5/15/16

Maoni ya Wadau: Takukuru Msiishie Temeke Mulikeni Manispaa Zote Nchi Nzima

HIVI karibuni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Temeke, ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ya utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kwa mwaka huu.

Katika taarifa hiyo, Takukuru iliainisha kuwa ofisi yao ilipokea malalamiko 52 kutoka kwa wananchi, yakiwemo ya vitendo vya rushwa. Ilibainisha kuwa malalamiko hayo yalipokelewa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na wananchi kufika katika ofisi hizo za Takukuru, kupitia vyombo vya habari, taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na taarifa za kiintelijensia kupitia kwa maofisa wa Takukuru na watu wengine.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Temeke, Pilly Mwakasege alisema taarifa hizo zilifanyiwa kazi kwa kufungua majalada ya uchunguzi 24, ambayo kati ya hayo majalada nane yanaendelea na uchunguzi wa kina na 16 yanaendelea na uchunguzi wa awali ili kubaini makosa ya rushwa na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, pale makosa ya rushwa yatakapothibitika.

Pia Mwakasege alisema kati ya malalamiko 52 yaliyopokelewa na taasisi yake kwa kipindi hicho, eneo lililoongoza kwa kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa ni Halmashauri ya Manispaa ya Temeke.

Anasema katika Manispaa ya Temeke kulikuwa na malalamiko 17 yaliyofikishwa katika taasisi yake. Baada ya manispaa hiyo, waliofuatia ni sekta binafsi, ambapoTakukuru ilipokea malalamiko 10.

Baada ya sekta binafsi ilifuatia Jeshi la Polisi, kitengo cha Usalama Barabarani (trafiki) ambapo kulikuwa na malalamiko nane. Idara nyingine ni Mahakama ambapo malalamiko sita yalipokelewa na yote yanaendelea kufanyiwa uchunguzi.

Taarifa hii iliyotolewa na Takukuru inabidi kufanyiwa kazi kwa haraka ili haki iweze kutendeka. Pia malalamiko 17 yaliyotolewa ndani ya Manispaa ya Temeke kwa kipindi kifupi cha miezi mitatu ni ishara kuwa hali si shwari katika manispaa hiyo.

Ni ukweli usiopingika kuwa manispaa inabeba jukumu zito la kuhudumia wananchi katika nyanja mbalimbali. Hivyo hatua ya wananchi kutoa malalamiko dhidi ya manispaa hiyo ni jambo la kuvunja moyo na kukatisha tamaa, kuwa hakuna mtetezi wao katika eneo hilo.

Suala hilo lililoelezwa na mkuu huyo wa Takukuru, si la kupuuza hata kidogo, kwani hali hiyo ikiachiwa iendelee hivyo italeta shida kubwa kwa wananchi. Ni vyema wahusika wakashughulikia jambo hilo kwa makini na haraka ili haki iendelee kutendeka kwa wananchi.

Wananchi wanatakiwa wafurahie huduma zinazotolewa na manispaa hiyo, badala ya kuzichukia. Nawapongeza Takukuru Temeke kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuchunguza watendaji wabovu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo manispaa hiyo ya Temeke.

Pia nawashauri wananchi waendelee kuwafichua wale wote wanaofanya vitendo vilivyo kinyume na maadili ya kazi zao, kwani kuwafichua kutarahisisha kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola.

Manispaa hiyo imulikwe zaidi ili kuwabaini watumishi wote wasio waaminifu, ambao hawajafikiwa na mkono wa sheria. Umulikwaji huo usiishie katika manispaa ya Temeke tu, bali uendelee katika manispaa zote jijini Dar es Salaam, na nchi nzima. Naamini kwa kufanya hivi, itakuwa fundisho kwa wengine wanaotumia vyeo au madaraka waliyonayo kuwanyanyasa wananchi, badala ya kuwasaidia.

Shime viongozi na wananchi tuungane na Rais John Magufuli katika jitihada zake za kutumbua majipu ili kila mmoja afurahie pale alipo, badala ya watu wachache. Wote tumejionea ama kushuhudia matunda ya utumbuaji wa majipu unaoendelea, kwa wote wasio waadilifu katika nafasi walizopewa za kuwatumikia wananchi.

Kwa kufanya hivyo, Tanzania itakuwa ni nchi ya kukimbiliwa na wengi, badala ya kuwa nchi ya matatizo. Hakuna kinachoshindikana. Tukiamua kuwa kitu kimoja kwa umoja wetu, tutashinda na kutokomeza rushwa na ufisadi.
 
Chanzo: Habari Leo
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts