5/4/16

Padri Ahimiza Wazazi kuacha Kudekeza Watoto

 
WAZAZI na walezi wameshauriwa kuacha kudekeza watoto na badala yake wawafundishe na kuwahimiza kushiriki katika kazi za mikono ili kupata kizazi imara, chenye kuheshimu kufanya kazi.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Paroko wa Parokia ya Mt Yakobo Mkuu Mtume iliyopo Kijitonyama, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Arnold Tarimo wakati akihubiri kwenye misa ya kuadhimisha sherehe za Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Siku ya Wafanyakazi Duniani.
Padri Tarimo aliwataka wazazi wawalee watoto wao katika maadili ya kumcha Mungu na kupenda kufanya kazi kama ambavyo alifanya Mtakatifu Joseph kwa mtoto wake wa mlishi, Yesu.
Alisema wazazi wanatakiwa kuwa makini katika malezi ili vijana wao wakue katika hali ya kuweza kujitegemea, tofauti na ilivyo sasa ambapo watoto wengi wanadekezwa na hawawezi kufanya kazi kwa kisingizio cha kupendwa. Padri Tarimo alisema inashangaza mtoto anafikia umri wa mtu mzima lakini hajui kufanya kazi za nyumbani hata zile ndogo ndogo.
“Wazazi kazi yenu kubwa ni kuwafundisha watoto wenu kazi za nyumbani wanapokuwa wadogo na hao wakubwa wanatakiwa wawe wanajua kufanya kazi zote za nyumbani. “Msifikiri kuwadekeza watoto bila kufanya kazi ni kuwapenda watoto, hapana, hapo ni kuwaharibu watoto,” alisema Padri Tarimo.
Alisema mtoto anatakiwa kufundishwa kazi angali bado mdogo, kama alivyofanya Mt Joseph kwa kumfundisha mwanawe Yesu kazi za useremala hadi akakomaa.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts