5/24/16

Majuto ya Kitwanga yawatwanga wengi


KITENDO cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kutimuliwa na Rais John Magufuli kwa makosa ya kuingia bungeni akiwa amelewa Ijumaa iliyopita, kilisababisha fadhaa si katika familia yake tu, bali pia kwa wabunge wenzake.
Taarifa zinasema mkewe Kitwanga alilazimika kusafiri usiku baada ya taarifa ya kutimuliwa mumewe kutolewa na Ikulu, Ijumaa iliyopita, huku wabunge wenzake, hasa wale wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, wakipanga mikakati ya kumfariji.

Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Richard Ndassa, alisema aliamua kuunda timu ya wabunge ili kutoa ushauri nasaha na kumfariji Kitwanga, baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wake.

Taarifa ya kutimuliwa kwa Kitwanga, ilitolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ikieleza kuwa Rais Magufuli alichukua uamuzi huo kutokana na Waziri Kitwanga kuingia bungeni na kujibu maswali yaliyoelekezwa kwenye wizara yake (Mambo ya Ndani ya Nchi) akiwa amelewa.

Ndassa, ambaye pia ni Mbunge wa Sumve (CCM), alisema kutokana na ukubwa wa tukio hilo, aliona kuna haja ya kutoa ushauri kwa Mbunge mwenzao wa mkoa wa Mwanza ili "asije akachukua uamuzi mbaya."

Aliongeza kuwa baada ya uamuzi wa Rais, yeye na wabunge wengine wanne wa CCM, akiwamo Mwenyekiti wa Bunge na Mbunge wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge, waliamua kufika nyumbani kwa Kitwanga, ambaye ni Mbunge wa Misungwi mkoani Mwanza kwa nia ya kumfariji.

Aliwataja wabunge wengine wa CCM waliofuatana nao kwenda nyumbani kwa Kitwanga, Area D mjini hapa, Jumamosi iliyopita kuwa ni William Ngeleja (Sengerema), Kiswaga Desdery (Magu) na Dk. Charles Tizeba (Buchosa).

"Baada ya tukio (la kutenguliwa kwa uteuzi) kutokea, tulienda mimi, Chenge, Kiswaga, Ngeleja na Tizeba nyumbani kwa Kitwanga pale Area D. Tulienda baada ya kikao cha Jumamosi cha Bunge," alisema Ndassa.

Aliongeza kuwa: "Tulimkuta mke wake amekuja kutoka Dar es Salaam, akasema amelala, amepumzika (Kitwanga), kwa hiyo tukaamua kuondoka, tukawaacha. Yule mama (mke wake Kitwanga) ali'drive' (aliendesha) gari usiku kucha baada ya tukio hilo kutokea. Alifika hapa (Dodoma) saa tatu asubuhi."

Alisema kuwa yeye na wenzake tangu Ijumaa wamekuwa wakimpigia simu Kitwanga na kumfariji.

"Baadaye jioni (Jumamosi) tukapiga simu tena. Alikuwa anaendelea vizuri na alikuwa anakula chakula. Hata jana (juzi) nilizungumza naye anaendelea vizuri. Kwa kweli alikuwa na mawazo mengi, lakini sasa ametulia," alisema Ndassa.

Aliongeza kuwa: "Leo (jana) saa 1:56 asubuhi nimezungumza naye wakati wanaanza safari ya kwenda Dar es Salaam. Haya yote yaliyotokea ni ya kawaida, ingawa ilikuwa haijawahi kutokea Tanzania Waziri kufukuzwa kazi kutokana na ulevi.

"Mwalimu (Julius Nyerere) alikuwa anawahamisha tu kimajukumu. Nakumbuka mmoja wa alikuwa Profesa (John) Machunda (Mbunge wa zamani wa Ukerewe), huyu alikuwa na tabia za kunywa kupita kiasi. Kwa hili la Mheshimiwa Kitwanga, isingekuwa rahisi kwa Rais kusema amhamishie sehemu nyingine."

Ndassa alikaririwa na Nipashe juzi akisema alijaribu kumzuia Kitwanga kuingia ndani ya bungeni mara tatu na kumshauri kuondoka kwenye viwanja vya Bunge hilo lakini ilishindikana.

Ndassa alisema Kitwanga alionekana amelewa tangu asubuhi (Ijumaa) na wakati anaingia bungeni alimuuliza kwa lugha ya Kisukuma `Ole sawa ielelo?’ akimaanisha ’uko sawa leo’.

Mbunge huyo alisema alimuuliza Kitwanga swali hilo baada ya kumwona hayuko sawa na alikuwa na harufu ya pombe mdomoni lakini akamjibu: `Nale sawa gete’, akimaanisha yuko sawa kabisa.

Alisema baada ya kipindi cha Bunge kumalizika asubuhi siku hiyo aliyotimuliwa, alikutana na Kitwanga nje ya viunga vya Bunge na alijaribu kumshika mkono ili kumwondoa na eneo la Bunge, lakini alimkimbia.

Alisema aliamua kumfuata dereva wa Kitwanga na kumwambia amchukue na kumuondoa kwenye viwanja hivyo vya bunge, lakini Kitwanga hakuwa tayari kuingia ndani ya gari.

“Unajua mimi ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM Mkoa wa Mwanza, hivyo nilijitahidi sana kumzuia, lakini nilishindwa na wakati akiwa getini ndipo alipoitwa na Waziri Mkuu ofisini na jioni mkasikia taarifa ya Rais Magufuli,” alisema Ndassa.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts