5/27/16

Mkwasa amchinja kimoja Cannavaro


KOCHA wa Timu ya Taifa - Taifa Stars, Boniface Mkwasa, amemfungia rasmi vioo nahodha wake wa zamani, Nadir Haroub 'Cannavaro' baada ya kumtema moja kwa moja kwenye kikosi hicho.

Stars ilitarajiwa kuondoka leo kwenda Kenya kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Harambee Stars bila na Cannavaro pamoja na kwamba aliitwa kwenye kikosi hicho.


Beki huyo wa kati, ambaye pia ni nahodha wa Yanga, ameshikilia msimamo wake wa kustaafu kucheza Stars kama ishara ya kupinga kuvuliwa unahodha bila kushirikishwa.

Cannavaro alitangaza kujiuzulu kuichezea Taifa Stars muda mfupi baada ya Mkwasa kumpa kitambaa hicho mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika, Mbwana Samatta.

Beki huyo, aliliambia gazeti juzi kuwa hatajiunga na kambi ya Stars licha ya kocha Mkwasa kumjumuisha kwenye kikosi chake kinachojiandaa na mchezo dhidi ya Misri, Juni 4 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeona uamuzi wa Cannavaro kususa wito wa kuitumikia nchi ni utovu wa nidhamu.
Kiongozi mmoja TFF, ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwenye gazreti, ameshutumu mchezaji huyo kukosa uzalendo kwa taifa.


"Sidhani kama kuna maana tena kumwandalia mechi ya kumuaga kama ilivyofanyika kwa wenzake waliotangulia Mecky Mexime na Shadrack Nsajigwa," alisema mtoa habari huyo.

Wakati huo huo Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema jana kuwa maandalizi ya safari yamekamilika na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, Omar Walii kutoka Arusha ndiyo ataongoza msafara wenye wachezaji 23.

Lucas alisema kuwa mshambuliaji Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ataungana na timu hiyo jijini Nairobi kesho akitokea Lubumbashi.

"Timu inaondoka kesho (alfajiri), itafanya mazoezi siku mbili na Jumapili itashuka dimbani kucheza na wenyeji Harambee Stars," alisema Lucas.

Samatta anayecheza soka Ubelgiji hatakuwepo katika mchezo kutokana na kubanwa na ratiba ya timu yake, lakini atafika kuingoza Stars dhidi ya Misri.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts