5/9/16

Magufuli: Utumbuaji Majipu Sio Ukatili
Rais John Magufuli amewataka Watanzania wasimuone katili kwa kuwafukuza kazi baadhi ya watendaji wa Serikali, kwakuwa anataka kuirejesha nchi kwenye mstari.


Akizungumza katika misa ya Jumapili kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Tokeo la Bwana Burka jijini Arusha, Rais Magufuli alisema watu katili ni wale ambao walikuwa wanawaibia Watanzania na kuwanyonya wanyonge.


Dk Magufuli alisema analazimika kuchukua hatua ya kuwafukuza kazi si kwamba ni katili, bali lengo ni kuwatumikia Watanzania na kuirejesha nchi kwenye mstari.


Alisema Tanzania ni taifa tajiri, hakuna sababu ya wananchi kulalamika kila kona, kwani kuna ardhi ya kutosha, madini ya kila aina, wanyama wa aina mbalimbali ambao baadhi wameanza hadi kupelekwa nje.


“Ninapochukua hatua nataka kuweka Tanzania iliyonyooka, mimi tayari nimesema nimejitoa sadaka kwa Watanzania hasa wanyonge,” alisema.


Aliongeza kuwa hatawaangusha Watanzania na hatabadilika, ataendelea kusimama na kutetea haki za Watanzania maskini na siku zote atatembea na maskini.


Masilahi ya vyama


Akizungumzia masuala ya kisiasa, alisema uchaguzi umekwisha kama kuna watu walikuwa Chadema, CCM, NRA au chama cha CUF lengo ni moja kuhakikisha wanashirikiana kuleta maendeleo ya Watanzania.


“Tupeleke masilahi ya Watanzania mbele kuliko ya vyama vyetu, kwani hata kama vyama visingekuwapo taifa lingekuwapo,” alisema.


Alirudia wito wake wa kuwataka Watanzania kuendelea kumuombea na kuliombea taifa, kwani kuongoza taifa maskini kunahitaji mkono wa Mungu.


Paroko wa kanisa hilo, Peter Pinto akizungumza kwa niaba ya Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya kwa Watanzania.


Alisema Watanzania walio wengi wanamuunga mkono hasa katika kauli mbiu yake ya “Hapa kazi tu”, kwani hata maneno ya Mungu yanasisitiza watu kufanya kazi kwa bidii.


Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Philemon Mushi akitoa salamu za waumini alieleza kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli hasa katika utumbuaji wa majipu.


Alisema hata katika vitabu vya Mungu mafisadi walitoswa baharini, hivyo kazi ambayo anafanya Rais Magufuli ni kazi ya Mungu, kuhakikisha anarejesha nidhamu na uwajibikaji kwa manufaa ya Watanzania wote.


Katika misa hiyo, Rais Magufuli alikabidhiwa zawadi ya Biblia, shuka na rozali, naye alitoa zawadi ya Sh1 milioni kwa kwaya ya kanisa hilo na kukubali kuwa mwanaparokia hiyo.


Rais Magufuli yupo mkoani hapa katika ziara ya kikazi, na leo anatarajiwa kuzindua miradi ya majengo ya mashirika ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF.


Wakizungumzia kauli ya Rais Magufuli kwamba yeye si katili, Dk James Jesse Mhadhiri katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema tatizo siyo kuonekana katili au la, kikubwa kinapaswa kuonekana kama maamuzi hata kama ni sahihi je, yamefuata misingi ya sheria.


Dk Jesse alisema kitendo cha watumishi wa umma kusimamishwa kazi hadharani, ni sawa na kuwatia hatiani kwani ambao wanapaswa kufikia maamuzi wataogopa kufikia maamuzi sahihi kwa kuogopa shinikizo la Rais.


Alisema ni vyema watumishi wa umma ambao wanatuhuma mbalimbali, zifuatwe taratibu za utumishi wa umma katika kuwawajibisha na siyo kuondolewa hadharani.


John Bayo ambaye ni mratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Arusha (Angonet) alisema kwa taifa lilipofikia, Rais Magufuli hafanyi ukatili kwa kuwasimamisha kazi watumishi wa umma.


Alisema kuna makosa ya wazi ambayo yameligharimu taifa, ambayo yamefanywa na watumishi kiasi kwamba hata kuwasimamisha kazi tu hadharani hakutoshi.


“Kwa mfano, suala kama la sukari, watu wanaficha sukari ili wengine wakose watu wanafuja mali za umma lazima hatua kali zichukuliwe,” alisema.


Hassan Hashi Ahmed, mfanyabiashara wa Karatu, alisema Rais Magufuli hafanyi ukatili wowote, wananchi wanamuunga mkono asilimia 100, kwani anatetea wanyonge.


Ahmedi alisema Tanzania ilikuwa imefikia mahala pabaya, hivyo lazima sasa hatua kali zichukuliwe na anampongeza Rais kwa kazi nzuri.


Joram Laizer mkazi wa Arumeru, alisema Rais anafikia maamuzi ya kuwafukuza watu kazi kutokana na kubaini dosari, lakini anajikuta baadhi wanamlaumu kutokana na kukosekana uwajibikaji katika ngazi nyingine za Serikali.


Laizer alisema Rais anapochukua hatua za kusimamisha kazi siyo kama ni katili, bali kuna watendaji wengi wenye nafasi za maamuzi ya kufukuza kazi na kuwajibisha wameshindwa kutimiza mamlaka yao, ama wanahusika na ubadhilifu au hawajui wajibu wao.


Alisema umefika wakati Rais akibaini ubadhirifu, akimsimamisha kazi mtendaji wa ngazi ya chini, basi walio juu yake ambao walikuwa wanamlinda nao waondolewe.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts