5/1/16

Tanzania Yaongoza Uhuru wa Vyombo vya Habari

 

WAKATI keshokutwa ni Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema utafiti uliofanywa hivi karibuni na waandishi wa habari wasio na mipaka katika nchi 180, umebaini kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika Mashariki kwa kutunza uhuru wa vyombo vya habari.

Akizungumza bungeni jana, Nape alisema kimataifa, Tanzania imeshika nafasi ya 71 na hivyo kuwa moja ya mataifa yanayofanya vizuri duniani katika kutunza uhuru wa vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa Nape, utafiti huo ni uthibitisho dhahiri kuwa madai yanayoibuliwa na baadhi ya wabunge na wadau wengine kwamba Serikali inaminya uhuru huo, si ya kweli. “Tanzania tunafanya vizuri kimataifa na hata kwa nchi za Afrika Mashariki tumekuwa wa kwanza kwa kuhifadhi uhuru huo, hili linafuta dhana inayojaribu kujengwa ya kwamba uhuru unaminywa, hii ni taarifa ya kitafiti na si suala la kubuni,” alisema Nape.

Alisema dhana inayojengwa na baadhi ya wabunge kuwa kuna mwingiliano mkubwa kati ya Serikali na Bunge, baadhi ya wabunge kusema studio ya Bunge inaendeshwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), ni madai ya uongo.

Alifafanua kuwa studio hiyo ya Bunge inaendeshwa na Bunge na kilichofanyika ni kuomba msaada wa kitaalamu kutoka TBC, ili kusaidia studio hiyo hadi hapo Bunge litakapopata wataalamu wake.

Weka Maoni Yako Hapa
Share:

Advertisment

Habari Mpya

Follow us on Facebook

Popular Posts

Blog Archive

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger Design by Yuvinusm