5/9/16

Takukuru Yazuia Tani 154 za Sukari Dodoma

 

Zaidi ya tani 154 za sukari inayodaiwa kufichwa kwenye maghala na mfanyabiashara mkubwa wa bidhaa hiyo mkoani Dodoma zimezuiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Maofisa wa Jeshi la Polisi ili kupisha uchunguzi na endapo itabainika kuwa ilifichwa makusudi muhusika atachukulia hatua kulingana na maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.

Shehena hiyo imebainika kufuatia msako uliofanywa usiku na TAKUKURU na Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa ya uwepo wa sukari kwenye maghala hayo ambapo Mkuu wa TAKUKURU mkoani Dodoma Emma Kuhanga amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na endapo itabainika kuna hujuma ndani yake hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya muhusika.

Kwa upande wake mmoja kati ya watunza ghala aliyefahamika kwa jina moja la Samir aliyekutwa eneo la tukio wakati wa msako amekanusha kufichwa kwa sukari hiyo huku akidai kuwa inauzwa sokoni kila siku kwa utaratibu maalum.

Wakati sakata la uhaba wa sukari likiendelea kutikisa nchi nzima Jukwaa Huru la Wazalendo Tanzania limetoa tamko la kulaani wafanyabiashara wanaohujumu upatikanaji wa bidhaa hiyo huku makundi mbalimbali ya jamii yakiendelea kupaza sauti kuitaka serikali itafute suluhisho mapema kwani wanaoumia asilimia kubwa ni wananchi wa maisha ya kawaida.

Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts