5/24/16

Mwenyekiti auawa akisuluhisha wanandoa

IKIWA ni siku sita tangu waumini wawili, akiwamo Imamu wa Msikiti wa Rahmani, ulioko Ibanda Relini, Feruzi Eliasi, kuuawa kinyama jinamizi la mauaji limeendelea kuuandama mkoa wa Mwanza, baada ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Bulale, Kata ya Buhongwa, Nyamagana jijini Mwanza, kuuawa kwa kupigwa risasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi


Mauaji hayo yametokea ikiwa ni wiki mbili tangu kutokea kwa mauaji ya watu saba wilayani Sengerema, hivyo kufanya kuwa tukio la tatu katika kipindi cha wiki mbili na kusababisha vifo vya watu 11 katika wilaya za Sengerema na Nyagamana.

Mauaji hayo yamemkumba mwenyekiti huyo, Alphonce Mussa (48), aliyepigwa risasi mbili na watu wasiojulikana wakati akisuluhisha mgogoro wa ndoa kati ya Neema Marangula na mumewe.

Akisimulia tukio hilo kwa majonzi huku akiangua kilio, mke wa marehemu, Getrude Henrico, alisema wakati tukio hilo linatokea hakuwapo nyumbani kwa kuwa alikuwa bustanini na alisimuliwa tukio hilo alipofika nyumbani.

Hata hivyo, mjane huyo alisema kabla ya tukio hilo, siku za karibuni waliuawa mbwa wao saba waliokuwa wanalinda mifugo, hivyo anahisi tukio hilo la mauaji ya mumewe linaendana na na kuuawa kwa mbwa hao.

“Siwezi kuzungumza kwa kina, lakini kikubwa kuna baadhi ya matukio ambayo huenda yakawa chanzo cha mauaji ya mume wangu. Nikijaribu kuangalia na matukio ya nyuma, sipati picha na hili,” alisema mjane huyo.

Naye mtoto wa kwanza wa marehemu kati ya watoto 14, Leonard Mussa, alisema baba yake alikuwa na mgogoro wa mashamba na jirani yao (jina linahifadhiwa) huku kesi ya mgogoro huo kwa sasa ikiwa mahakamani.

“Huyo jirani aliwahi kumtishia baba kuwa atamwondoa duniani, lakini siamini kama hilo linahusiana na mauaji haya ya mzee moja kwa moja,” alisema.
Mtoto mwingine, Joseph Mussa, alisema baba yake aliuawa kiuonevu kwa kuwa hakuwa na ugomvi wa mtu zaidi ya kuwindwa kutokana na kuwa na mifugo mingi.

MAJIRANI WASIMULIA

Akisimulia mkasa huo, mjumbe wa mtaa huo, Dilu Luzelela, ambaye alikuwa na Mussa wakati anauawa, alisema wauaji hao walikuwa wawili na walikuwa wanatembea kwa miguu wakiwa wamebeba mabegi mgongoni ksha kutekeleza unyama huo kabla ya kukimbilia mlimani jirani na maeneo hayo.

“Hakukuwa na ugomvi wowote, lakini kumekuwapo na matukio ya mara kwa mara ya wizi wa kawaida na uporaji katika miezi ya hivi karibuni. Hakujawahi kutokea mauaji yoyote zaidi ya kuendesha shughuli zetu na marehemu kama kawaida bila chuki wala ubaguzi wa aina yoyote,” alisema.

Luzelela alisema uhusiano kati ya Mussa na wananchi na watendaji wenzake, ulikuwa mzuri huku akichapa kazi na kukubalika na wananchi waliomchagua katika uchaguzi wa serikali za mitaa Desemba 14, 2014.

“Katuachia pengo, hatutapata mtu kama yeye. Maendeleo hayakuwapo lakini yeye alijitahidi sana na amefanikisha haya yote sasa hivi maji na umeme vimeenea mtaa wa Bulale,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mtaa huo, Sajenti (mstaafu) Samadu Kigato, alisema siku ya tukio walikuwa na Mussa kwenye kikao cha kamati hiyo ili kuimarisha ulinzi na usalama kutokana na vitendo vya wizi mtaani humo kuanzia saa 10 hadi 12 jioni, baada ya kikao walirejea nyumbani.

“Tulipofika dukani jirani na nyumba ya marehemu, aliagiza maji na soda tukanywa. Baadaye nikaenda kununua chakula, lakini wakati narudi nikasikia milio ya risasi hivyo nikawaambia wananchi wakimbie kwani hizo ni risasi za moto,” alisema Kigato.

Aliongeza kuwa baada ya wauaji hao kuondoka, walikwenda eneo la tukio na kumkuta Mussa akiwa amepigwa risasi mbili, moja ya tumboni na nyingine kifuani na kuokota maganda ya risasi ya bunduki aina ya SMG. Baada ya hapo walimbeba na kumpeleka ndani kabla ya kuagiza gari kwa ajili ya kumpeleka hospitalini lakini alifariki dunia wakiwa njiani.

Baadhi ya wananchi wa eneo hilo, walilitupia lawama jeshi la polisi mkoani Mwanza kwa kuchelewa kufika eneo la tukio, hali iliyosababisha majambazi hayo kutoroka kwa urahisi. Wameliomba jeshi hilo kuanza utaratibu wa kufanya doria za mara kwa mara.

“Matukio yanatokea mapema mno. Hawa watu hawakufika mbali kwani walikimbilia mlimani wakiwa na mabegi mgongoni, hivyo ilikuwa rahisi kwao kubadilisha nguo na kujichanganya na raia wema,” alisema Marando James.

Aidha, alisema polisi baada ya kufika eneo la tukio, walishindwa kupanda mlimani kuwatafuta wauaji hao zaidi ya kuanza kuwauliza maswali kuhusu wauaji na silaha waliyotumia na kuwataka kwenda mlimani kuwazingira watuhumiwa hao.

“Sijui walitaka kutufanya chambo, wakati wao walikuwa zaidi ya askari 10 wenye silaha, tunategemea ulinzi shirikishi na silaha zetu haziwezi kuwazuia wala kupambana na wauaji hao. Tunatumia marungu na fimbo pekee na ulinzi wetu ni wa kuzuia wizi na uporaji mdogo mdogo tu,” alisema.

KAMANDA POLISI MWANZA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alithibitisha kutokea tukio hilo juzi saa mbili usiku na kwamba Mussa ambaye wakati wa uhai wake, alikuwa akijishughulisha na biashara.

Msangi alisema Mussa alipigwa risasi kifuani na kutokea chini ya kwapa upande wa kulia. Alisema risasi hiyo ilimjeruhi mwanamke Neema Marangula (23), mkazi wa Bulale katika kiganja cha mkono wa kulia.

Kamanda Msangi alisema tuko hilo lilimkumba mwenyekiti huyo wakati akitokea katika kikao alichofanya na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mtaa wake.

“Baada ya tukio hilo, wananchi wa eneo hilo walijitokeza kwa msaada wa kumsaidia marehemu, walimchukua na kumkimbiza hospitalini kwa matibabu, lakini alifariki dunia wakiwa njiani,” alisema Msangi.

Msangi aliwaomba wananchi kushirikiana na polisi kutoa taarifa ili kufanikisha watu hao kupatikana. Mwanamume na mkewe waliokuwa wakisuluhishwa wanaisaidia polisi.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts