5/27/16

Wachina waja na suluhishi la usafiri Dar


Wakati Tanzania ikiiingia katika ‘ulimwengu’ mpya wa huduma za usafiri katika jiji la Dar es Salaam, kwa kuanzisha usafiri wa mabasi yaendayo haraka Udart, Wachina wamebuni kile kinachoweza kuwa suluhu ya usafiri katika majiji makubwa duniani.


Usafiri huo mpya ambao hauathiriwi na foleni za barabarani ni wa mabasi mapana ambayo kwa chini yanaruhusu magari kupita na kupishana bila wasiwasi wowote, huku yenyewe yakisafiri bila kulazimika kusimama kusubiri magari yapite, isipokuwa njiapanda na kwenye taa za barabarani.


Msongamano wa magari barabarani ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kusababisha maradhi, vifo, kupoteza fedha, kurudisha nyuma maendeleo na hata kuvuruga ndoa za baadhi ya watu.


Ubunifu wa China unaweza ukawa suluhisho kwa mji wa Dar es Salaam wenye changamoto ya usafiri kutokana na msongamano, hususan kwenye barabara ambazo mradi wa mabasi ya kasi haujafika.


Ili kubana matumizi ni vyema Serikali ingeamua kutumia mfumo huu wa China ambao hauna sababu ya ujenzi mpya wa barabara zaidi ya kuzikarabati.


Kadri teknolojia inavyozidi kukua kila siku katika usafirishaji, ndivyo ufumbuzi wa baadhi ya changamoto zinavyozidi kupatiwa majibu, Beijing China wao wameweza kutengeneza basi la umeme lenye uwezo wa kupita juu ya magari mengine ili kupunguza msongamano wa magari barabarani.


Basi hilo lina uwezo wa kubeba watu 1,200 kwa mara moja, linatajwa kuwa ufumbuzi wa msongamano wa magari barabarani. Pia, lilifanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza wiki iliyopita.


Magari madogo yenye urefu wa futi 6.6 yanapita chini ya gari hilo jambo ambalo linaelezwa hupunguza idadi ya magari kwenye msongamano. Basi hilo linalotumia umeme na inaelezwa kwamba, linaweza kusafiri kilomita 60 kwa saa moja.


Utengenezaji wa basi hilo moja umegharimu kiasi cha Yuan 500 milioni sawa na Dola 74.1 za Marekani. Mabasi hayo yanapunguza msongamano wa foleni kwa asilimia 20 mpaka 30.


Mkurugenzi wa Kampuni ya China TBS Limited ambayo imetengeneza mabasi hayo, Shenzhen Hashi alisema walitumia mwaka mmoja kutengeneza basi moja na walianza mwaka 2010.


Kama ulivyo usafiri wa treni ikipita kwenye barabara zenye maungano ni lazima ipige honi kwa ajili ya kuashiria magari yasimame, basi kwa magari haya yanapopita kwenye barabara hizo yenyewe hupiga king’ora.


Afrika Kusini


Inatumia zaidi ya mabasi hayo pia inatumia usafiri wa treni ya Gautrain, inatumia dakika zisizozidi thelathini kwa safari ya umbali huo wa kilometa 54.


Kwa gari mwendo wa safari hiyo huchukua hadi saa mbili wakati watu wengi wakiwa wanatumia usafiri kwenda ama kurejea kazini.


Lakini kwa kufika Pretoria, inaonekana itatumiwa zaidi na wasafiri wa kawaida nchini Afrika Kusini ili kukabiliana na foleni katika barabara yenye magari mengi nchini humo.


Ethiopia


Ni nchi ya Afrika ambayo inachangamoto la msongamano wa magari hivyo imeanza kutumia usafiri wa treni za mwendo kasi kubeba abiria na kurahisisha usafirishaji wa watu kwenye mji mkuu wa Addis Ababa.


Treni hizi za umeme zina uwezo wa kuhudumia abiria 15,000 ndani ya dakika 60 na treni moja inaweza kubeba abiria 286 kwa wakati mmoja.


Tanzania ni nchi ya pili Afrika kuwa na magari ya mwendo kasi ikifuatiwa na Ethiopia huku Afrika Kusini ikiwa ya kwanza.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts