Muswada wa bima ya afya kwa kila mtu Septemba | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

5/5/16

Muswada wa bima ya afya kwa kila mtu Septemba

MUSWADA ambao utawezesha kutungwa kwa sheria, itakayomlazimisha kila Mtanzania kujiunga na bima ya afya kwa lengo la kusaidia kuboresha huduma za afya nchini, utawasilishwa bungeni Septemba mwaka huu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Mfano cha Uchunguzi na Matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ambacho kimejengwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Ummy alisema Septemba mwaka huu, serikali itapeleka bungeni muswada utakaomtaka kila Mtanzania kuwa mwanachama wa mfuko wa bima ya afya. Alisema serikali itaongeza gharama za matibabu za papo kwa papo ili wananchi wengi wajiunge na mfuko huo.

Kwa mujibu wa takwimu za NHIF iliyoanzishwa takribani miaka 15 sasa, hadi Juni 30, 2015, Watanzania 9,914,678 sawa na asilimia 23 ya Watanzania wote (sawa na asilimia 76.6 ya lengo) walikuwa wanahudumiwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Lengo ni kufikia asilimia 50 ya Watanzania wote mwaka 2020. Waziri Ummy alisema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano yenye kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ni kuboresha huduma kwa kuzingatia uwazi, uadilifu na uwajibikaji wenye matokeo.

Aidha, Waziri huyo alihoji kwa nini NHIF isijenge hospitali kwenye wilaya 27 ambazo hazina hospitali nchini na kukawa na makubaliano ya kulipa.

Alisema kuanzia Julai 2015 hadi Machi 2016, vituo vya matibabu Mkoa wa Dodoma vimepokea jumla ya Sh bilioni 2.6 kutoka kwa NHIF kwa huduma za matibabu walizotoa kwa wanufaika 166,578.

“Wakati fedha zikiwa katika baadhi ya akaunti za vituo, dawa katika baadhi ya vituo zimeendelea kukosekana hali inayoleta malalamiko na usumbufu kwa wateja na wananchi kwa ujumla,” alisema Ummy.

Aliwaagiza NHIF, Bohari ya Dawa na Mganga Mkuu wa Mkoa na timu yake kukutana ili kubaini ni nini chanzo cha tatizo na hatua zipi zichukuliwe kulitatua kwa haraka. Pia aliagiza vituo vyote vya kutolea huduma viwe na dirisha la kuhudumia wazee.

“Hata jengo hili haliwezi kukamilika bila kuwa na dirisha la kutolea huduma kwa wazee, katika fedha za dawa ambazo rais ameongeza itafutwe namna ya kuangalia kiasi gani kinatengwa kwa ajili ya kuhakikisha wazee wanapata dawa,” alieleza waziri.

Alisema magonjwa ya wazee yanafahamika kama matatizo ya mifupa, maumivu na shinikizo.

Alisema kulingana na takwimu wazee ni asilimia 5.6 na inawezekana kutenga asilimia sita ya bajeti ya dawa kwa ajili ya wazee wakawa na uhakika wa matibabu.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema ujenzi wa kituo hicho ulianza Oktoba 31, 2009 na gharama za mradi ni Sh bilioni 6.2, ikiwa ni gharama ya jengo bila kuweka vifaa vya tiba na samani.

Konga alisema kituo hicho kitaendeshwa na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa kupitia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa makubaliano ambayo katibu tawala wa mkoa ataurejeshea mfuko gharama iliyowekeza katika ujenzi.

google+

linkedin