5/17/16

Mwingine afariki akiwa gesti Dar

 
Mwanzo wa safari yake ya mwisho ulikuwa kwenye lango la nyumba ya wageni ya Rubafu iliyopo Tabata Relini jijini hapa.
Aliingia saa 8:00 mchana juzi, lakini juhudi zake za kutoka siku iliyofuatia kuendelea na shughuli zake ziliishia kwenye lango hilo; alianguka na kupoteza maisha papo hapo.
Kati ya saa 8:00 mchana juzi na saa 2:00 asubuhi jana, mtu huyo aliyejiandikisha kwa jina la Amani Daudi, aliomba maji ya kunywa ya Sh700 na pombe kali ya kwenye pakiti, maarufu kwa jina la kiroba cha Sh1,500 na baadaye aliondoka kwa saa tatu kabla ya kurejea akiwa amelewa.
“Alikuwa amelewa sana,” alidai mhudumu wa nyumba hiyo ya wageni, Sara Mwakyaba akizungumzia hali aliyokuwa nayo Daudi wakati aliporejea usiku.
“Ilibidi nimwombe mhudumu mwenzangu aliyekuwa anaingia zamu ya usiku, amsindikize chumbani kwake.
Baadhi ya vyumba vilikuwa wazi kwa hiyo nilihofia angeweza kuingia bila kujua.”
Mhudumu mwingine aliyemsindikiza chumbani usiku, Tulia Leonard Mwakyaba alisema jana saa 2:00 asubuhi, Daudi alitoka chumbani kwake ili aondoke, lakini aliuona mwili wake ukiwa umenyong’onyea.
“Nilimwambia akae nikamtafutie supu au mtori ili anywe kabla ya kuondoka, lakini akasema hana hela,” alisema Leonard.
Wakati wakiongea, kulikuwa na mteja mwingine ambaye ni mzee wa makamo aliyempa Leonard Sh5,000 ili amnunulie supu au mtori.
Leonard alichukua hela na kutoka nje, kununua supu kwenye mgahawa uliokuwa karibu na gesti hiyo, lakini wakati anatoka Daudi alianza kumfuata na ghafla akasikia kishindo.
“Niligeuka nyuma baada ya kusikia kishindo. Kukimbia namkuta Daudi amelala chali,” alisema Leonard huku akionyoshea mkono kwenye geti alipomkuta Daudi ameanguka.
“Nilikimbia kwenda kumwita dada (Mwakyaba),”alisema.
Mwakyaba ambaye alisema tukio hilo ni mara ya kwanza kutokea Rubafu, alijaribu kumgusa Daudi kuona kama angeitikia au kujigusa, lakini hakushtuka.
“Alikuwa tayari (amefariki dunia) siku nyingi,” alisema Mwakyaba.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema chanzo cha kifo chake ni kunywa pombe kupita kiasi.
Fuime alisema marehemu alianguka kutokana na kushindwa kujihimili na akagonga kichwa sehemu ya kisogo akiwa anatoka getini.
Kamanda huyo alisema mwanaume huyo, ambaye vitambulisho vyake vinaonyesha anaitwa Steve Weston Mloli (46), alifariki akiwa njiani kwenda hospitalini na si eneo la tukio.
Mloli, ambaye mwili wake umehifadhiwa Hosptali ya Amana, ni derena na alikuwa mkazi wa Tabata Kimanga.
Hili ni tukio la pili baada ya hivi karibuni mwanamke kufariki dunia akiwa gesti kwa madai ya kulishwa sumu na mpenzi wake aliyekuwa ameongozana naye.

chanzo: Mwananchi
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts