Upinzani Waanika Ufisadi Bajeti ya Makamba | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

5/3/16

Upinzani Waanika Ufisadi Bajeti ya Makamba


KAMBI ya Upinzani Bungeni imeibua kashfa ya ufisadi wa Sh. bilioni 9.24 ambazo imesema ulifanywa na vigogo wawili, mmoja aliyekuwa Ikulu wakati wa serikali ya awamu ya nne na mwingine Ofisi ya Makamu wa Rais.
Hayo yamesema jana Bungeni na Msemaji wa Kambi ya Upinzani Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Pauline Gekul.

Alisema mwaka 2009 Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF), ulikubali mradi wa kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi maeneo ya Bagamoyo, Pangani, Rufiji na Zanzibar.
Alisema dola za Marekani 225,000 zilitolewa ili kuandaa na kusambaza masuala mbalimbali ya kisera, dola 345,000 za kujenga uelewa wa mabadiliko ya tabianchi na dola 325,000 za usimamizi wa utekelezaji wa mradi na kununua vitendea kazi.
Kambi ya upinzani iliibua hilo baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, kuwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka 2016/17.
Hata hivyo, Nipashe haikuweza kuthibitisha maofisa hao waliotuhumiwa kutumia fedha hizo kinyume cha malengo yaliyowekwa.
“Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni imeshangazwa na kitendo cha serikali ya CCM kuomba fedha kwenye mwaka huu wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kufanya kazi ileile ambayo ilishatengewa fedha na wafadhili na zilishatolewa kama nilivyoainisha hapo awali,” alisema.
Alisema mradi mwingine ambao fedha zake zilishatolewa na kuliwa, kwa mujibu wa kambi ya upinzani, umejumuishwa kwenye fedha hizo zilizoombwa ni ule wa kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi jijini Dar es Salaam.
Alisema mradi huo lengo lake kuu lilikuwa kujenga ukuta wa kuzuia bahari eneo la Ocean Road na Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Alisema Desemba, 2011 Bodi ya GEF ilipitisha mradi huo wa kuisaidia Tanzania wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni tano.
“Mradi ulikuwa ukitekelezwa kupitia UNEP kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Mei 2012 hadi Aprili, 2017 na ulitakiwa kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikisha Jiji la Dar Es Salaam na Halmashauri zake,” alisema.
Alisema kuwa mradi huo ulikuwa utengeneza baadhi ya miundombinu ya majitaka ya jiji la Dar es Salaam na zilitolewa Dola 200,000 kukarabati na kuimarisha ukuta wa Bahari ulioharibika katika maeneo ya Ocean Road na Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere na zilitolewa dola za Kimarekani milioni 3.337
Alisema uhifadhi mwambao wa jiji la Dar es salaam ili kupunguza kasi ya uharibifu wa fukwe, zilitolewa dola za Marekani 35,000 kulinda matumbawe maeneo ya Dar es Salaam zilitolewa dola za Kimarekani 110,000 na kutengeneza maeneo ya ukanda wa Bahari zilitolewa dola za Kimarekani 67,500.
Alisema katika kukuza uelewa wa mabadiliko ya tabianchi na kuhuisha suala la mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya kuhifadhi maeneo ya fukwe za Dar Es Salaam zilitolewa dola za Kimarekani 235,000, na kutengeneza Mpango Kazi wa utunzaji wa mazingira ya pwani kuhimili mabadiliko ya tabinachi zilitolewa dola za Marekani Marekani 190,000.
Alisema gharama za usimamizi wa UNEP, wahandisi, waratibu na kununua vitendea kazi, zilitolewa dola 757,064.
“Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa za kina kuwa miradi hii miwili ilikumbwa na ufisadi mkubwa ambao ulikuwa ukiendeshwa baina ya Mtumishi Mmoja aliyeko katika Ofisi ya Makamu wa Rais idara ya mabadiliko ya tabia nchi akishirikiana na kigogo mmoja aliyekuwa Ikulu wakati wa utawala wa awamu ya nne katika kutafuna fedha ambazo zilikuwa zimetolewa na wafadhili.
“Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Ofisi ya Makamu wa Rais imtake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanyie ukaguzi maalumu (Special Audit) wa miradi hii miwili ya kupambana na mabadiliko ya Tabia nchi, pamoja na miradi mingine yote iliyosimamiwa na kitengo cha Mabadiliko ya tabianchi kilichopo chini ya Idara ya Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais ,Mazingira na Muungano kwani kuna majipu ya kutumbua.
“Aidha tunalishauri Bunge lisitishe kupitisha maombi ya fedha ya mradi huu kifungu 5001-idara ya mazingira hadi hapo ukaguzi maalum utakapofanyika kuhusu fedha za mradi huu ambazo zilikuwa zimetolewa na wafadhili tajwa hapo juu utakapokamilika,” alisema Gekuli.
Katika hatua nyingine serikali serikali imesema asilimia 61 ya nchi ipo katika hatari ya kugeuka jangwa.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2016/17, Makamba alisema matumizi yasiyo endelevu ya rasilimali za mazingira huleta majanga na kuhatarisha maisha ya binadamu.
“Hali na mwelekeo wa mazingira ya nchi yetu ni mbaya kiasi cha kuzorotesha jitihada za maendeleo na ustawi wa Watanzania kwa miaka mingi ijayo.
Kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea nchini, asilimia 61 ya nchi yetu inatishiwa kuwa jangwa.Kilamwaka tunapoteza hekta 372,000 au takriban ekari milioni moja za misitu,” alisema.
“Matokeo yake katika miaka 10 iliyopita nchi yetu imepoteza eneo la misitu linalolingana na ukubwa wa nchi ya Rwanda. Kasi ya upoteaji wa misitu inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka,” alisema January.
Alisema hali hiyo inatokana na matumizi makubwa ya bidhaa za misitu ambapo asilimia 90 ya nishati inayotumika nchini inatokana na misitu na kwa jiji la Dar es Salaam pekee hutumia magunia 2000,000 hadi 300,000 ya mkaa yenye wastani wa kilo 50 kwa mwezi.
Alisema kutokana na matumizi hayo yanayochangia uharibifu wa mazingira kwa sasa vyanzo vingi vya maji vimeharibika, mvua zimekuwa hazitabiriki, mafuriko na ukame umeongezeka kwenye maeneo mengi na rutuba ya ardhi imepungua.
Makamba alisema katika kukabiliana na uharibifu huo wa mazingira wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha imeandaa mkakati wa kitaifa wa miaka mitano wa upandaji na utunzaji miti utakaogharimu kiasi cha Sh bilioni 105.2.
Alisema lengo la mkakati huo ni kuimarisha na kuboresha kampeni ya upandaji miti nchini na kwa mwaka wa fedha ujao, Serikali imejipanga kuhakikisha kila kijiji, kitongoji, mtaa, kaya na kila taasisi inapewa lengo la upandaji miti.
Pamoja naserikali kuendelea kusimamia sera, miongozo na mikataba ya mazingira iliyopo, imebainisha kuwa ili kuweza kutimiza majukumu yake Mfuko wa Mazingira kwa mwaka ujao wa fedha utahitaji Sh bilioni 100.
Alisema fedha hizo zitatumika kufanya ufuatiliaji, utafiti, tathmini na uchambuzi wa hali ya uharibifu wa mazingira, kugharamia mkakati wa Serikali wa upandaji miti, kugharamia miradi ya uhifadhi wa mazingira na kusaidia jamii zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Dk. Dalaly Kafumu, alisema kamati hiyo imeitaka Serikali ihakikishe suala la mazingira linapewa kipaumbele kwa kutengewa bajeti ya kutosha.
Alisema kutokana na hali halisi ilivyo ni vyema serikali ikaendelea nautaratibu wa kuwaondoa wakazi waliojenga mabondeni ili kuepusha maafa.
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh, alisema Zanzibar imetekwa na ‘Jeshi la Tanganyika’.
“Tangu kipindi cha uchaguzi mkuu wa kwanza wa Rais na Wawakilishi hadi uchaguzi wa marudio na mpaka sasa majeshi ya JWTZ yako Zanzibar in full combat, kana kwamba nchi yetu ipo vitani.
“Kama Jeshi la Tanganyika linatumika kuulazimisha Muungano, ni dhahiri kwamba Muungano huo hauna ridhaa ya wananchi na kwa sababu hiyo hautadumu.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa rai kwa Serikali hii ya awamu ya tano kwamba, kama kweli ina nia ya kuuenzi na kuudumisha muungano basi, izingatie maoni ya wanananchi waliyoyatoa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu muundo wa Muungano ili kuwa na Muungano unaoridhiwa na wananchi wa pande zote mbili za Muungano,” alisema.
Alisema pia kuwa, kwa uchaguzi wa marudio uliofanyika Zanzibar, haikuwa mara ya kwanza mikono ya Serikali ya Muungano kuchafuka kutokana na chaguzi za Zanzibar bali imeanza toka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.
Alisema katika uchaguzi huo, CUF ilishinda lakini Serikali ya Muungano ikachagua kuibeba CCM Zanzibar na ikawa ni sehemu ya dhulma kwa Wazanzibari waliotaka mabadiliko.

google+

linkedin