Mawaziri 6 Wamkwepa Waziri Aliyetumbuliwa | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

5/22/16

Mawaziri 6 Wamkwepa Waziri Aliyetumbuliwa


SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga baada ya kuingia bungeni akiwa amelewa, mawaziri wenzake kadhaa wameamua kujiweka mbali na suala hilo.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga.

Juzi usiku, Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilitoa taarifa kuwa Rais Magufuli amechukua uamuzi wa kutengua nafasi ya Kitwanga kutoka na kile kilichoelezwa kuwa ni hatua yake ya kuingia bungeni na kujibu maswali yaliyoelekezwa kwenye wizara yake (Mambo ya Ndani ya Nchi) huku akiwa amelewa.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli ulipokewa kwa hisia tofauti, huku wengi wakiupongeza kwa maelezo kuwa unadhihirisha kwa vitendo ni kwa namna gani serikali ya wamu ya tano isivyokuwa tayari kuvumilia ukiukwaji wa miiko ya uongozi.

Hata hivyo, walipotafutwa na Nipashe na kutakiwa watoe maoni yao kuhusiana na uamuzi wa Rais wa kumuondoa Kitwanga, mawaziri sita walikwepa kueleza chochote na kutaka suala hilo aulizwe Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Baadhi ya mawaziri waliokwepa kumzungumzia Kitwanga jana ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Aidha, kama ilivyokuwa kwa mawaziri hao, naibu mawaziri kadhaa waliozungumza na Nipashe pia walijiweka kando na suala hilo la kufutwa kazi kwa Kitwanga, wakiwamo

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula.

Alipofuatwa na mwandishi kwenye viunga vya Bunge, Mwakyembe alisema kwa kifupi: "Siwezi kuzungumzia suala hilo."

Lukuvi alipoulizwa, pia alijibu kwa kifupi, akisema kuwa yeye hawezi kueleza chochote kuhusu suala hilo bali aulizwe Waziri Mkuu Majaliwa.

"Mimi najiandaa kusoma bajeti ya Wizara yangu, siwezi kuzungumzia suala hilo…tafadhali mtafute PM (Waziri Mkuu)."

Nchemba alisema: "Siwezi kulizungumzia suala hilo" na Simbachawene akajibu kwa kifupi zaidi: "No comment (sina cha kuzungumza)."

Aidha, Waziri Mwijage alisema: "Siwezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa, nawahi, nina safari ya kuelekea Dar es Salaam mchana huu."

Naibu Waziri Angelina alisema: "Siwezi kuzungumza chochote kuhusu suala hilo."
Hata Mpina alipoulizwa, naye hakuwa tayari bali alisema: "Ooh, hapana, siwezi kusema chochote kuhusu tukio hilo wala uamuzi uliofanywa."

Alipoulizwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kingwallah, alisema pia kwa kifupi:"ni ajali ya kisiasa."

UONGOZI WA BUNGE
Akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na kufutwa kazi kwa Waziri Kitwanga, Naibu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema hakuna kifungu chochote cha Kanuni za Bunge kinachozuia mtu kuingia bungeni akiwa amelewa.

“Kanuni zinahusiana na uendeshaji wa shughuli za Bunge, hizi za maadili ni Kanuni za Maadili ambazo zinatakiwa kutungwa ili kudhibiti hali hiyo," alisema Joel.

ALIZUIWA KUINGIA BUNGENI
Katika hatua nyingine, imedaiwa kuwa muda mfupi kabla ya kuingia bungeni juzi asubuhi katika siku anayodaiwa kuingia bungeni akiwa amelewa, Kitwanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi alizuiwa (kuingia) mara tatu na mbunge mwenzake kutoka Mwanza, Richard Ndassa wa Jimbo la Sumve (CCM) lakini hakutaka kusikia ushauri huo.

Akizungumza na Nipashe jana, Ndasa alisema alijaribu kadri alivyoweza kumzuia (Kitwanga) asiingie bungeni na badala yake kuondoka kabisa eneo hilo lakini ilishindikana.

Alisema yeye (Ndasa) alimuona Kitwanga ana kila dalili kuwa amelewa na ndiyo maana alijaribu kumsihi asiingie bungeni, lakini hakuwa tayari baada ya kusisitiza kuwa “yuko sawa kabisa”

Akielezea zaidi, Ndasa alisema alimuuliza Kitwanga kwa lugha ya Kisukuma; “Ole sawa ielelo?" akimaanisha “uko sawa leo”, naye akamjibu pia kwa lugha ya Kisukuma: “Nale sawa gete” akimaanisha yuko sawa kabisa.

“Unajua Kitwanga nakaa naye kiti cha jirani, sasa wakati anaingia asubuhi nikamuona hayuko sawa. Nikamuuliza na alinijibu kwa kifupi, kisha akaenda mbele kukaa tayari kwa kujibu maswali,” alisema Ndassa.

Ndasa alisema hata baada ya kipindi cha Bunge kumalizika asubuhi, alikutana na Kitwanga nje ya viunga vya Bunge na kujaribu kumshika mkono ili kumuondoa na eneo la Bunge, lakini alimkimbia.

Ndassa alisema aliamua kumfuata dereva wa Kitwanga na kumwambia amchukue na kumuondoa kwenye viwanja hivyo vya bunge, lakini Kitwanga hakuwa tayari kuingia ndani ya gari.

“Unajua mimi ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM mkoa wa Mwanza, hivyo nilijitahidi sana kumzuia jana (juzi) lakini nilishindwa… na wakati akiwa getini ndipo alipoitwa na Waziri Mkuu ofisini na jioni mkasikia taarifa ya Rais Magufuli,” alisema Ndassa.

Mbunge wa Manonga (CCM), Seif Gulamali, alisema anaunga mkono uamuzi wa Rais Magufuli kwa kuwa kitendo cha mtu yeyote kunywa pombe asubuhi ni kukiuka sheria.

"Mimi sijathibitisha kama kweli Kitwanga alikuwa amelewa. Lakini kwa sababu taarifa ya vyombo vya nchi imesema kwamba alikuwa amelewa, si jambo zuri," Gulamali alisema.

Naye Mbunge wa Nkasi (CCM), Ali Keissy, alisema sheria iko wazi kwa mtumishi yoyote wa serikali kuingia kazini akiwa amelewa ni kosa.

Keissy alisema Kitwanga alionekana kuwa na dalili za kulewa hata kabla ya kuingia kwenye Ukumbi wa Bunge.

Mbunge wa Rombo (CCM), Joseph Selasini, alisema Kitwanga alikuwa anajibu maswali tofauti na siku zote na hivyo anaunga mkono uamuzi wa Rais Mgufuli kumfuta kazi ya uwaziri.

“Rais angemwacha Kitwanga, maana yake ingekuwa Rais anaunga mkono vitendo kama vile, hivyo imeonyesha Rais anataka viongozi wenye nidhamu na maadili.

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alisema mambo hayo yote yanatokea kwa sababu ya mfumo mbovu wa utawala kwa sababu viongozi hawapigiwi kura na wananchi bali wanateuliwa na Rais bila ya kuidhinishwa na mamlaka yoyote.

Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bungara 'Bwege', alisema anaunga mkono uamuzi wa Rais Magufuli kumuondoa Kitwanga, huku akidai uamuzi huo ulichelewa.

"Mimi naunga mkono uamuzi uliochukuliwa ingawa sijui wametumia kipimo gani kumpima. Kama kweli alikuwa amelewa, ni kinyume cha sheria," alisema.

Aliongeza: "Hata hivyo, Kitwanga alipaswa kusimamishwa kazi mapema hata kabla ya tukio hili la kuelewa. Rais alipaswa kumsimamisha mara tu baada ya kuhusishwa na mkataba tata wa kampuni ya Lugumi na Jeshi la Polisi."
Wakati

Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare, alisema alimpongeza Rais Magufuli kwa kuchukua uamuzi huo haraka, huku akibainisha kuwa bado kuna mawaziri wengine nane ambao anaamini wataungana na Kitwanga kwa kuwa wameonyesha dalili zote kuwa ni 'mizigo'.

"Kitwanga ni sehemu ya matatizo ya serikali nzima ya CCM. Hivyo ndivyo walivyolelewa. Huyu ni mmoja tu, tutaendelea kuwaona wakiwajibishwa kwa sababu Rais ana mtazamo wake, si wa taasisi," alisema.

"Hizi ndizo tabia zao, na alipowanyima semina elekezi aliharibu zaidi. Na bado kuna mawaziri wengine nane hivi wataondoka madarakani kwa utaratibu huu huu,” alisema Lwakatare ambaye aliongeza kuwa alisoma na Kitwanga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) miaka ya 1986-1988 na kwamba kadri amjuavyo, wakati huo hakuwa mnywaji wa kiwango cha kuingia kazini akiwa amelewa.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendp), Zitto Kabwe, aliandika pia kwenye ukurasa wake wa Facebook akipongeza uamuzi huo.

Zitto alisema: "Uamuzi wa Rais kumfukuza kazi Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, unatuma ujumbe mmoja - hataki mchezo. Rais amethibitisha kuwa anao uwezo wa kutumbua hata aliowateua. Ni maamuzi muhimu sana kwa kiongozi wa aina yake.”

WASOMI, WANAHARAKATI
Akizungumzia kuondolewa kwa Waziri Kitwanga, Mhadhiri Mwandamizi katika Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, alisema Spika alitakiwa kumtoa bungeni mapema kwa sababu alishaonekana kuwa amelewa.

“Tatizo la Bunge letu kutoka limeanza limegeuka idara ya Serikali halina meno tena linafanya kazi kwa maelekezo, suala hili katika hali ya kawaida Kitwanga hakutakiwa kuruhusiwa kuingia bungeni,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia (TGNP), Lilian Liundi, ameipongeza hatua aliyoichukua Rais na kueleza kuwa, alichokifanya Kitwanga ni kuliaibisha bunge na Rais aliyemteua na hivyo alistahili kuondolewa.

“Kilichotokea hadi Rais anachukua maamuzi iwe kama kengele kwa Bunge… kama walikuwa hawajaweka mfumo mzuri wa kutambua ulevi basi wajiimarishe ili aibu kama hii isijirudie tena,” alisema.

Mwanasheria Chris Maina alisema kuruhusu mtu aliyelewa bungeni ni udhaifu mkubwa kwa taasisi ya Bunge .

“Bunge kukaa kimya na kumruhusu hadi anasimama mbele kujibu maswali ni udhaifu na inaonekana ni dalili kwamba hamuwezi kutetea maadili,” alisema kabla ya kumpongeza Rais kwa uamuzi aliouchukua.

Mtaalam wa Sayansi ya Siasa Profesa Mwesiga Baregu, alisema hadhani ulevi ndio sababu pekee iliyomfanya Rais amuondoe Kitwanga katika uwaziri.

Profesa Baregu ambaye pia alikuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema hoja zilizojengwa na upinzani kuhusu sakata la Lugumi nazo zitakuwa chanzo kingine cha kuondolewa kwa Kitwanga. 

Chanzo: Nipashe

google+

linkedin