5/4/16

Ndugai ahutubia bunge la Afrika

 

Spika wa Bunge la Tanzania , Job Ndugai 
Spika wa Bunge la Tanzania  Job Ndugai amesema ili Bara la Afrika liweze kuwa Bara lenye nguvu kiuchumi na sauti ya maamuzi duniani halina budi kujikita katika umoja na mshikamano.
Ndugai ameyasema hayo alipokuwa akilihutubia Bunge la Afrika (Pan African Parliament) leo kuwasilisha Ujumbe wa Mshikamano kwa wabunge wa Bunge hilo wakati wa Ufunguzi wa rasmi wa Mkutano wa Pili wa Bunge hilo uliofanyika Mjini Midrand Afrika Kusini.
Akizungumzia changamoto zinazolikabili bara la Afrika Ndugai amesema nchi nyingi barani Afrika zinakabiliwa na matatizo yanayolingana ambayo ni vita vya wenyewe kwa wenyewe, ugaidi, umasikini na mengineyo ambayo yanahitaji suluhisho la Pamoja kuyakabili.
“Katika dunia ya sasa ni vyema tukakabiliana na changamoto zinazotukabili kwa pamoja. Matajiri hawawezi kuepuka athari za umasikini na ukosefu wa amani. Kinachotokea eneo moja kinaathiri maeneno mengi mathalani vita vya wenyewe kwa wenyewe Somalia imesababisha wakimbizi katika maeneo mengi duniani” amesema Ndugai
Akizungumzia nafasi ya wabunge katika kupiga vita changamoto zinazolikabili bara la Afrika, Ndugai amesema wabunge wa Bunge la Afrika kama wawakilishi wa mabunge ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wanawajibu wa kutetea maslahi ya Bara la Afrika bila kujali itikadi za kisiasa, maeneo wanayotoka na mambo mengine yanayoweza kuligawa bara la Afrika.
Mapema akitoa salamu za Bunge la Lesotho, Spika wa Bunge la Nchi hiyo  Nthloi Motsamai alisifu juhudi za Mwalimu Julius Nyerere pamoja na waasisi wengine wa bara hili katika kuimarisha umoja wa Afrika na kuwataka wabunge wa Bunge la afrika kuhakikisha mawazo ya viongozi hawa ya kulifanya bara la Afrika kuwa moja yanatimia.
Katika hatua nyingine, wabunge wa Tanzania wanaowakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika walikula kiapo cha uaminifu kuwa wabunge wa Bunge hilo baada ya Bunge la Tanzania kuwachagua mapema mwezi Januari.
Wabunge hao ni pamoja na  Faustine Ndugulile, Mboni Mhita, David Silinde na  Asha Abdalah Juma.  Ndugai anatarajia kurejea nchini kesho jumatano ambapo Bunge la Afrika linaendelea na Vikao vyake hadi tarehe 13 Mei, 2016
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts