Utitiri wa shule binafsi wachangamkia biashara zaidi Zanzibar | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

5/17/16

Utitiri wa shule binafsi wachangamkia biashara zaidi Zanzibar


ZANZIBAR ni kisiwa kidogo katika bahari ya hindi.Mazingira hayo yamechangia kuzifanya mamlaka husika kwamba huwezi kutembea zaidi ya kilomita tano kabla hujakuta Shule ya maandalizi, msingi au sekondari ya binafsi ama ya Serikali.
Ina wakazi wapatao 1,303,569 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012. Hata hivyo imekuwa na ongezeko kubwa la shule binafsi za maandalizi, msingi na sekondari.Hali hiyo ni tofauti na miaka 40 iliyopita kulikuwa na idadi chache ya shule hizo.
Hatua hiyo inawezekana ikawa imechangiwa na kukua kwa sekta ya elimu pia jamii kuwa na mwamko wa kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata elimu bora ambayo ni ufunguo wa maisha.
Baadhi ya watu wamekuwa wakijiuliza masuala mengi kuwa je, Uanzishwaji wa shule binafsi unachangia ongezeko la kiwango cha elimu Zanzibar?.
Siajabu Suleiman Pandu ni Mrajis wa elimu Zanzibar amekuwa na muono tofauti.
Anasema kuwa kuwa wingi wa shule binafsi anaouita kuwa ni utitiri wa shule binafsi, kwa njia moja ama nyingine umekuwa ukidumaza kiwango cha elimu Zanzibar, kwa sababu baadhi ya shule hizo hazina sifa za ufundishaji pia baadhi ya majengo yake hayapo kimuundo wa shule.
Kwa sasa Zanzibar haswa katika Mkoa wa Mjini Magharibi alisema kumekuwa na utitiri mkubwa wa Shule binafsi jambo ambalo limekuwa kero, kwani baadhi ya shule hazina hata usajili.
“Imefikia pahala sasa, mtu akiwa amejenga nyumba yake nzuri hajawa tayari kwa makaazi, basi utaona anaifanya kuwa shule wakati jengo hilo ni kwa ajili ya makaazi na halijajengwa katika ubora wa Shule,” alisema Siajabu.
Baadhi ya Shule zipo katika makaazi ya watu na wanafunzi wanakuwa hawana usalama na wakati mwengine hufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo kubakwa.
Aliongeza kusema ”unakuta jengo upande Shule na upande mwingine makaazi ya watu.Wakati mwingine unawakuta wanafunzi wanafanyishwa kazi za nyumbani wakati wa masomo kwa sababu mwalimu au mmiliki wa shule anaishi humo na upande mmoja ni eneo lake la makaazi ” alisema.
Pia alisema, baadhi ya majengo ya Shule sio imara na hayana ubora, jambo linalochangia kudumaza kiwango cha elimu Zanzibar, kwa sababu wanafunzi watakuwa hawapati elimu bora.
Shule binafsi alisema kuwa zipo nyingi sana Zanzibar kati ya hizo zipo zilizosajiliwa na ambazo hazijasajiliwa zinazoendelea kupokea wanafunzi na kutoa elimu.
Licha ya Wizara ya Elimu Zanzibar kutoa matangazo na kuwataka wamiliki wa shule kuhakikisha kuwa wanazisajili Shule zao, serikalini kupitia wizara ya elimu bado wanakiuka agizo hilo.
Kimsingi alisema ni kosa la jinai kuanzisha Shule bila ya kusajiliwa na adhabu yake ni kifungo, faini au adhabu zote mbili kwa mujibu wa sheria ya elimu ya mwaka 1982.
Alisema Shule binafsi zilizosajiliwa Zanzibar ni 426 pia zipo shule zaidi ya 90 hazijasajiliwa na zinaendelea kutoa elimu.
“Miongoni mwa Shule zilizosajiliwa baadhi yao zimekuwa zikitoa elimu nzuri na kutimiza vigezo, masharti na ubora wa shule, lakini baadhi yao hazina ubora na wala elimu inayotolewa sio bora,”alisema Mrajis wa elimu.
Alibainisha kuwa sio kama wizara ya elimu inapinga uanzishaji wa Shule binafsi, lakini inapaswa kuhakikisha Shule zinazoanzishwa zina kiwango na ubora unaotakiwa ili wanafunzi waweze kupata elimu bora.
Alisema wamiliki wa Shule hizo binafsi wamekuwa wakianzisha shule kwa malengo ya kibiashara zaidi na sasa umekuwepo ushindani mkubwa wa kibiashara katika uanzishwaji wa Shule hizo.
“Watu wamekuwa wakianzisha shule binafsi bila ya kufuata taratibu, hususan shule za Maandalizi hivyo tunawaomba wamiliki wa shule hizo kufuata taratibu kabla hatua kali hazijachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kufungiwa Shule hizo,au kufikishwa mahakamani,”alisema.
Wakati umefika sasa, kwa Wizara ya Elimu Zanzibar kuhakikisha kuwa inafuatilia elimu inayotolewa katika shule binafsi iende sambamba na shule za Serikali.
Shule zote binafsi katika ngazi ya maandalizi na msingi alisema kuwa zinatakiwa zifuate mitaala ya Wizara ya Elimu Zanzibar, lakini baadhi ya Shule hizo, hazifuati mitaala hiyo na badala yake hufuata mitaala ya Tanzania bara, jambo ambalo halikubaliki kwa ngazi ya maandalizi na msingi.
Hata hivyo alisema, Sheria ya elimu inayotumika ambayo ni ya mwaka 1984 inahitaji kufanyiwa marekebisho, kwani ina mapungufu makubwa hasa katika suala zima la uanzishwaji wa shule binafsi.
Alisema sheria hiyo haijaeleza wazi ni mtaji wa kiasi gani awe nao mtu ili aweze kuanzisha Shule binafsi na kuweza kudhibiti utitiri wa shule hizo, kwani yahitajika mikakati imara ya kuimarisha shule binafsi na sio kila mtu aanzishe shule anapojisikia kufanya hivyo.
“Tunapozikagua Shule zilizosajiliwa mwanzo unakuta nzuri zina ubora lakini ukikaa muda wa miaka mitano ukisema uzipitie tena shule hizo unakuta ubora wake umetetereka.Utakuta hakuna walimu wenye sifa za ufundishaji, hazina maabara na mambo mengine muhuimu,” alisema.
Alifahamisha kuwa, sababu zilizochangia kuwepo idadi kubwa ya Shule binafsi ni uhaba wa majengo ya Shule za Sekondari hali iliyosababisha kuwepo msongamano mkubwa wa wanafunzi darasani katika shule za Serikali hali iyoifanya wizara ya elimu itoe ruhusa ya uanzishwaji wa shule binafsi.
Lakini agizo hilo alisema, sasa linatakiwa lifanyiwe kazi ili kuhakikisha kuwa shule binafsi zinazoanzishwa zinakuwa na kiwango na ubora wa utoaji wa elimu ili kuweza kuboresha kiwango cha elimu Zanzibar.
Khamis Mohammed mkaazi wa Maungani wilaya ya Magharibi Unguja, alisema kuwa, idadi ya shule binafsi Zanzibar zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku, na baadhi ya shule hizo zipo kibiashara zaidi.
“Utakuta imeazishwa shule mpya, basi kila mzazi mwenye uwezo atampeleka mtoto wake huko, kwa kuwa shule hiyo kwa kipindi hicho, ndio inayosifika.
Lakini baada ya miaka mitatu au mitano shule hiyo hiyo inashuka sifa za ufundishaji,” alisema.
Alifahamisha kuwa, baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kuwahamisha watoto wao kutoka shule moja kwenda nyingine hali hiyo imekuwa ikiwasumbuwa watoto katika kupata elimu bora.
Alishauri kuwepo na usimamizi madhubuti katika uanzishwaji wa shule binafsi, pia kuhakikisha shule hizo zinazoanzisha hazitozi ada kubwa ya wanafunzi.
“Kitendo cha shule kutoza ada kubwa kimekuwa kikinikera sana maana mzazi unagharamia kumlipia mtoto wako ili aweze kupata elimu bora, lakini elimu inayotolewa ni ya kawaida sasa najiuliza kuna haja gani ya kutoza ada kubwa,”alisema Khamis.
Alisema ili serikali iweze kudhibiti wingi wa shule binafsi ni kuziboresha shule za serikali kuhakikisha zina walimu wa kutosha,vifaa vya kutosha vya ufundishaji,madawati na kuongeza idadi ya majengo ya shule.
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule moja ya Sekondari, Ali Khamis alisema, shule anayosoma ni ya nne kuhamia tangu alipoanza shule ya msingi.
“Hii ni shule ya nne sasa, wazazi wangu wamekuwa wakinitoa shule moja kwenda nyingine baada ya kugundua kuwa kiwango cha ufundishaji katika shule hizo, kimepunguwa basi amekuwa akinihamisha na kunipeleka shule nyingine,”alisema Ali.
Hali hiyo, alisema imekuwa ikimpa usumbufu mkubwa hata kumlazimisha kila mara akiwa shuleni ajenge mazoea mapya kutoka shule moja kwenda nyingine.
Aliongeza kwa kusema ”unapokuwa shule ya kwanza ambayo ndio umeanzia kupata elimu, unakuwa umejenga mazoea na walimu na wanafunzi wenzangu lakini uamuzi wa kunihamisha shule nyingine inaniwia vigumu.Inabidi nianze tena kujenga mazoea ya kufahamiana na walimu na wanafunzi wenzangu”.
Alisema mzazi wake anapoamua kumtoa shule moja na kumpeleka shule nyingine huwa hana jinsi kwa sababu kiwango cha ufundishaji huwa kimeshuka miongoni mwa shule alizosoma awali.
Alisema angelitamani shule aliyoanza kusoma kuanzia darasa la kwanza ndio angemalizia hadi kidato cha sita, lakini kwa sababu hana uwezo wa kujilipia ada, inabidi afuate matakwa ya wazazi wake wanapoona shule bora itakayoweza kumpatia elimu.

google+

linkedin