5/16/16

Wananchi watishiwa kwa bastola wakiandaa ujenzi wa sekondari


MAANDALIZI ya ujenzi wa Shule ya Sekondari katika mtaa wa Kilimahewa Juu kata ya Wazo Manispaa ya Kinondoni, yaliingia dosari baada ya juzi kuibuka vurugu kubwa zilizosababishwa na mwananchi anayedai eneo hilo ni lake, kuchomoa bastola kuwataka wananchi wasiendelee na maandalizi ya ujenzi huo.
Kitendo hicho kilitokea baada ya wananchi hao kufika eneo hilo na kuanza kufyeka na kukata miti tayari kwa maandalizi ya ujenzi wa shule hiyo.

Huku wakiwa `bize' na shughuli hiyo, ghafla ailibuka mwananchi huyo aliyefahamika kwa jina moja la Costa na kuwazuia wananchi hao kuendelea na shughuli maandalizi ya ujenzi wa shule hiyo akidai kuwa ni eneo lake.

Hata hivyo, wananchi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi wa shule hiyo, Joseph Kabengwe, walipinga kauli hiyo na kumueleza kuwa aende Manispaa akachukue fedha zake ambazo amekuwa akigoma kwenda kuchukua wakati wenzake watatu walishakuwa na kuachia maeneo yao ambayo yanatumika kujenga shule ya sekondari.

Hata hivyo, Costa alidai kuwa hakuna barua aliyotumiwa na Manispaa kwa ajili ya kumlipa fidia, hivyo eneo lake liachwe hivyo hivyo hadi atakapolipwa.

Kufuatia kauli hiyo, ndipo wananchi walipoanza kumzonga, kitendo kilichomfanya Costa achomoe bastola yake aliyokuwa ameiweka kiunoni na kutishia kufyatua risasi juu.

Licha ya kuchomoa bastola hiyo na kuilekeza juu kama anataka kufyatua risasi, lakini wananchi waliendelea kumzonga wakitaka awaue wote.

Hata hivyo, mwananchi huyo alipoona wananchi hawatishiki na bastola yake, aliamua kuingia kwenye gari lake lenye namba za usajili T739 BGJ Toyota Land Cruser na kuondoka katika eneo hilo.

Baada ya mwananchi huyo kuondoka eneo hilo, wananchi waliendelea na shughuli yao ya kufyeka na kukata miti.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Kuruthum Kazema, aliyekuwapo eneo la tukio, alisema wanachokifanya hapo kina baraka zote za uongozi wa Manispaa ya Kinondoni.

Kazema alisema kabla ya kuanza shughuli ya kulisafisha eneo hilo, alifuatilia Manispaa ili kujiridhisha kuhusu uhalali wa eneo hilo kama ni kweli lilitengwa kwa ajili ya matumizi ya shule.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts