5/9/16

Mpina anusa ufisadi ofisi yake

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Luhanga Mpina, amemwagiza Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa ofisi hiyo (CIA), kukagua matumizi ya Sh. milioni 773 zilizotumika katika kutekeleza miradi mitatu ya kukabiliana na mabadiliko tabianchi.
Mpina alitoa agizo hilo juzi wakati akikagua miradi hiyo katika wilaya za Bahi na Chamwino, mkoani Dodoma, ambapo alibaini miradi hiyo kujengwa chini ya kiwango kulinganisha na fedha zilizotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Alisema miradi hiyo ambayo ilikuwa ikisimamiwa na mashirika matatu yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) ambayo yalipatiwa fedha kutoka ofisi hiyo, yanatakiwa kufanyiwa ukaguzi ili kubaini matumizi sahihi.
“Nakupa wiki mbili mkugauzi wa ndani kuniletea majibu juu ya matumizi ya hizi fedha ambazo serikali imetoa kwa ajili ya wananchi wake lakini inaonekana kuna watu wamezitumia vibaya,” alisema Mpina.
Alizitaja NGOs zilizokuwa zikisimamia miradi hiyo kuwa ni TEFA iliyokuwa ikiendesha mradi wa kupunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika Halmashauri ya Chamwino, kijiji cha Machali A, ambayo ilipatiwa Sh. milioni 267.5.
Nyingine ni FECE iliyokuwa ikitekeleza maradi wa kuwezesha jamii kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia nishati ya jua katika wilaya ya Bahi kwenye vijiji vya Ibiwa na Ilindi ambayo ilipatiwa Sh. milioni 265.
Na ya tatu ni ya ECOVIC ambayo ilikuwa inaendesha mradi wa matumizi ya nishati ya jua kijiji cha Namagombo, Ukerewe ambayo ilipatiwa Sh. milioni 240.
Mpina alisema baada ya kukagua miradi miwili ambayo ipo mkoani Dodoma katika wilaya za Bahi na Chamwino, ameona kuna haja ya mkaguzi wa ndani kufanya ukaguzi wa haraka ili kubaini ubadhilifu uliofanyika.
Alisema jambo ambalo linatoa maswali ni namna ambavyo NGOs hizo zilivyoendesha miradi hiyo kwa kificho bila kuishirikisha Ofisi ya Makamu wa Rais au halmashauri husika.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts