5/1/16

Wakuu wa Mikoa Marufuku Bungeni

 
Mkakati Rais John Magufuli kubana matumizi umewashukia wakuu wa mikoa, makatibu tawala na watendaji mbalimbali wa ngazi ya mkoa baada ya Ofisi ya Rais, Tamisemi kuwazuia kuhudhuria vikao vya bajeti ya wizara hiyo bungeni mjini Dodoma ili kubana matumizi.
Uamuzi huo ni tofauti na mikutano iliyopita ya bajeti ambayo watendaji hao walikuwa wakijazana bungeni huku wakitumia magari na kukaa hotelini kwa takriban wiki moja.
Tangu kuanza kwa mjadala wa bajeti hiyo Alhamisi iliyopita, ukumbi wa wageni uliopo ndani ya Bunge ulikuwa tupu na huku Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene akisema kuanzia sasa wakuu hao hawatashiriki Bunge la bajeti lengo likiwa ni kubana matumizi.
Hata zile nderemo zilizokuwa zikitawala nje ya viwanja vya Bunge baada ya bajeti kupitishwa, zikiambatana na sherehe ya kupongezana katika kumbi mbalimbali hivi sasa hazipo.
Idadi ya wageni katika mkutano wa bajeti imepungua tofauti na miaka ya nyuma walipokuwa wakijaza kumbi.
Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Bunge walisema wameona tofauti kubwa kati ya mkutano huu wa bajeti na zilizopita kwani katika eneo lilipo karibu na geti ya Hoteli ya Fifty Six lilikuwa likijaa magari ya wakuu wa mikoa.
“Miaka mingine hapa ungekuta magari yamefurika hadi eneo la kuegesha hakuna. Ukifika umechelewa inabidi kwenda kuegesha Veta au upande wa pili wa barabara inayoelekea Morogoro,” alisema mmoja wa madereva ambaye hakutaka jina lake liandikwe.
Simbachawene alisema huo ni mkakati wa kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kubana matumizi.
Alisema katika bajeti hii waliokuja ni maofisa wa wizara ambao hawazidi watu 10 .
“Hii yote ni kwenda na dhamira ya Rais ya kubana matumizi ya Serikali zamani alikuwa akija RC (Mkuu wa Mkoa), Ras (Katibu Tawala), na mchumi na hawa wote wanakuwa na magari kati ya moja hadi matatu,” alisema: “Safari hii wamekuja watumishi wa wizara, wakuu wa mikoa nilimalizana nao kule Dar es Salaam wabaki mikoani kwao wafanye kazi zao.”

Wabunge waunga mkono
Akizungumzia hatua hiyo, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema watumishi hao hawakuwa na kazi ya kufanya kwa kuwa bajeti zinazojadiliwa ni za wizara na si za mikoa.
“Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kubana matumizi na hili ni jambo zuri, walikuwa wanatumia fedha nyingi kugharamia mafuta ya magari wanayokuja nayo hili ni wazo zuri,” alisema Kangi.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cecilia Pareso alisema wapinzani wamekuwa wakilipigia kelele jambo hilo kwa muda mrefu: “... Serikali sasa wamesikiliza kilio chetu.”
Aliitaka Serikali kusikiliza ushauri unaotolewa na vyama vya upinzani katika kubana matumizi na utekelezaji wa masuala mbalimbali ya nchi.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts