhidi ya dosari za ukaguzi zilizopo katika kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika uwanja huo.
Mara baada ya kutua na ndege katika uwanja huo, Rais alikwenda katika kitengo hicho na kuonana na maofisa wa uwanja huo ambao walianza kumpa maelezo kuhusu ukaguzi.
Maofisa hao walikuwa wakitoa kauli zinazotofautiana kuhusu utendaji kazi wa mashine hizo hali iliyosababisha Rais kuiagiza wizara na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja.
“Unajua mimi sipendi kudanganywa, ni vizuri uzungumze ukweli tu. Kwanini nimeanzia hapa huwezi kujiuliza?” alihoji.
“Sipendi kudanganywa, ukinidanganya nitachukia sasa hivi. Wewe umenidanganya kwamba hiyo ndiyo mbovu na hii ndiyo nzima, nikakwambia muiwashe hiyo nzima, akaja huyu mwenzako amezungumza ukweli kabisa, akasema hii (mashine) ni mbovu kwa miezi miwili,” aliwabana maofisa hao alipotaka watoe maelezo kama wanakagua mizigo inayopita.
“Nikiamua kuja na dawa zangu za kulevya, nikaja na dhahabu zangu na almasi na meno ya tembo kwa kutumia hizi ndege ndogondogo napita tu.”
Bomba la mafuta
Alipokuwa nchini Uganda, Dk Magufuli alifanya mazungumzo na Rais Museveni kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima, Uganda hadi bandari ya Tanga ambapo alishauri kufupisha muda wa ujenzi wa mradi huo kwa kutumia mbinu inayojumuisha usanifu na ujenzi na kutumia makandarasi wengi watakaogawanywa katika vipande tofauti badala ya kutumia mkandarasi mmoja.
“Nashauri tutumie mbinu ya usanifu na ujenzi wa pamoja, hii ni njia ya haraka zaidi na pia tugawe vipande vya ujenzi kwa njia yote ya bomba la mafuta yenye urefu wa kilomita 1,410. Tunaweza kuwa na makandarasi watano mpaka sita ambao watatumia njia hiyo mpya ya usanifu na ujenzi,” alisema.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts