5/17/16

Ugaidi Sasa Tishio Afrika Mashariki- Serikali
Nchi za Afrika Mashariki zimetakiwa kutafuta mbinu za kupambana na ugaidi ambao umetajwa kuwa tishio kubwa katika ukanda huu, katibu mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alisema jana.


Katibu huyo, Job Masima alisema hayo kwenye mkutano wa wakuu wa majeshi ya nchi za Afrika na vikosi 36 vya nchi kavu unaofanyika jijini Arusha.


“Ugaidi umekuwa ukifanyika kwa mitindo tofauti, ugaidi unaofanyika Kenya ni tofauti na unaofanyika Tanzania. Tunapokaa pamoja inatuwezesha kusoma mbinu zao tofauti kupitia uzoefu wa nchi hizi ili kujua jinsi ya kupambana nao,” alisema Masima.


Mkutano huo una lengo la kubadilishana mbinu mbalimbali za kijeshi ili kutatua changamoto zilizopo.


Pamoja na ugaidi, Masima alitaja changamoto nyingine zinazolikabili bara la Afrika kuwa ni milipuko ya magonjwa, wakimbizi, dawa za kulevya na usafirishwaji wa binadamu.


Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Masima alisema ugaidi umekuwa ni tishio kubwa hasa kwa nchi za Kenya na Tanzania ambako alisema katika mkutano huo watapata mbinu za kujua namna ya kupambana na ugaidi.


Wakati mashambulizi ya kigaidi yakitokea kwa nadta Tanzania, hali ni tofauti nchini Kenya ambako magaidi wa kikundi cha Al Shabab wamekuwa wakishambulia sehemu tofauti na kuua wananchi.


Pia alisema kukaa meza moja kwa wakuu wa makamanda wa majeshi wa nchi zote kutachochea kudumisha amani barani Afrika na kuondoa tofauti zao


“Kukaa katika meza moja kama hivi kunaondoa tofauti baina ya nchi na nchi,” alisema.


Masima alisema nchi za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto nyingi, lakini akasema mkutano huo utawezesha kupata mbinu mbadala za kupambana na matatizo hayo.


Kwa upande wake, mnadhimu mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Venance Mabeyo alisema mkutano huo ni wa faida barani Afrika kwa kuwa utawezesha kujifunza uzoefu wa kijeshi kati ya majeshi ya Afrika na majeshi ya kimarekani ambao ndio wafadhili wakuu wa mkutano huo.


Akizungumza kwenye mkutano huo, Jenerali Mark Milley wa Jeshi la Kimarekani linaloshughulikia masuala ya Afrika aliwataka wakuu hao kutatua changamoto hizo mapema kwa kuwa zinaathiri maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


‘Tuna kila sababu ya kukuza wigo wa usalama ili kuhakikisha wimbi la wakimbizi linapungua barani Afrika,” alisema Jenerali Milley.


Hata hivyo, balozi wa Marekani nchini, Mark Childress amelisifu jeshi la Tanzania kuwa mstari wa mbele kuleta amani barani Afrika na ameahidi kushirikiana nalo ili kuimarisha usalama nchini.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts